Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RC Chalamila awapa ujumbe Chadema wa Rais Samia

Chalamila: Viongozi Wa Dini Muiombee Serikali RC Chalamila awapa ujumbe Chadema wa Rais Samia

Wed, 24 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amekutana na wafuasi na wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kuwapa salamu za kubariki maandamano hayo akidai ni za Rais Samia Suluhu Hassan.

Chalamila anayeongoza shughuli za usafi jijini Dar es Salaam, amewasili eneo la Mbezi Luis asubuhi ya leo Jumatano, Januari 24, 2024 ambako maandamano ya chama hicho cha upinzani yanaanzia.

Akiwa eneo hilo, Chalamaila amewataka wafuasi na wanachama wa Chadema waendelee kuandamana na kufikisha ujumbe wao.

Pia, amesema wakati Chadema wakiendekea na maandamano, yeye na watu wake wanaendelea na usafi, akisisitiza Rais Samia ameyabariki maandamano hayo na kila mmoja anapaswa kulinda amani.

Muda mfupi ujao, wanachama na wafuasi wa chama hicho wataanza maandamano yao ya amani yenye ajenda ya kuitaka Serikali kusikiliza maoni ya wananchi kuhusu kuondoa miswada ya sheria ya uchaguzi ya vyama vya siasa bungeni ili kuandikwa upya baada ya marekebisho ya Katiba ya 1977.

Miswada hiyo ni Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Muswada wa Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Vyama vya Siasa ya mwaka 2023.

Pia, inataka Serikali itengeneze mpango wa dharura wa kukabiliana kwa kupanda gharama za maisha kwa Watanzania na mfumuko wa bei.

Wakati wanachama hao wakiendelea kukusanyika Mbezi ili kuanza maandamano, Chalamila ambaye ameiongoza timu yake kufanya usafi kwenye eneo hilo alizungumza na wanachama hao akiwataka kuendelea na maandamano.

"Nawapa salamu za Rais, ninyi endeleeni kuandamana na sisi tunaendelea na usafi," amesema Chalamila huku akishangiliwa na wafuasi na wanachama wachache wa chama hicho waliokuwa wakiimba, kucheza na wakipiga makofi huku baadhi ya nyimbo wakimtaja Rais Samia na sukari bei juu.

Hali ilivyo hadi sasa

Hadi kufikia saa 2:00 asubuhi wanachama wachache walikuwa wamekusanyika Kituo cha Daladala cha Mbezi Luis wakiwa wamevaa fulana za chama hicho na wengine wakipeperusha bendera wakiimba na kucheza huku takribani mita 20 pembezoni mwao, usafi ukiwa unaendelea ukiongozwa na Chalamila.

Wanachama hao wanaendelea kukusanyana kabla ya kuanza maandamano yenye vituo viwili cha kwanza ni Mbezi Mwisho yakiongozwa na Makamu Mwenyekiti Bara, Tundu Lissu kwenda Ofisi za Umoja wa Mataifa (UN), eneo la Ubungo katika Jengo la PSSSF na mengine yakianzia Bunguruni kupitia Karume- Kariakoo kisha Barabara ya Morogoro yakiongozwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live