Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Queen Mlozi: Mabadiliko ndani ya CCM ni kuleta tija

44634 Pic+mlonzi Queen Mlozi: Mabadiliko ndani ya CCM ni kuleta tija

Tue, 5 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Chama cha Mapinduzi kimepitia mabadiliko mbalimbali ambapo katika utawala wa awamu ya tano, chama hicho kimefanya mabadiliko ya kupunguza idadi ya wajumbe wa mikutano ya uamuzi kama vile Kamati kuu, Halmashauri Kuu na Mkutano mkuu.

Vilevile chama hicho kimefanya mabadiliko ya umiliki wa mali kwa kuweka bodi moja ya wadhamini inayoangalia mali zote za chama zikiwamo za jumuiya zote tatu za UWT, Wazazi na Vijana.

Mabadiliko hayo yote yamekifanya chama kujiita ‘CCM mpya’. Hata hivyo, kwa upande mwingine mabadiliko hayo yamehojiwa na wadau yakionekana kuminya demokrasia ndani ya chama hicho.

Lakini, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wanawake ya chama hicho (UWT), Queen Mlozi anakanusha akisema yamelenga kuleta tija kwa chama na kwa wananchi, alipokuwa akizungumza katika mahojiano maalum na mwandishi wetu.

Swali: Unayazungumziaje mabadiliko haya ndani ya CCM na jumuiya zake, kwa kuwa sasa yanaonekana kukifanya chama kuwa cha watu wachache?

Jibu: Katika taasisi yoyote taifa lolote, unapokuwa na mabadiliko fulani, wengine si wepesi kukubali mabadiliko. Lakini mabadiliko tunayofanya yana tija ndiyo maana yanaitwa mabadiliko.

Binadamu inawezekana alipenda kuishi kwa mtindo fulani wa maisha, sasa unapomwambia leo unatakiwa kuishi hivi, inawezekana hakubali.

Mabadiliko haya ni ya kawaida, kwa sababu yanafanyika ili kuleta tija katika CCM.

Swali: Kuhusu mali za chama, awali kila jumuiya ilikuwa na mali zake zinazosimamiwa na bodi ya jumuiya husika, lakini sasa mali zote zinasimamiwa na bodi moja unaonaje utaratibu huo?

Jibu: Kuwa na bodi moja ni hatua muhimu sana kwa sababu chama ni kimoja lakini jumuiya zote ni za chama, hata jumuiya ya vijana na wake zote ni za chama. Kwa nini tuwe na bodi nyingi?

Kwa hiyo mabadiliko yapo na tunayakubali na sisi wote sasa lazima mali zetu zote zinasimamiwa na bodi ya wadhamini wa chama cha mapinduzi.

Katika makusanyo tumeona ili kudhibiti mapato ya jumuiya za chama tumeona tutumie control number. Kwa mfano leo naweza kujua Manyara leo wamekusanya nini, Arusha leo wametumia kiasi gani. Inatusaidia kudhibiti mapato na matumizi ili tuwe na matumizi ya tija yanayotusaidia, kuliko ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Mfumo wa control number ni wa wazi ambao hata mimi nikiomba msaada kutoka kwako, lazima kwenye mfumo ule itaonekana kwamba leo mtu huyu amesaidia kiasi fulani.

Swali: Kamati maalumu ya kuangalia mali za chama iliagiza wachukulie hatua wanachama waliofanya ubadhirifu wa mali za chama, je, mmetekeleza hilo?

Jibu: Tumeyatekeleza, kwa sababu unapopewa maagizo na bosi utaacha kutekeleza? Sasa ndiyo tumetengeza huo mfumo wa mali zote za chama na jumuiya zijulikane na ziwe wazi. Huko site hivi sasa kuna vijana wanaendelea na kuziingiza kwa njia ya kisasa.

Tuko pamoja na ndiyo maana nimeeleza chama ni koja na jumuiya zake. Wale walituonyesha njia. Sasa tunakwenda kuzihakiki vizuri. Zikishajulikana tutawapa bodi ya wadhamini ili wajue ili wajue kilichopo ni kiwanja, nyumba, shamba.

Ripoti ipo lakini ni lazima tuende hatua kwa hatua. Mimi nimeambiwa mali ni za fulani labda zichukuliwe, si lazima niende site nikahakikishe? Naye atatoa maelekezo. Vitu vingine unakwenda pamoja na maagizo lakini pia unabainisha kujua ukweli ili usimwonee mtu.

Swali: Huoni kwamba mabadiliko yanayopunguza idadi wa jumbe kwenye vikao vya uamuzi yanaminya demokrasia ndani ya chama?

Jibu: Si kweli huo ni mtazamo wa mtu tu, kwa sababu mbona Rais ni mmoja hatuko 10? Ni demokrasia kwamba tupunguze kwa manufaa ya chama. Walipokuwa wengi sana wingi ule haukuleta mafanikio, tulifanya mabadiliko ya Katiba, tukapunguza idadi ya wanachama kulingana na mazingira ya hali ya sasa tuliyonayo.

Ukisema demokrasia imepungua siyo kweli, demokrasia ipo palepale kwa sababu wawakilishi wapo. Hata ukiangalia idadi iliyopunguzwa siyo kubwa, kwa mfano. Mjumbe wa NEC walikuwa kila wilaya, hatukuona tija ya kila mtu katika wilaya zote, tukasema wajumbe watoke kila mkoa. Lakini kuna wajumbe wanaoingia kupitia nyadhifa zao.

