Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rais JPM Ataka kampeni zifanywe kistaarabu

Dd8d3b3434b698cbe1c19fd575c5f405 Rais JPM Ataka kampeni zifanywe kistaarabu

Thu, 23 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

RAIS John Magufuli alivitaka vyama vya siasa nchini, kufanya kampeni kistaarabu bila kutukana wakati wa kunadi sera, ili wananchi wawapime na kuchagua wagombea wanaowataka. Rais alitoa kauli hiyo jana jijini Dodoma wakati akifungua jengo la Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ambalo hadi litagharimu Sh bilioni 16.8 ujenzi utakapokamilika.

Magufuli alipongeza NEC kwa kuwa na jengo lao, watakalolitumia kutangaza matokeo ya uchaguzi wa Rais na wabunge Oktoba 28 mwaka huu baada ya kura kupigwa. NEC ilianzishwa 1993 na tangu wakati huo, imekuwa ikitumia majengo ya kupanga jijini Dar es Salaam.

Rais Magufuli alisema NEC wanatakiwa kutekeleza wajibu wao, kwa kusimamia uchaguzi vizuri na kwa haki kwa kuzingatia sheria na kanuni za uchaguzi. Aliwataka wagombea wote kupitia vyama vyote vya siasa, kumtanguliza Mungu katika kampeni zao na kuepuka vitendo vya vurugu, kwani vurugu haijengi na vyombo vya usalama vihakikishe vinalinda usalama.

Rais Magufuli alisema ana hakika uchaguzi, utakwenda vizuri na aliwaomba wananchi kushiriki kikamilifu kwa kufika kwa wingi katika mikutano ya hadhara kuanzia Agosti 26. Kampeni zitakamilika Oktoba 27, mwaka huu na Oktoba 28, mwaka huu Watanzania watapiga kura.

Siku hiyo itakuwa Jumatano na itakuwa siku ya mapumziko. Rais aliahidi kutoa ushirikiano wa hali na mali kwa vyama, vitakavyoshiriki uchaguzi na kwa wagombea wote ili kuhakikisha kampeni na uchaguzi vinafanyika kwa ustaarabu na usawa.

Alivitaka vyombo vya ulinzi na usalama, kuhakikisha havitumii nguvu kwa wanasiasa au wagombea; na wanasiasa nao wana wajibu wa kutofanya vitendo ambavyo vitalifanya jeshi hilo kutumia nguvu.

“Katika uchaguzi tunatakiwa kwenda na kufanya kampeni za upole, tukimtanguliza Mungu, kwani sisi sote tunajenga taifa moja Tanzania,” alisema.

Kabla ya kuanza kuzungumza, Rais Magufuli aliwaita wenyeviti wenzake wa vyama 15 vya siasa kutoka walipokaa katika viti vya nyuma na kuwataka waende kukaa pamoja katika jukwaa kuu, kwamba ni wenyeviti wenzake wapo sawa na wote jengo hilo la NEC ni lao.

Katika uzinduzi wa jengo hilo ambalo viongozi wa siasa ni wadau, alikuwepo Katibu wa CCM, Dk Bashiru Ali, Kiongozi wa CCK, David Mwaijojele, wa SAU Bether Mpale, wa NLD Oscar Makaidi, wa DP Philip Fumbo na wa UMD, Masodo Kamani.

Wengine ni Mohammed Aboud wa Demokrasia Makini, wa UPDP Twalib Ibrahimi, wa TLP Richard Lyimo, wa Chauma Kayombo Kabutai, wa ADC Queen Cuthbeth na wa Ada Tadea, John Shibuda, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa.

Wengine ni Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia. Wakati huo huo, Rais Magufuli ametoa wiki mbili kwa taasisi zinazodaiwa madeni na Suma Guard, ambayo ni kampuni tanzu ya Suma JKT kulipa Sh bilioni 11 zikiwa ni gharama za ulinzi.

Rais Magufuli alimwagiza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuhakikisha anafuatilia na ampe taarifa ya taasisi hizo zilizolipa hata kama atakuwa kwenye kampeni, kwani hakuna cha bure.

Alisema taasisi hizo kama zimelindwa na kampuni hiyo, lazima zilipe fedha hizo ili kampuni hiyo ilipe pia gawio la Serikali. Pia aliwapongeza Suma JKT kwa kazi nzuri ya kujenga majengo hayo, ambayo yatatumika kwa ajili ya uchaguzi mkuu mwaka huu.

Alisema vijana hao wanazidi kumpa deni na hatawasahau katika ufalme wake. Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Semistocles Kaijage alisema Suma JKT wamefanya kazi nzuri na ikiwezekana wapewe kazi za ujenzi wa majengo jijini Dodoma.

Kaijage alisema kampuni hiyo imefanya kazi nzuri katika ujenzi wa majengo hayo matatu, kwa kuwa jengo la utawala limefikia asilimia 97, jengo la ghala limefika asilimia 92 na la kutangazia matokeo asilimia 79.

Majengo yote yamefikia wastani wa asilimia 88 na yatakamilika Agosi 30 mwaka huu. Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Meja Jenerali Charles Mbuge alisema mradi huo umetekelezwa kwa faida tangu Desemba 24 mwaka jana, uliposainiwa mkataba wa ujenzi. Alisema ujenzi ulianza rasmi Januari 17, mwaka huu kwa gharama ya Sh bilioni 12.3 na wajenzi wameshalipwa Sh bilioni 10.3, bado Sh bilioni 2.15.

Jengo hilo liitwalo “Uchaguzi House” lilianza kujengwa na Wakala wa Majengo nchini (TBA) mwaka 2017. Lakini, Desemba 12, mwaka jana Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliingilia kati, baada ya kuona kazi inasuasua na ndipo wakapewa Suma JKT.

Chanzo: habarileo.co.tz