Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Posta inavyotekeleza Ilani  ya CCM uchumi wa dijitali

548ba8216b578c3550f40e227b1c5a73 Posta inavyotekeleza Ilani  ya CCM uchumi wa dijitali

Tue, 2 Mar 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

ILANI ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020- 2025 imetaka mawasiliano kuwa ya kidigiti kwa kuwa ndio njia ya kisasa zaidi inayoharakisha maendeleo.

Ilani hiyo inasema kwamba katika kipindi cha miaka mitano ijayo CCM itahakikisha kuwa sayansi, teknoloja na ubunifu vinatumika kikamilifu katika kuendesha sekta za kukuza uchumi kwa lengo la kufikia uchumi wa hadhi ya kipato cha kati ambao ni shindani, jumuishi na unaoongozwa na viwanda.

Ilani hiyo pia inasema: “Chama Cha Mapinduzi kinatambua kuwa uchumi wa kidigitali ni muhimu katika kuleta maendeleo kwa kuongeza ufanisi katika uzalishaji na utekelezaji wa shughuli mbalimbali na kutoa fursa za kuongeza vipato vya wananchi na Taifa kwa ujumla.

“Uchumi huo umeonekana kuwa eneo muhimu katika kuchangia kukuza uchumi nchini kama ilivyofanyika katika nchi nyingine za kipato cha kati. Aidha, uchumi wa kidijitali unarandana na mapinduzi ya nne ya viwanda yanayokuja na ambayo hayaepukiki. Hivyo basi, CCM itaendelea kusimamia Serikali kuhakikisha kuwa teknolojia mpya za kidijitali zinatumika kuongeza ufanisi katika sekta za uzalishaji na kuepuka madhara yanayoweza kutokea…”

Kwa kutambua hilo, mashirika ya umma ambayo kwa muda mrefu yalikuwa yakiendesha shughuli zao kianolojia, yamekuwa yakikuna kichwa ili kwenda sambamba na uchumi wa kidijitali.

Moja ya mashirika hayo ni Shirika la Posta Tanzania ambalo limejiongeza na kuja na suluhisho la kutoa huduma ya barua na vifurishi kwa wananchi kidigitali zaidi kwa kuanzisha huduma itakayojulikana kama ‘Posta Kiganjani’.

Kwa hiyo, wale ambao jina la ‘Posta’ likitajwa wanapata picha ya kufungua sanduku na kwenda kuchungulia kama wana barua ama kifurushi, sasa mambo watayapata kiganjani, alimradi wawe na simu na kujisajili na kuzingatia masharti yatakayowekwa.

“Huduma hii inajibu mapungufu yaliyopo ya utumiaji wa Sanduku la Posta ambapo watu wengi hutumia sanduku moja. Pia katika Anwani za Makazi, familia moja au watu kadhaa walio katika nyumba moja hulazimika kutumia anwani moja ambayo ni namba ya nyumba,” anasema Postamasta Mkuu wa Shirika hilo, Hassan Mwang’ombe.

Anasema maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) imelifanya shirika hilo kuja na suluhisho la kila mwenye simu ya mkononi kumiliki sanduku lake na siyo ‘kushea’.

“Hii inamaanisha kuwa kila mmoja atakuwa na anwani yake binafsi hata kama watu wengi wanaishi katika nyumba moja au wanafanya kazi eneo moja. Hivyo kuongeza usiri wa taarifa binafsi za mtu kwa kuwa zitakwenda moja kwa moja kwa mhusika,” anasema.

Akifafanua zaidi, Postamasta Mkuu huyo anasema huduma hiyo ni rahisi kutumiwa na Watanzania wote kwa kuwa namba ya simu ndio sanduku la posta la mhusika badala ya kutumia lililopo ofisi za Posta.

Hatua hiyo anasema inamwongezea uhuru mwenye sanduku la kuamua wapi apelekewe mzigo wake, kifurushi, kipeto au barua.

Jinsi ya kupata anwani hiyo anasema kila mwenye simu ya mkononi anaweza kujisajili katika huduma hiyo ya Posta Kiganjani. Simumtelezo (simu janja) na baadhi ya vifaa vingine kama kompyuta vinaweza kutumika kusajili mtu katika huduma ya Posta Kiganjani.

Anasema kwa barua au nyaraka au mizigo inayotoka nje ya nchi inatakiwa kuwa na jina la nchi ya Tanzania ili iweze kumfikia mhusika.

Anasema huduma za shirika hilo zinazotumia anwani ya posta kuwa ni usafirishaji wa bidhaa, mizigo, barua, nyaraka, vipeto na vifurushi vya kawaida na vya haraka.

