Mbunge wa Ubungo, Profesa Kitila Mkumbo amemuomba Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa kujenga barabara ya kilomita 8 kati ya Kimara – Kinyerezi kwa kiwango cha lami ili aweze kufanya mikutano ya hadhara.
Profesa Mkumbo amesema hana raha kwenye eneo hilo na hajui atakwenda kuwaambia nini wananchi 118,000 ambao wanaishi katika eneo hilo kwani imekuwa ni ahadi ya muda mrefu tangu utawala wa awamu ya nne.
Mbunge huyo amemwangukia Profesa Mbarawa kwamba aliyekuwa kiongozi wake wakati wote walipokuwa Wizara ya Maji wakati huo Profesa Mbarawa akiwa Waziri na Profesa Kitila akiwa ni Katibu Mkuu.
Amesema eneo hilo licha ya kuwa na watu wengi lakini kuna biashara za kutosha ikiwemo baa za pombe 48, nyumba za kulala wageni 34, saloon 20, maduka 121 na Super Market 21 hivyo kuna umuhimu wa kujengwa kwa barabara hiyo.
“Mheshimiwa Waziri wewe ulikuwa kiongozi wangu, nilikusaidia na ukaupiga mwingi hadi sasa bado wanakuona na mama amekupa hiyo Wizara, hebu nisaidie na mimi kwenye hili mbona kilomita nane tu na ukisema neon tu na linakuwa,” amesema Profesa Mkumbo.
Waziri huyo wa zamani wa Viwanda na Uwekezaji ameliambia Bunge hatakuwa na hali nzuri kama atakwenda kufanya mikutano katika Kata ya Kimara kwani wananchi wanasubiri kwa hamu kubwa ujenzi wa barabara hiyo.
Kwa mujibu wa Profesa Kitila, wananchi waliipa jina la Kikwete barabara hiyo ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Rais huyo katika kuwasaidia kuijenga kwa kiwango cha lami lakini hali imeendelea kuwa tofauti hadi sasa.