Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RPC mstaafu kuwa mwenyekiti wa CCM Arusha kwaibua mjadala

89170 Zelote+pic RPC mstaafu kuwa mwenyekiti wa CCM Arusha kwaibua mjadala

Thu, 19 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Kamanda mstaafu wa polisi, Zelothe Stephene amejikuta akizua mjadala baada ya kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha.

Wachambuzi waliozungumza na Mwananchi wamesema ushindi huo unaashiria kuwa maofisa wa vyombo vya ulinzi na usalama nchini wanajihusisha na siasa jambo linaloweza kuibua hali ya sintofahamu, wengine wakisema kujihusisha na siasa baada ya kustaafu si jambo baya.

Zelothe alichaguliwa juzi kuwa mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha baada ya kupata kura 468 dhidi ya wagombea wenzake Balozi Batilda Baruani aliyepata kura 339 na Bakari Msangi aliyepata kura 42.

Mwanasheria wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Fulgence Masawe alisema ushindi wa Zelothe una ukakasi, “tuliona jaji mkuu mstaafu, Augustine Ramadhani akigombea urais kwa tiketi ya CCM, tumeona wakuu wa vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama wakigombea nafasi za kisiasa, haya yanachafua vyombo vya ulinzi na usalama.”

Alisema sheria ya utumishi wa umma ipo wazi kuzuia baadhi ya viongozi kujihusisha na masuala ya siasa, “wanapochaguliwa sasa kuna maswali je ni lini walijiunga na siasa hadi kushika nafasi za juu.”

Mkurugenzi wa taasisi ya haki za kiraia na msaada wa kisheria (Cilao), Charles Odero alisema kuchaguliwa kwa Zelothe kunakinzana na sheria inayowataka polisi kutojihusisha na siasa. “Inaonyesha Zelothe alikuwa mwanachama wa CCM muda wote alipokuwa askari na hili linafanya hata askari ambao bado wako kazini kutamani kujiingiza kwenye siasa. Ikiwa hivyo ni jambo ambalo ni hatari katika kutekeleza haki kwa vyama vyote vya siasa,” alisema Odero.

Wakili, Paul Ogendi wa Chama cha Mawakili Afrika Mashariki (ELS) alikuwa na hoja tofauti akisema si kosa Zelothe kuwa mwanasiasa. “Kama alistaafu zaidi ya miaka mitatu inawezekana ndio muda aliojiunga na siasa, kimsingi ana haki ya kuchagua na kuchaguliwa katika nafasi za kisiasa,” alisema Ogendi.

Mkazi wa Arusha, Jane Lyimo alisema ushindi wa Zelothe ni ishara kuwa kuna viongozi wengi wa Serikali ambao ni wanachama wa vyama vya siasa na kwamba uamuzi wao unaweza kuwa na mapenzi kwa chama fulani.

Mwanasheria Dk Onesmo Kyauke alisema sheria haimkatazi mtumishi yeyote wa vyombo vya usalama kujihusisha na siasa baada ya kustaafu bali inamkataza kufanya hivyo wakati akiwa mtumishi wa Serikali ili kuondoa mgongano wa kimaslahi.

“Anaweza kuwa mtumishi lakini moyoni anacho chama anakipenda na akistaafu anakuwa huru kujiunga nacho na akijiunga anakuwa huru kugombea nafasi yoyote, wamekatazwa kujihusisha na siasa wakiwa kazini kwa sababu wanahofia kuwa anaweza kukipendelea chama chake wakati wa kutoa maamuzi endapo akipewa uongozi,”

Juzi baada ya kuchaguliwa, Zelothe aliahidi kuvunja makundi ndani ya chama hicho, kuongeza ushirikiano na idara na taasisi za Serikali na kupanga mikakati za ushindi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Katika miaka yake ya mwisho kabla ya kustaafu Zelothe alikuwa RPC katika mikoa ya Dodoma, Mwanza na Mtwara.

Chanzo: mwananchi.co.tz