Postamasta Mkuu anataja manufaa ya huduma ya Posta Kiganjani kuwa, ni kila mmiliki wa simu ya mkononi kuwa na anwani yake. Pia ni rahisi kwa mtu kujisajili na huduma ya Posta Kiganjani.

Manufaa mengine anasema ni pamoja na mtu kujisajili na kulipia anwani kwa mwaka mmoja au zaidi, uwezo wa mtu kulipia anwani yake kwa kurudia wakati wowote muda wa malipo ya awali unapokwisha na kuweza kutumia huduma mbalimbali za Posta kwa urahisi.

Jambo analosisitiza Postamasta Mkuu ni kwamba mteja atapewa taarifa ya mzigo wake tangu unapotumwa hadi anapoupokea na hatua zote za usafirishaji kupitia ujumbe mfupi mara tu mzigo wake aliotuma au aliotumiwa unapopokelewa Posta.

Kwa hiyo anasema ataweza kufuatilia mwenendo wa mzigo wake kwa uhuru zaidi pasipo kuhitaji kuuliza au kufika ofisi za Posta.

Vile vile anasema hatua hiyo itamwezesha mteja kubadili mahali pa kupokelea mizigo yake wakati wowote, kuongeza uhuru wa mawasiliano kidijitali na kuliwezesha shirika hilo kumhudumia mteja kwa uhuru zaidi kadri anavyohitaji mteja.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Rais John Magufuli mwaka jana, idadi ya laini za simu za mkononi nchini zinazomilikiwa na watanzania ni takribani milioni 42.9 huku zinazowekewa vifurushi (data) zikiwa milioni 22.

Tafsiri yake ni kwamba, kwa makadirio Watanzania zaidi ya milioni 12 wanaweza kuwa na anwani zao binafsi za Posta hivyo kuwapa urahisi wa kufuatilia mizigo na vifurushi vyao mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi vinavyohusiana na shughuli mbalimbali za kiuchumi, na kuamua mahala pa kuvipokelea na hivyo kurahisisha mawasilinao na kuongeza pato la taifa.

Hivyo ubunifu na maendeleo ya Teknolojia ya Habari na mawasiliano (Tehama) yamesababisha shirika hilo kuja na suluhisho la kila mwenye simu ya mkononi kuweza kumiliki anwani yake ya Posta.

Hata kama watu wengi wanaishi katika nyumba moja au wanafanya kazi eneo moja tofauti na ilivyokuwa zamani kuwa anwani moja inatumiwa na watu wengi kwa mfano kwenye shule anwani inatumiwa na shule nzima, wakiwemo wanafunzi, waalimu pamoja na watumishi wengine, kupitia simu ya kiganjani kila mmoja atakuwa na anwani yake binafsi.

Mkuu wa Mawasiliano wa Posta, Elia Madulesi anasema huduma hiyo ya Posta Kiganjani ni rahisi kutumiwa na watanzania wote, kwani kila mmoja anatumia namba yake ya simu kuwa sanduku lake la barua.

“Tunasema namba yako ya simu ndiyo anwani yako. Badala ya kutumia sanduku la Posta lililopo Ofisi za Posta, mtu anaweza kuwa na sanduku lake dhahiri kwa kutumia simu yake ya mkononi.

Anasema ‘Posta Kiganjani… Twen’zetu Kidigitali!’ ni kaulimbiu ya huduma hiyo mpya ya Posta Kiganjani iliyoanzishwa na shirika hilo.

Mwang’ombe anafafanua zaidi kwamba sera ya Posta ya mwaka 2003 inatamka wazi kuwa kila mtu anatakiwa na anwani hivyo katika kutekeleza hilo Tanzania ilianzisha Anwani za Makazi na Postikodi ambazo zinaendelea kutumika kwa watu wote.

Anasema sababu ya kuanzishwa kwa Anwani za Makazi na Postikodi inatokana na uwepo wa masanduku machache ikilinganishwa na idadi ya watu.

“Hivyo kwa kutumia masanduku ya Posta yaliyopo inalazimisha watu wengi kutumia sanduku moja. Mfano ni watumishi wa taasisi na jamaa zao, makanisa, misikiti, shule na ofisi mbalimbali wote kuendelea kutumia anwani ya taasisi zao hata kama wamehama au wameacha kazi.

“Ili kuondoa changamoto hii Anwani za Makazi zilianza kutumika na sasa tunakuja na Posta Kiganjani,” anasema.

Chanzo: habarileo.co.tz