Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Prof. Lwaitama: Chadema ilitaka kujinusuru sakata la kina Mdee

MDEE NA WENZAKEEE Mdee ma wenzake

Thu, 21 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Moja kati ya kesi zilizovuta hisia za watu na kufuatiliwa zaidi ni ile inayohusu wabunge 19 wa viti maalumu wakiongozwa na Halima Mdee, waliovuliwa uanachama na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Novemba 27 mwaka 2020, Halima Mdee na wenzake 18 walivuliwa unachama na Kamati Kuu ya Chadema kwa madai ya kuapishwa kuwa wabunge wa viti maalumu wakati kamati kuu ilikuwa haijafanya uteuzi wowote wa nafasi hizo kwa mujibu wa Ibara ya 7.7.16(a) ya Katiba ya chama hicho.

Mdee na wenzake walivuliwa uanachama wa chama hicho na Kamati Kuu ya Chadema na wakakata rufaa Baraza Kuu la chama hicho lililoketi Mei 11, 2022 kusikiliza rufaa na likabariki maamuzi ya Kamati Kuu.

Wabunge hao hawakuridhika na maamuzi, wakafungua maombi Mahakama Kuu, wakipinga maamuzi ya baraza hilo ambapo Desemba 14, 2023, ilibatilisha uamuzi wa Baraza Kuu hilo lililothibitisha uamuzi wa Kamati Kuu wa kuwafukuza uanachama.

Maombi hayo yalifunguliwa na Halima Mdee na wenzake 18 ambao ni Grace Tendega, Ester Matiko, Ester Bulaya, Agnesta Kaiza, Anatropia Theonest, Asya Mohamed, Ceceilia Paresso, Conchesta Rwamlaza na Felister Njau.

Wengine ni Hawa Maifunga, Jesca Kishoa, Kunti Majala, Naghenjwa Kaboyoka, Nusrat Hanje, Salome Makamba, Spphia Mwakagenda, Stella Fiyao na Tunza Malapo.

Katika gazeti letu la jana tuliwaletea waleta maombi watano kesi iliyofunguliwa na akina Halima Mdee na wenzake walivyojibu maswali ya dodoso ya wakili Kibatala Peter Kibatala anayeongoza jopo la mawakili wa wajibu maombi katika kesi hiyo.

Pia tuliwaletea majibu ya mjibu maombi wa kwanza ambaye ni Baraza la Wadhamini Chadema, leo tunawaletea majibu ya wajumbe watano wa Baraza hilo walipododoswa na mawakili wa waleta maombi ambao ndio waombaji.

Profesa Lwaitama

Profesa Azaveli Lwaitama ni miongoni mwa wajumbe wa bodi ya wadhamini, akijibu maswali ya mawakili hao, alisema kulingana na Katiba ya Tanzania, hakuna anayeweza kuwa mbunge kama si mwanachama wa chama cha siasa.

Wakiongozwa na wakili Ipilinga Panya kumdodosa maswali, Profesa Lwaitama alisema yeye alishuhudia waombaji wakisikilizwa ngazi ya rufaa na kwamba barua ya mwaliko waliyopewa ilikuwa haizuii yeyote kuwa na mwakilishi kwenye kikao.

Alieleza kuwa hata baada ya akina Mdee na wenzake kuapishwa, bado kulikuwa na udharura wa kushughulikia jambo hilo kwa kuwa chama kilitaka kujinusuru ili kisigawanyike, kwa hiyo kulikuwa hakuna nafasi ya kuchelewa katika jambo hilo.

Profesa Lwaitama alisema kuwa waombaji walichukulia kukataliwa kwa ahirisho lao kama mkakati na kwamba Mwenyekiti wa chama, Freeman Mbowe aliyeshiriki kikao kilichowafukuza uanachama, pia alipiga kura katika rufaa yao iliposikilizwa.

Kulingana na maelezo yake, waliounga mkono uamuzi wa Kamati Kuu wa kuwafukuza uanachama akina Mdee na wenzake walikuwa wengi, kwa hiyo kwa vyovyote mwenyekiti wa chama ni lazima angeunga mkono uamuzi wa kamati.

