Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi yawaachia mbunge Matiko, mwandishi

11048 Matiko+pic TanzaniaWeb

Thu, 9 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tarime. Mbunge wa Tarime Mjini,  Ester Matiko, mwandishi wa gazeti la Tanzania Daima Sitta Tuma na wafuasi wengine 14 wa Chadema waliokuwa wamekamatwa na polisi kwa tuhuma za kufanya mkutano usio halali wameachiwa.

Hata hivyo, wametakiwa kuripoti polisi kesho.

Matiko, Tuma na wafuasi hao walikamatwa na polisi jana wakati wa kampeni za kumnadi mgombea udiwani wa chama hicho Kata ya Turwa.

Akizungumza na wanahabari leo Agosti 9 Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Tarime /Rorya Henry Mwaibambe amesema polisi iliwataka wafuasi hao na viongozi watawanyike kwa kuwa mkutano huo siyo halali.

“Mkusanyiko huo haukuwa halali kwa kuwa chama hicho kilikuwa kimezuiwa kufanya mkutano,” amesema Kamanda Mwaibambe.

Pia, amesema baadhi ya wananchi waliondoka lakini wengine walikaidi, ndipo polisi ikalazimika kuwatawanya kwa mabomu lakini watuhumiwa hao walikaidi kuondoka jambo lililolazimu polisi kuwakamata.

“Nilipokea barua jana kutoka kwa Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi Kata ya Turwa ya kusitishwa kwa kampeni za chaguzi za Chadema lakini chama hicho kilikaidi licha ya kupewa barua ya kusitisha mkutano.

“Polisi tulipewa barua ya zuio la mkutano ikionyesha kuwa Chadema wamekiuka kifungu cha 124 A cha Sheria ya Taifa ya uchaguzi,kamati ya maadili ya uchaguzi Kata ya Turwa kupitia kikao kilichoketi Agosti 8,2018 kilichowashirikisha na viongozi wa siasa kilisitisha kampeni za Chadema,” ameongeza.

Amesema Chadema waliambiwa wasifanye mkutano tangu saa sita mchana jana lakini saa kumi jioni kundi la watu zaidi ya 300 walionekana ofisi ya Chadema wakiwa kwenye mkusanyiko.

Mwaibambe amedai mbunge Matiko alitakiwa kuondoka eneo hilo lakini aligoma na kuanza kutukana polisi na hakuna yeyote aliyepigwa wakati wanakamatwa na kupandishwa kwenye gari.

“Kama wamepigwa wakiwa ndani ya kituo hiyo ni ishu,” amesema.

Akizungumzia kukamatwa kwa mwandishi wa habari Mwaibambe amesema;

“Nimepigiwa simu nyingi na media nyingi, waandishi wa habari wakiwamo wa Tarime wakiomba nimwachie Mwandishi mwenzao lakini polisi tumekataa, huyu amekamatwa akiwa kwenye mkusanyiko uliozuiwa. Waandishi wenzake waliondoka yeye akabaki.”

Soma Zaidi:

Chadema watawanywa kwa mabomu Tarime

 

Chanzo: mwananchi.co.tz