Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rais Samia alivyovunja makufuli ya kisiasa

Rais Samia Kukataa Njombe Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania

Thu, 11 Aug 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Mwanazuoni wa Marekani, Karen Franklin (PhD), mwaka 2013, alitoa andiko lenye kichwa: “The Best Predictor of Future Behavior Is Past Behavior.” – “Mtabiri Bora wa Tabia Zijazo ni Tabia Zilizopita.”

Wanahistoria wenyewe hunena kwa ufupi kuwa “historia hufundisha matukio yaliyopita na kuwezesha utabiri wa yanayofuata”. Safari ya miaka 30 ya demokrasia Tanzania inaweza kutumika kutabiri mingine 30 ijayo.

Julai 1992 mpaka Julai 2022 ni miaka 30 iliyotimia. Ndicho kipindi mfumo wa vyama vingi vya siasa ulizaliwa upya, ukalelewa na kukua. Ndani ya miongo mitatu ya nchi kuchipua na kukua kidemokrasia, mengi yametokea.

Zigawe awamu; mwaka 1992 mpaka 1995, kilikuwa kipindi cha utambulisho wa mfumo. Kuzaliwa kwa vyama, kutambaa na kuanza kutembea kwa kuchechemea. Mwaka 1995, ulifanyika Uchaguzi Mkuu wa kwanza kuhusisha vyama vingi, Tanzania ikiwa dola huru.

Tafsiri Uchaguzi Mkuu 1995 kama kipimo cha mtoto aliyezaliwa mwaka 1992, je, ameshaota meno ya kung’ata? Ukweli ni kuwa Uchaguzi 1995 ulikuwa sawa na mapambano ya mtoto mdogo na mzazi.

Mwaka 1995 kwenda 2005 ilikuwa awamu ya kuzoea mfumo na vyama vya upinzani kujitegemea. Hapa ndipo vyama vilivyozaliwa kati ya mwaka 1993 na 1995, vilitambua kuwa kazi ya siasa sio ya lelemama.

Mwaka 1992 mpaka 1995, ni kipindi cha mtoto na kijiko chenye chakula mdomoni. Wakati huo vyama vyote vya siasa vilipewa ruzuku ili kujiendesha. Vilidekezwa. Mwaka 1995 hadi 2005, muda wa kula kwa urefu wa kamba. Vyama vyenye wabunge na vilivyopata asilimia nzuri za kura kwenye uchaguzi ndivyo vilianza kupewa ruzuku.

Mwaka 2005 mpaka 2015 ni kipindi cha ukuaji mkubwa wa demokrasia ya vyama vingi. Huu ni wakati ambao haiba za wanasiasa wa upinzani zilijengeka kutokana na uwezo wa kujenga hoja hasa bungeni na agenda ya ufisadi.

Marekebisho ya kanuni za Bunge mwaka 2007, zilizoweka sharti la kamati za kudumu za Bunge kuongozwa na wapinzani, zilikuza sura ya uwajibikaji na ukuaji wa demokrasia ya vyama vingi.

Hiki ndicho kipindi vyama vya upinzani vilijenga kuaminika kwa sehemu kubwa ya umma na kutengeneza wabunge wengi hadi kufikia theluthi moja mwaka 2015. Ni wakati ambao CCM walionekana kutumia msuli mkubwa kubaki madarakani.

Julai 2016 mpaka Machi 17, 2021, ilikuwa awamu ya giza. Mfumo wa vyama vingi vya siasa ulioonekana umeshakomaa, ghafla ulitiwa ulemavu. Taifa lilihama kutoka kufanya siasa na kuishi chuki na uhasama.

Uchaguzi Mkuu 2020 ukageuka kaburi la demokrasia. Machi 19, 2021 hadi Julai 2022, ni kipindi cha tabasamu la demokrasia. Maumivu na machozi yaliyoletwa na siasa za chuki, yalifutwa, faraja ikaingia, kisha matumaini mapya yamejengwa. Mfumo wa demokrasia ya vyama vingi, unavuka miaka 30 kwa matumaini na matarajio chanya. Hata hivyo, umepitia miongo mitatu yenye sura anuwai ambazo zinatosha kuitazama miaka mingine 30.

