Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rufani vigogo Chadema kusikilizwa na warufani, mawakili pande husika

CHADEMATZ Rufani vigogo Chadema kusikilizwa na warufani, mawakili pande husika

Wed, 29 Apr 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imesema rufani ya vigogo wanane wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) akiwamo Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe, dhidi ya Jamhuri itasikilizwa na warufani na mawakili wa pande zote mbili na haitaruhusu wasikizaji.

Rufani hiyo ilitajwa jana na Jaji Mfawidhi Lameck Mlacha, huku akibainisha kuwa itasikilizwa mbele ya Jaji Ilvin Mgeta wa mahakama hiyo.

"Siku ya kusikiliza rufani hii wataruhusiwa kuingia warufani na mawakili wao tu. Wasikilizaji wengine hawataruhusiwa kutokana na kuepusha mkusanyika wa kujilinda na maambukizo ya corona," alisema Jaji Mlacha.

Awali upande wa walalamikiwa ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon na Salim Msemo, ulidai kuwa rufani hiyo imepangwa kwa ajili ya kutajwa na kupanga tarehe ya kusikiliza. Upande wa walalamikaji uliongozwa na Wakili Peter Kibatala.

Mbowe na wenzake wamekata rufani Mahakama Kuu kupinga hukumu ya kulipa faini ya jumla ya Sh. milioni 320 au kwenda jela miezi mitano kwa kila kosa.

Rufani hiyo iliyosajiliwa kwa namba 76 mwaka huu imewasilishwa na wakili wa walalamikaji, Peter Kibatala ikiwa na sababu 14.

Kwa mujibu wa hati ya rufani, walalamikaji wanadai kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam ilighafilika kisheria kuwatia hatiani Mbowe na wenzake kwa sababu haikuchambua ushahidi wa Jamhuri wakati wa kuandika hukumu hiyo.

Hoja nyingine, Mahakama ya Kisutu katika hukumu yake haikuonyesha sababu zilizofanya washitakiwa kutiwa hatiani.

"Upande wa Jamhuri ni jukumu lao kuthibitisha makosa bila kuacha shaka na kwamba si kazi ya mshitakiwa kujitetea" ilieleza sehemu ya hoja za walalamikaji.

Hoja nyingine inadai kuwa Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba hakutilia manani utetezi wa washitakiwa akiwamo Esther Matiko na John Mnyika katika ushahidi wa Jamhuri hakuna ulipoeleza kama washitakiwa walikuwapo kwenye tukio.

Pia mahakama inadaiwa ilighafilika kisheria kuwatia hatiani washitakiwa katika shitaka lililokuwa na mashitaka manne ndani yake ikiwamo kufanya maandamano, kusababisha kifo cha Akwilina na kusababisha Askari polisi wawili kujeruhiwa.

Hoja nyingine kwamba mahakama ilipokea CD iliyoonyesha maandamano ya washitakiwa kinyume cha sheria na kwamba utaratibu wa kisheria haukufuatwa kielelezo hicho kilipokelewa kiholela.

Mbali na Mbowe, Matiko, Mnyika washitakiwa wengine ni, Mchungaji Peter Msigwa, Halima Mdee, John Heche, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu, na Mbunge wa Bunda , Esther Bulaya.

Katika kesi ha msingi, Mbowe na viongozi wenzake walishtakiwa kwa mashitaka 12 ya uchochezi na moja la kula njama.

Mashitaka 12 yaliyokuwa yakiwakabili, katika shitaka la kula njama, wanadaiwa kati ya Februari Mosi na 16, 2018 wakiwa Kinondoni Dar es Salaam kwa pamoja walikula njama na wengine ambao hawapo mahakamani kwa kutenda kosa la jinai na kuendelea na mkusanyiko isivyo halali na kusababisha chuki na uchochezi wa uasi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live