Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ripoti ya Kikosi Kazi na mapokeo yake

Kikosiipiic Kaziii Mikutano Ripoti ya Kikosi Kazi na mapokeo yake

Mon, 24 Oct 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati vyama vya NCCR- Mageuzi, CUF na ACT- Wazalendo, vikisema vimeipokea ripoti ya kikosi kazi cha kuratibu maoni ya wadau kuhusu demokrasia ya vyama vingi nchini, Chadema kimepinga mapendekezo yaliyotolewa, huku kikiitaka Serikali kueleza gharama ambazo kikosi kazi kimetumia.

Akizungumza jijini hapa, wakati akichambua mapendekezo yaliyotolewa na kikosi kazi hicho, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alisisitiza kwamba wataendelea kudai mabadiliko ya Katiba na kuondolewa kwa zuio la mikutano ya hadhara nchini.

Juzi, mwenyekiti wa kikosi kazi, Profesa Rwekaza Mukandala alimkabidhi Rais Samia Suluhu Hassan ripoti yao baada ya kufanya kazi kwa kipindi cha miezi 10, wakichambua maoni na mapendekezo ya wadau kuhusu demokrasia ya vyama vingi na madai ya Katiba.

Katika ripoti hiyo, kikosi kazi kimetoa mapendekezo 18 kwa Serikali, ikiwemo kuruhusiwa kwa mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa, mchakato wa katiba mpya kuendelezwa na ruzuku kwa vyama vyote vya siasa.

Hata hivyo, Rais Samia alitoa angalizo kwamba mapendekezo hayo siyo amri kwa Serikali kuyatekeleza.

Akizungumza na vyombo vya habari jana, Mnyika alisema kuundwa kwa kikosi kazi ni matumizi mabaya ya fedha za umma, kwa sababu maoni ya wananchi yaliyokusanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba yapo na hayajafanyiwa kazi.

“Hakukuwa na sababu yoyote ya kuunda kikosi kazi, badala yake Rais, kwa sababu alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, ana ufahamu juu ya makabrasha haya, ilikuwa ni kiasi cha Serikali kurudi kwenye makabrasha haya (ripoti za Jaji Warioba), kuyapitia na kuendeleza mchakato wa mabadiliko ya katiba,” alisema Mnyika huku akionyesha vitabu hivyo.

Kuhusu mikutano ya hadhara, Mnyika alisema walikuwa na matumaini kiasi baada ya kusoma makala ya Rais Samia siku ya demokrasia duniani Septemba 15, aliposema jambo hili angelitolea mwelekeo baada ya kupokea ripoti ya kikosi kazi.

Alisema walivuta subira pamoja na kukumbusha mara kwa mara wakitumaini kwamba jambo hilo litatatuliwa baada ya kikosi kazi kukamilisha kazi yake, hata hivyo jambo hilo halijapata ufumbuzi, huku akiitaka Serikali kuondoa zuio la mikutano ya hadhara.

“Kwa bahati mbaya, kauli ya Rais imekwenda kuendeleza uvunjifu wa Katiba, uvunjifu wa sheria,” alisema Mnyika.

Alisema wanaendelea kusisitiza maelekezo ya Kamati Kuu ya Chadema iliyokaa Septemba 17 na 18 kwa ngazi zote za chama kuendelea na maandalizi ya mikutano ya hadhara na katika tarehe itakayotangazwa, wataendelea kufanya mikutano ya hadhara kwa mujibu wa sheria.

Katiba Mpya

Kuhusu pendekezo la kikosi kazi la kuundwa kwa jopo la wataalamu litakaloandaa rasimu ya mwisho ya Katiba na kuipeleka bungeni kwa ajili ya kupitishwa, Mnyika alisema hiyo inaonyesha nia isiyo njema ya kikosi kazi.

“Bunge la sasa ambalo kila mtu anajua lilivyopatikana, eti ndiyo linakwenda kukabidhiwa kazi ya kwenda kupitia rasimu ya tatu ya Katiba.

“Jambo hili halipaswi kukubalika kwa wote, ni lazima kupaza sauti kuikataa ripoti hii ya kikosi kazi, kwa sababu ikiruhusiwa tu ni sumu ya kwenda kuua mchakato wa Katiba mpya au kuuvuruga mchakato huo katika nchi yetu,” alisema katibu mkuu huyo.

Kuhusu hoja ya mjadala wa kitaifa ili kuleta maridhiano ya kitaifa, Mnyika alisema inapaswa kujengewa muundo, uratibu na utaratibu wa kisheria ili kupata mwafaka na maridhiano.

“Utaratibu uliopendekezwa na kikosi kazi ni utaratibu mbovu, usiokuwa na ratiba, usiokuwa na utaratibu, usiokuwa na muundo mwafaka wa kujenga mwafaka wa kitaifa,” alisema Mnyika.

Vyama vingine vyafunguka

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu alisema wamepokea mapendekezo ya kikosi kazi lakini wanataka ripoti hiyo iwekwe wazi na Serikali ifanyie kazi mapendekezo.

“Tumepokea mapendekezo ya kikosi kazi. Rai yetu, mapendekezo yawekwe wazi ili watu waisome, kuichambua na kuielewa. Tunachotaka sasa ni Serikali iweke ratiba ya utekelezaji ili tuone mabadiliko ya sheria zilizotajwa ikiwamo mchakato wa Katiba kuanza,” alisema Ado.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, Joseph Selasini alisema kazi iliyofanywa na kikosi kazi kwa miezi 10 sio ndogo na wanamuomba Rais katika ripoti hiyo kuanza na yale mambo yanayolalamikiwa na wananchi.

Alisema kazi ya kutafuta demokrasia ni kubwa, na Rais amesema amepokea ripoti hiyo lakini hakuna haja ya kuiharakisha, ili kutoa nafasi kwa taasisi nyingine ziweze kuichambua.

“Sisi hatuna mgogoro na kazi iliyofanywa na kikosi kazi, wamefanya kazi kubwa, haiwezekani kwa miezi tisa tuseme hakuna kazi iliyofanyika,” alisema Selasini.

Naye Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa CUF, Mohamed Ngulangwa alisema mwanzoni watu wengi walikosa imani na kikosi kazi kwa kuwa kilikuwa chini ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, lakini walipata imani baada ya kuitwa kikosi kazi cha Rais.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live