Kwa nini sura anuwai?

Kitabu cha Profesa wa Sayansi ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Chuo Kikuu cha Southern California, Gerardo Munck, kinachoitwa “Modes of Transition and Democratization” – “Miundo ya Mpito na Usimikaji Demokrasia”, kinaweza kutusaidia kufahamu kwa nini miaka 30 imebeba sura anuwai.

Hasi na chanya, ustaarabu wa kisiasa na husuda, uhuru wa vyama na ukandamizwaji, huruma ya viongozi wenye dola na ubabe, yote hayo yalijiri miaka 30, itakuwaje miongo mitatu baadaye? Jibu linaweza kupatiwa ubashiri.

Ndani ya kitabu cha “Modes of Transition and Democratization”, Munck akishirkiana na mwanazuoni mwenzake, Carol Leff, ukurasa wa 356 na 357, wanaandika dhana ya Mapinduzi kutoka Juu (Revolution from Above), kama ilivyotokea Bulgaria. Ni dhana hii inayovifanya vyama vya upinzani nchini kuimarika na kupepesuka tangu mwaka 1992. Chama cha Kikomunisti nchini Bulgaria, kilifanya mapinduzi ya kidemokrasia kutoka juu mwaka 1989. Chenyewe kikiwa kinatawala, kikaamua kuanzisha mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Kwa kuwa Komunisti ndio kilianzisha vyama vingi, kikawa na fursa ya kuchora ramani ya jinsi ambavyo siasa zinapaswa kuendeshwa. Hivyo, chenyewe kikajipa uzazi na ulezi wa mfumo mzima na vyama. Baada ya kuanzisha mfumo wa vyama vingi, Komunisti kilijibadilisha jina na kuwa Chama cha Kijamaa (Bulgaria Socialist Party ‘BSP’). Kwa mujibu wa Munck na Leff, mapinduzi kutoka juu yalifanya BSP, kiingie kwenye uchaguzi wa mwaka 1990 kikiwa imara, hivyo kushinda.

Kama BSP kutoka Komunisti Bulgaria, ndivyo ilivyo Tanzania na CCM. Pamoja na kuwepo vuguvugu kadhaa za kudai vyama vingi, lakini CCM walihodhi mchakato, wakaitisha maoni, ripoti ikaonesha asilimia 80 walitaka kuendelea na chama kimoja.

Rais wa Pili wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi (CCM), ndiye aliyeteua tume ya kukusanya maoni ambayo iliongozwa na aliyekuwa Jaji Mkuu, Francis Nyalali. Ripoti ilipowekwa wazi, CCM ndio wakavaa ushujaa wa kuipeleka nchi kwenye mfumo wa vyama vingi.

Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, akiwa bado Mwenyekiti wa CCM, alisimama mstari wa mbele kuwa lazima mabadiliko yatoke. Akatoa angalizo kuwa “ni vizuri kukubali kubadilika kabla ya kubadilishwa”.

Hata baada ya kuachia kiti cha uenyekiti wa CCM, Mwalimu Nyerere, aliendelea kupigania mabadiliko ya mfumo wa vyama vingi. Na alitumia sehemu kubwa ya hoja zake kukishawishi Chama Cha Mapinduzi kikubali kubadilika kabla hakijabadilishwa.

Hivyo, kwa hesabu nyingi ni kwamba CCM waliibuka washindi katika ujio wa demokrasia ya vyama vingi.

Walifanya mabadiliko ya Katiba, wakatunga sheria za siasa, wakaanzisha ofisi ya msajili wa vyama vya siasa, vyama vikasajiliwa na kupewa ruzuku. Hata Uchaguzi Mkuu 1995, mgombea urais wa upinzani aliyekuwa mstari wa mbele alikuwa Augustino Mrema, aliyehamia chama cha NCCR-Mageuzi kutoka CCM. Hii ilikutana na kauli ya Mwalimu Nyerere kuwa “upinzani wa kweli utatoka CCM”.

Dhana ya Mapinduzi kutoka Juu ndio sababu ya sura zote za kisiasa Tanzania katika miaka 30 ya mfumo wa vyama vingi kuamuliwa na CCM. Kama Mwalimu Nyerere alivyopiga marufuku vyama vingi mwaka 1962 ndivyo na Mwinyi alivyorejesha mwaka 1992.

