Dodoma. Pongezi kwa Serikali ya Tanzania zilizotolewa na mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini bungeni mjini Dodoma zimeibua shangwe kutoka kwa wabunge wa CCM.
Mbunge huyo ambaye hivi karibuni alijiuzulu kuwa kaimu mnadhimu wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, ameipongeza Serikali leo Jumanne Januari 28, 2020 alipokuwa akiuliza swali la nyongeza kuhusu upatikanaji wa maji wilayani Rombo.
Selasini amesema hivi sasa katika jimbo lake maji yanatoka, kuishukuru Serikali.
Awali, naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema Serikali imepanga kutumia chanzo cha maji cha ziwa Kyara kufikisha maji Rombo, kwa kuanza inapeleka Sh1.5 bilioni.
"Kwa awamu zote za Serikali na wabunge walionitangulia wamekuwa wakitaka ziwa Kyara litumike kama chanzo cha maji lakini haikuwezekana, lakini Serikali hii naipongeza imewezesha," amesema Selasini.