Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rais Samia atoa mwelekeo 2024

Samiaa Ikulu E Rais Samia atoa mwelekeo 2024

Mon, 1 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Rais Samia Suluhu Hassan ametoa mwelekeo wa Serikali kwa mwaka 2024 na kubainisha matukio muhimu ambayo Taifa linayatarajia ikiwemo uchaguzi wa Serikali za Mitaa na uboreshaji wa daftari la wapigakura.

Rais Samia alieleza hayo jana wakati wa hotuba yake kwa Taifa na kueleza mambo yaliyofanyika mwaka 2023 na kuhitimisha na mwelekeo wa Serikali kwa mwaka mpya 2024.

Akizungumzia mwelekeo huo, Rais Samia alisema mwaka 2024, kuna maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano pamoja na miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar. Alisema matukio hayo ni chachu ya kuendelea kudumisha umoja wa kitaifa na kuimarisha ustawi wa jamii.

Pia alisema uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni tukio jingine linalolitarajiwa kwa tarehe itakayotangazwa na mamlaka husika.

“Nitoe rai kwa Watanzania kushiriki uchaguzi huo ili tuchague viongozi wanaotufaa,” alisema Rais Samia.

Alibainisha kwamba mwaka huu pia wataendelea kuongeza tija na kupunguza gharama za uzalishaji kwa wakulima na kuhakikisha usalama wa chakula pamoja na kuendeleza programu ya Jenga Kesho iliyo Bora (BBT).

Aliongeza kuwa wataanza kutekeleza miradi ya kuuza na kukodisha kwa bei ya ruzuku zana za kilimo kwa wakulima ikiwamo matrekta.

Rais Samia alieleza Serikali itaendelea na mageuzi katika sekta mbalimbali ikiwemo uendeshaji wa mashirika ya umma na taasisi, lengo likiwa kuongeza ufanisi na tija.

“Tutaimarisha pia utekelezaji wa sera ya elimu ili kuhakikisha tunaandaa watoto wetu kwa mazingira ya sasa. Vilevile, tutaendelea na mchakato wa kuandika Dira mpya ya Maendeleo,” alisema Rais Samia.

Kiongozi huyo alieleza mwaka huu pia kwa mujibu wa sheria, wataboresha daftari la kudumu la wapigakura, hivyo kutoa wito kwa wote wenye sifa wajitokeze pindi shughuli hiyo litakapotangazwa na mamlaka husika.

Suala jingine lililotiliwa mkazo na Rais Samia ni umuhimu wa kampuni changa (StartUps) kwa Taifa. Alisema Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi tanzu za kampuni changa na kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa ustawi wake.

“Pamoja na mikutano mingine, tutakuwa wenyeji wa kilele cha nchi 25 za Afrika zinazozalisha kahawa,” alieleza Rais Samia katika hotuba yake.

Katika kuendelea kujenga uhimilivu na uwezo wa kukabiliana na majanga, ikiwemo majanga ya moto, Rais Samia alisema Serikali itachukua hatua za kulijengea uwezo zaidi Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na taasisi nyingine zinazoshirikiana nazo, ili kujenga uwezo wa kukabiliana na majanga ikiwemo majanga ya moto.

Kwa upande wa michezo, alisema Tanzania itakuwa mwenyeji mwenza wa michuano ya kombe la Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN).“Hii ni fursa kubwa ya kibiashara tuichangamkie.”

“Mwaka 2023 ulikuwa wa mageuzi na mwaka 2024 utakuwa ni wa utekelezaji na matokeo zaidi. Natoa rai kwa wananchi wenzangu kuazimia kubadilika, kila shughuli halali tunayoifanya tuifanye kwa bidii, maarifa na uadilifu na In shaa Allah, Mwenyezi Mungu atabariki kazi za mikono yetu,” alisema Rais Samia.

Agizo kuanza SGR

Wakati huohuo, Rais Samia alieleza kukerwa na kuahirishwa mara kwa mara kuanza kwa safari za treni ya kisasa kati ya Dar es Salaam na Dodoma.

“Nimekuwa nikisikia mabadiliko ya tarehe za kuanza kwa safari za treni na kwa kweli, wananchi wamechoshwa na vijisababu, wanataka kuona reli ikifanya kazi. Sasa, naelekeza ifikapo mwisho mwa Julai 2024, safari kati ya Dar es Salaam hadi Dodoma zianze,” alisema Rais Samia.

Alieleza ujenzi wa vipande vya kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro na Morogoro hadi Makutupora vimefikia zaidi ya asilimia 90. Aliongeza kuwa wamepata udhamini wa Benki ya Maendeleo Afrika utakaowezesha uendelezaji wa kipande cha Tabora-Kigoma na Uvinza-Musongati.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live