Mwalimu Nyerere alipopiga marufuku vyama vingi, Januari 1963 ilitungwa sheria ya Bunge kutambua chama kimoja tu. Mwinyi aliruhusu vuguvugu za kudai demokrasia ya vyama vingi, akaunda tume kutafuta maoni, akaanzisha mchakato wa mabadiliko ya Katiba, kisha akasaini sheria ya kwanza ya vyama vingi. Rais wa Tatu, Benjamin Mkapa, hakutaka kuvidekeza vyama vya upinzani.

Hata hivyo, hakuvibana kufanya shughuli zao. Hiki ndicho kile kipindi ambacho vyama vilibaini kuwa siasa sio kazi ya madeko wala lelemama.

Rais wa Nne, Jakaya Kikwete, alionesha kuwa upinzani ni taa kwa Serikali kujikosoa na kufanya vizuri. Akiwa ameshika usukani wa nchi, ndipo upinzani ulikua kwa kiasi kikubwa na wabunge wa vyama pinzani kuwa wengi zaidi katika historia ya nchi.

Rais wa Tano, Dk John Magufuli, hakuwa na utaratibu wa kutabasamu na wapinzani wala kusikilizana nao sikio kwa sikio, bali alitazamana nao jicho kwa jicho. Hiki ni kipindi ambacho vyama vya upinzani vilidumaa mno.

Mwandishi wa habari veterani na mwanasheria, Jenerali Ulimwengu, aliwahi kusema kuwa kidemokrasia nchi ilirudi nyuma kwa miaka 50 wakati wa uongozi wa Magufuli.

Hiki ni kipindi ambacho siasa za nchi ziliimbwa na kutafsiriwa kwa kumzunguka mtu mmoja. Wabunge na madiwani wengi wa vyama vya upinzani walijiunga CCM kwa hoja ya kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli.

Rais wa Sita, Samia Suluhu Hassan, ameamua kuuhami mfumo wa vyama vingi vya siasa. Anaondoa chuki za kisiasa na kuruhusu mwanzo mpya wa siasa za kusikilizana sikio kwa sikio badala ya kutazamana jicho kwa jicho. Manung’uniko ya wapinzani yameondoka. Kesi za kisiasa nyingi zimefutwa. Waliokuwa na vilio vya kudhulumiwa stahiki zao kisiasa wamelipwa. Mfano ni Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, Tundu Lissu, alishakiri kulipwa fedha zake zote. Kuanzia matibabu, mishahara na kiinua mgongo cha ubunge.

Septemba 7, 2017, Lissu alishambuliwa kwa risasi takriban 38, na 16 kati ya hizo ziliingia mwilini na kusababisha afanyiwe upasuaji mara 24. Lissu akiwa Ubelgiji kwenye matibabu, ilitangazwa jimbo lake lipo wazi kwa sababu ya utoro.

Rais Samia ameunda Kikosi Kazi chenye wanasiasa, viongozi wa dini, wanahabari, wanazuoni na kadhalika ili kutengeneza barabara mpya ya kisiasa.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), chenyewe hakikutaka kushirikiana na kikosi kazi kwa hoja kuwa hakikuwa na imani na baadhi ya wajumbe. Rais Samia alikutana na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, kisha ukazaliwa mkutano mwingine wa viongozi wa Chadema na CCM.

Mpaka hapo ni dhahiri kuwa Rais Samia hataki kumwacha yeyote katika safari aliyoianzisha ya maridhiano, mapatano na ushirikiano wa kujenga upya demokrasia.

Anataka kila mmoja aione kesho ya pamoja kwa mustakabali wa uhuru na demokrasia.

Tangu ameingia madarakani kuna mengi ambayo Watanzania wana kila sababu ya kumuona Rais Samia kama mkombozi kwenye Nyanja mbalimbali na hususan katika siasa.

Hakuna ubishi kwamba, miaka sita iliyopita siasa za Tanzania hasa vyama vya upinzani vilipitia kwenye ‘Ubatizo wa moto’ kama alivyowahi kusema mwanasiasa mkongwe na Katibu Mkuu mstaafu wa CCM, Mzee Yusuph Makamba.

