Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rais Magufuli alitaka baraza la wadhamini la CCM kufanya tathmini ya mali

11389 JPM+PIC TanzaniaWeb

Sat, 14 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli amelitaka Baraza jipya la wadhamini la chama hicho kutekeleza majukumu yake ipasavyo na kufanya tathmini ya mara kwa mara ya mali za chama na jumuiya zake

Taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais-Ikulu, Gerson Msigwa imesema Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo Julai 13, 2018 alipokutana na wajumbe wa baraza hilo Ikulu jijini Dar es Salaam.

Rais Magufuli amesema baraza hilo linapaswa kutekeleza majukumu yake ipasavyo, ambayo ni kusimamia mali zote za chama na jumuiya zake, kufanya tathmini ya mara kwa mara ya mali za CCM na jumuiya zake, kutoa ushauri juu ya mabadiliko yoyote yanayohitajika katika umiliki wa mali.

Mwenyekiti huyo amesema pamoja na kutekeleza majukumu mengine ambayo yatakabidhiwa kwake na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa.

Rais Magufuli amesisitiza hatarajii kuona dosari za usimamizi wa mali za chama zikiendelea na amewataka wajumbe hao kuhakikisha CCM inanufaika na mali zake na kuachana na utegemezi ambao umekuwa ukisababisha kuomba misaada kutoka kwa watu.

Naye Mwenyekiti wa baraza hilo Anna Abdallah amemshukuru Rais Magufuli kwa kuwaamini na kuwateua kuunda baraza hilo na ameahidi watahakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa umakini na kwa maslahi ya CCM.

“Mambo hayatakuwa kama walivyozoea huko nyuma kwamba kila mtu anamiliki kipande chake cha mali za chama, hapana, mali zote za chama ni mali ya Baraza la Wadhamini wa Chama Cha Mapinduzi” amesema Anna

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amesema baraza hilo la kwanza kuundwa baada ya kufanyika marekebisho ya katiba ya chama, litasimamia mali za CCM pamoja na kusimamia utekelezaji wa mapendekezo ya tume ya kufuatilia mali za chama ambayo yeye alikuwa mwenyekiti wake.

Wajumbe wa baraza hilo ni; John Chiligati, Jaji mstaafu Mark Bomani, Balozi mstaafu Daniel Ole Njoolay, Pandu Ameir Kificho, Christopher Gachuma, Dk Haruni Kondo na Hassan Omar Mzee.

Chanzo: mwananchi.co.tz