Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rufaa dhamana kina Mbowe leo ni kusuka au kunyoa

44322 PIC+MBOWE Rufaa dhamana kina Mbowe leo ni kusuka au kunyoa

Fri, 1 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya Rufani leo inatarajiwa kutoa hatka ya dhamana ya mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na mhazini wa baraza la wanawake wa chama hicho (Bawacha), Esther Matiko wakati itakapotoa uamuzi wa rufaa ya mkurugenzi wa mashtaka (DPP).

Hukumu hiyo ndiyo itakayotoa ama mwanga kwa wanasiasa hao kuendelea na safari ya mapambano ya kurejea uraiani kwa taratibu za kisheria kupitia rufaa yao iliyosimama Mahakama Kuu ya kupinga kufutiwa dhamana, ama kuzima matumaini yao na hivyo kuendelea kuishi mahabusu wakati kesi yao ya msingi ikiendelea.

DPP alikata rufaa hiyo Mahakama ya Rufani akipinga uamuzi wa Mahakama Kuu iliyokubali kuendelea na usikilizwaji wa rufaa ya wabunge hao ya kupinga uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwafutia dhamana.

Mbowe na Matiko walifutiwa dhamana na aliyekuwa Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri Novemba 23 mwaka huu baada ya kushindwa kufika mahakamani kwa ajili ya kesi ya jinai inayowakabili mahakamani hapo pamoja na viongozi wengine saba wa chama hicho.

Kufuatia uamuzi huo, Mbowe ambaye ni mbunge wa Hai mkoani Kilimanjaro na Matiko mbunge wa Tarime Mjini, walikata rufaa Mahakama Kuu siku hiyohiyo wakipinga kufutiwa dhamana yao chini ya hati ya dharura sana.

Hata hivyo, DPP aliweka pingamizi la awali akiiomba Mahakama hiyo isiisikilize rufaa hiyo pamoja na mambo mengine akidai haina mamlaka kwa kuwa ilikuwa inakiuka matakwa ya sheria.

Jaji Sama Rumanyika alitupilia mbali pingamizi hilo DPP badala yake akaamua kuendelea na usikilizwaji wa rufaa hiyo ya kina Mbowe, lakini kabla ya kuanza kuisikiliza DPP akakimbilia Mahakama ya Rufani kukata rufaa kupinga uamuzi huo.

Katika rufaa hiyo DPP kupitia kwa jopo la mawakili wa Serikali aliiomba Mahakama hiyo itengue uamuzi wa Mahakama Kuu wakidai ilikosea kukubali kusikiliza rufaa hiyo ya kina Mbowe kwa kuwa ilikuwa inakiuka matakwa ya kisheria na kwamba hawakupewa fursa ya kutosha kusikilizwa kabla ya kufikia uamuzi.

Iwapo Mahakama ya Rufani leo itakubaliana na hoja za rufaa ya DPP, basi itatengua uamuzi wa Mahakama Kuu na hivyo rufaa waliyoikata kina Mbowe itakuwa imekufa na kuendelea kusota mahabusu hadi pale kesi yao ya msingi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu itakapotolewa hukumu.

Kama Mahakama ya Rufani katika uamuzi wake itazikataa hoja za rufaa ya DPP na ikakubaliana na uamuzi wa Mahakama Kuu (kuendelea na usikilizwaji wa rufaa yao), itaamuru Mahakama Kuu iendelee na usikilizaji huo hivyo watasubiri wapangiwe tarehe kisha Mahakama hiyo itatoa uamuzi.



Chanzo: mwananchi.co.tz