MKUU wa Mkoa wa Iringa mteule Queen Sendiga, amesema kuwa yeye hawezi kuyabeba mambo yaliyotokea wakati wa kampeni na kuwa nayo hadi leo, kwa kuwa kwenye kampeni kunafanyika mambo mengi ambayo huishia huko huko.
Kauli hiyo ameitoa hii leo Mei 17, 2021, kupitia East Africa Radio alipohojiwa kuhusu tukio la kuvunjiwa kioo cha gari alilofanyiwa na baadhi ya vijana wa mkoa wa Iringa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, ambapo yeye alikuwa ni mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha ADC.
“Hizo zilikuwa kampeni zilishamalizika, hayo yatakuwa ni mambo ya kipuuzi sasa na kwenye kampeni huwa kuna mambo mengi mno, huwezi ukaondoka na mambo ya kwenye kampeni ulale nayo na uamke nayo, hayo yalishamalizika muda mrefu.
“Ukitaka kujenga nyumba imara hakikisha unasimamisha msingi imara, kama tunataka kutengeneza viongozi wanawake majasiri lazima tuhakikishe wanawake hawa tunawatengeneza tangu wakiwa wadogo ili wawe majasiri.
“Katika uchaguzi mkuu wa 2020 kilichonisononesha ni kutopata kura za kutosha kwa sababu nilitaka kwa dhati kabisa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa TZ, sikuomba Urais kwa mzaha sababu nilikuwa na uhakika naweza
“Rais anapochaguliwa haimaanishi yeye amepewa hatimiliki, CCM kwa kipindi hicho hawakuwa na hatimiliki ya kuongoza, kila mwananchi alikuwa na haki ya kugombea wakati wa uchaguzi mkuu, ningeingia madarakani na kuanzia pale alipoishia,” Queen Sendiga RC mteule Iringa.