Profesa Lwaitama alisema tuhuma dhidi ya waombaji zilikuwa wazi katika barua za wito za kuwataka wafike mbele ya Kamati Kuu na Chadema haijawahi kuwaona waombaji kama ni wabunge wa viti maalumu waliodhaminiwa na chama hicho.

Ruth Mollel na wenzake

Kwa upande wake, mjumbe mwingine, Ruth Mollel alisema kulikuwa na hali ya dharura iliyowalazimu akina Mdee na wenzake wahudhurie kikao cha Kamati Kuu na kwamba walifukuzwa kwa kukiuka Katiba ya chama hicho.

Mollel aliieleza kilichowawezesha Kamati Kuu ambayo iliwafukuza waombaji, kushughulikia rufaa yao kwenye Baraza Kuu ni matatizo ya Katiba ya Chadema na Ibara ya 83 ya Katiba ya Tanzania ni kwa waliofuata taratibu kuwa wabunge.

Ahmed Khamis na Maulida Komu walisema waombaji walijinyima wenyewe fursa ya kusikilizwa na kamati kuu kwa kukataa kuhudhuria kikao na kwamba NEC haikuidhinishwa na Chadema kuwatangaza waombaji kuwa wabunge viti maalumu.

Mjumbe mwingine, Francis Mushi alisema akina Mdee na wenzake hawakufuata taratibu za kuwa wabunge, walijinyima wenyewe fursa ya kusikilizwa na kwamba uamuzi wa baraza kuu ulifanywa na zaidi ya wale walioshiriki kamati kuu.

Mawasilisho ya mwisho ya akina Mdee

Jaji Mkeha alisema baada ya kumalizika kwa hatua hiyo, kila upande ulifanya wasilisho refu kufafanua ushahidi unaounga mkono msimamo wao, lakini katika uamuzi wake atarejea tu mawasilisho yaliyogusa mgogoro moja kwa moja.

Mawakili wa waombaji walisema maombi yao yanalenga kufidia (billet) uamuzi wa kamati kuu kwa sababu uamuzi wa kuwafukuza uanachama akina Mdee na wenzake 18 ulianzia katika kikao cha kamati kuu kilichoketi Novemba 27, 2020.

“Kwa msingi huo, mahakama ilikuwa inaombwa kufuta uamuzi wa Baraza Kuu la Chadema pamoja na mchakato wote wa kuwafukuza waombaji (Mdee na wenzake) uanachama wa Chadema,” alieleza Jaji Mkeha katika uamuzi wake.

Jaji alisema ilielezwa kamati kuu ya Chadema iliendelea kujadili hatima ya waombaji bila wao kuwepo na bila kuwasikiliza na hilo halijakanushwa na mjibu maombi wa kwanza katika kiapo chake na hata wajumbe za baraza la wadhamini.

“Kulingana na mawakili wa waombaji, kungekuwa na muda wa kutosha wa usikilizwaji kama kama kungekuwa na muda wa kutosha na mawasiliano ya hakika na waombaji. Ilisisitizwa huo wito haukuwasilishwa kwa usahihi,” alisema Jaji.

Kukataliwa ombi la ahirisho

Kuhusu hoja hiyo, Jaji alisema “Waombaji waliilaani kamati kuu kwa kukataa ombi lao la ahirisho la kikao. Mawakili wa waombaji waliwasilisha kuwa kukataliwa huko kulisababisha waombaji washindwe kusafiri kutoka Dodoma hadi Dar es Salaam.

“Kwamba waombaji hawakuwa na muda wa kutosha wa kuandaa utetezi wao na kwamba hali ilikuwa bado ni tete na wangeweza kushambuliwa na wanachama wa Chadema wenye hasira kama wangejitokeza,” alisema Jaji akirejea wasilisho.

“Mawakili hao wa waombaji waliendelea kuwasilisha kuwa kwa kuwa hakuna mwombaji hata mmoja alifika mbele ya kamati Kuu Novemba 27, 2020, haiwezi kuchukuliwa kuwa walipewa fursa ya kusikilizwa wakaamua kuikataa,” alisema.

“Kwa maoni ya waombaji, kubadilishwa kwa eneo la kikao cha kamati kuu haikuwa na uhusiano kwa kuwa baadhi yao walikuja kufahamu hilo baada ya maamuzi ya kuwafukuza uanachama kufanyika,” alisema Jaji.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live