Kwa hiyo demokrasia ipo kwa sababu demokrasia ya kupunguza imeanzia huku huku chini, nafikiri ni mtazamo tu, lakini mimi naona tuko sawa.

Haitaleta shida ndiyo maana nimesema ni mtazamo wa mtu. Tunapopunguza kuna jambo tunaloliangalia mbele, inaleta shida kwa sababu inawezekana kila mmoja alitaka kuingia. Hili siwezi kulisemea sana kwa babu kama kiongozi wangu ameliongea basi tungoje hivyo itakavyokuwa.

Swali: Kwa muda mrefu sasa wanawake wamekuwa wakitegemea kupata nafasi za viti maalumu bungeni na kwenye mabaraza ya madiwani. Ninyi kama UWT mnawasaidiaje ili kugombea kwenye majimbo na kata?

Jibu: Kazi yangu mimi ni kuhamasishana, kwa sababu nafasi ya wabunge wa viti maalumu iliwekwa kwenye Katiba ili wanawake na wanaume tuwe na uwiano sahihi, ili wanawake tuwepo kwenye ngazi za maamuzi.

Sasa kusema hii nafasi ya viti maalumu itoke iende moja kwa moja, hapana. Nafasi ya viti maalumu, itaendelea kuwepo kwa sasa hatutaendelea na jambo lolote mpaka Katiba itakapobadilishwa.

Lakini, hatutachoka kuwahamasisha walio nje nao waweze kugombea hizo nafasi. Hata hao waliomo, tutaendelea kuwahamasisha kwamba sasa wewe unaonaje, ukaacha nafasi ya viti maalumu ukagombea jimbo. Inategemea uwezo wa mtu.

Lakini, nafasi ziko wazi na wao hili wanalijua. Sisi tungependa wanawake wengine wagombee kama nilivyosema, nafasi yetu ni kuhamasishana. Unajua katika historia wanawake wengi ni waoga, lakini wanawake lazima tujitathmini. Tuna nafasi kubwa katika uongozi. Suala la uongozi katika jamii lina katika familia, lina historia.

Swali: Ukiacha nafasi hizi za viti maalumu na uteuzi ambazo wanawake wanafaidika, UWT mna mkakati gani wa kuhakikisha mwanamke anagombea kiti cha urais?

Jibu: Hilo linawezekana muda ukifika watajitokeza. Kwa sababu kama tunaye makamu wa Rais, na ukifikiria mwaka 2015 uchaguzi uliopita, mheshimiwa Mghwira (Anna) Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, lakini hata miaka ya nyuma wapo waliogombea.

Mimi naamini kwa mabadiliko tuliyonayo na hamasa tulionayo kuwajengea uwezo katika maeneo mbalimbali.

Nafikiri muda ukifika, uchaguzi wa serikali za mitaa utakaoanzia mwaka huu, na tumeshahamasisha wanawake hebu wanawake wengi wajitahidi kugombea katika nafasi mbalimbali. Nina imani kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu kwa kadiri itakavyowezekana, yawezekana ikawa zaidi kuliko miaka ya nyuma.

Swali: Suala la elimu ya watoto wa kike wanaopata ujauzito kuendelea na masomo limekuwa na mjadala mkubwa, licha ya ilani ya uchaguzi ya CCM kueleza kuwa wataendelea. Ninyi kama UWT mna msimamo gani?

Jibu: Mimi katika hilo mimi ni mzazi na ni mwalimu kama nilivyoambia. Hivi kule shuleni tunaweza kuchanganya mama, dada au mzazi? Kwa sababu mtoto aliyezaliwa lazima umpatie haki zake za msingi.

Yeye ni mtoto, lakini ni kwa nini wewe unaamua, wanasema mshika mawili moja humponyoka. Tuwahamasishe watoto wasome, ili waje kuwa viongozi kama sisi, tunataka ma-injinia mbele ya safari, tunataka kina mama wa taifa la kesho. Kwa hiyo nadhani kwa hili tuko sahihi kabisa.

Kama mtu amepata mimba na anatakiwa asome, sisi kaka UWT tuanzishe jambo jingine mtoto huyu tumpatie mafunzo ya Veta ya stadi za kazi, akafanya badala ya yale masomo na anaweza kufanya vizuri zaidi. Ndiyo maana siku hizi mtu anaweza kufanya mtihani akiwa mtahiniwa binafsi. nafikiri kupata mimba siyo mwisho wa masomo, siyo kusema kwamba tayari hauna faida katika jamii. Huu ni utaratibu.

Lengo ni kupunguza mimba za utotoni, watoto kupunguza ndoa za utotoni, ili watoto wale wanaokuwa katika umri mdogo wasipate mimba. Ndiyo maana tunawahimiza wazazi waongee na watoto wao. Wanahitaji malezi toka nyumbani, tunawatahadharisha madhara ya mimba na ndoa za utotoni. Wakishafahamu nafikiri jambo hili halitakuwa na kasi kubwa.

Kwanza mfumo wa elimu uko vizuri tu wala hauna shida, ilani ni ya miaka mitano tu, wakiona kipengele hiki hakikukidhi watakiondoa. Ndiyo maana nilisema hivi, wewe msichana lazima ujitawale silka zako. Nimewaambia wanaume hivi, mtoto wa mwenzio ni mtoto wako.



Chanzo: mwananchi.co.tz