Lakini, kwa sasa angalau vyama vinapumua, vikifanya harakati za kisiasa bila kukwaruzana na Serikali wala Jeshi la Polisi kama ilivyokuwa hapo awali.

Wasomi wachambua 4R

Katika makala maalumu ya Rais Samia iliyochapishwa kwenye vyombo vya habari Julai Mosi mwaka huu, alibainisha kwamba katika utawala wake ataongoza kwa kutumia 4R ambazo ni ufupisho wa dhana ya maridhiano, ustahimilivu, mabadiliko na kujenga upya.

Katibu Mkuu wa chama cha ADC, Doyo Hassan Doyo alisema nchi ilikuwa imesambaratika kwa namna serikali ya awamu ya tano ilivyokuwa ikiendesha mambo yake, hakuna aliyeridhika na mambo hayo hasa katika ujenzi wa umoja wa kitaifa na demokrasia.

“Ukiona Rais wa awamu ya sita amekuja na mifumo mipya ya ujenzi wa nchi maana yake amejiridhisha kuna tatizo ambalo lipo. Kwa hiyo nampongeza kwa kuja na mfumo ambao utatutoa huko.

“Sasa hivi karibuni kesi nyingi za kisiasa zimeondolewa mahakamani na wengine waliofungwa ambao wamekatiwa rufaa wameachiwa. Hii inaonyesha mifumo imeanza kufanya kazi yake, haiingiliwi na taasisi zingine,” alisema Doyo.

Mwanasiasa huyo aliongeza kwamba ADC wanaamini kwamba falsafa hiyo ya Rais Samia itawaponya Watanzania kwa sababu ameshatoa tamko la namna anavyotaka kuiendesha nchi katika ukuaji wa uchumi na demokrasia.

Kwa upande wake, mchambuzi wa siasa, Buberwa Kaiza alisema falsafa hiyo inahitaji kujengewa misingi ya kisheria au kupewa nguvu na chama chake kwenye Ilani ya uchaguzi ili kurahisisha utekelezaji wake.

Alisema falsafa ya 4R ilitakiwa kupitishwa kwenye chama na chama ndiyo kizitoe kwa wananchi baada ya kujadiliana. Alisisitiza kwamba ni vizuri hizo 4R zikaelezewa vizuri ili kila mtu afahamu zimetokana na nini.

“Unapofanya reconciliation (maridhiano) maana yake kumekuwa na mgogoro wa muda mrefu, sasa una-reconcile wapi, ndani ya chama chao au kati ya chama chao na vyama vingine au kati ya dola na wananchi?

Akiwa na mtazamo tofauti na Kaiza, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisulie alisema licha ya kwamba kuna misingi ya kisheria, kikanuni, kiutawala bora na kiuongozi, bado kuna nafasi ya mtu kama mtu kuhakikisha maono yake yanatimia.

Alisema viongozi wote waliopita walikuwa na maoni au kaulimbiu zao fulani ambazo walizitumia katika kuliongoza taifa. Alisema kaulimbiu au falsafa hizo ndiyo ziliwatambulisha na kuwatofautisha na wengine.

“Rais Samia kuleta hizo 4R ni kwamba inaendelea kumtambulisha yeye, anatamani kitu gani kifanyike ili kuendelea kulipeleka taifa mbele. Kwa hiyo mimi naamini kabisa kwamba hizo 4R ndiyo mwongozo mkuu wa Rais mwenyewe,” alisema Dk Loisulie.

Alisisitiza kwamba 4R zitasaidia kumtambulisha yeye kama kiongozi mkuu wa nchi na serikali lakini pia kumsaidia kutekeleza mambo ambayo angependa yafanyika katika utawala wake kwa wananchi wake.

“Kwa hiyo, hizo ni kaulimbiu za kawaida kwa kila kiongozi anayeingia madarakani,” alisisitiza Dk Loisulie wakati akizungumza na Mwananchi kuhusu 4R zilizoasisiwa na Rais Samia siku ya kumbukizi ya miaka 30 ya kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi, Julai Mosi.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz