Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi yabariki mkutano wa Chadema Mwanza

CHADEMA 660x400 Polisi yabariki mkutano wa Chadema Mwanza

Fri, 20 Jan 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Jeshi la Polisi Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza limebariki mkutano wa hadhara wa Chadema kanda ya Victoria kufanyika kesho katika uwanja wa Furahisha jijini Mwanza, huku likiahidi ulinzi na usalama katika mkutano huo.

Mkuu wa Polisi wilaya ya Ilemela, SSP Ignatus Kapira kupitia barua yenye kumbukumbu namba MZN/B.3/24/VOL.XVII/44 amekiri kuwa na taarifa ya uwepo wa mkutano huo unaotarajiwa kufanyika kesho Jumamosi Januari 21, 2023 katika uwanja wa Furahisha wilayani Ilemela mkoani hapa.

Aidha, SSP Kapira amekitaka chama hicho kikuu cha upinzani nchini kuzingatia kanuni na sheria zinazoongoza mikutano ya kisiasa na hadhara ikiwemo kuepuka maneno ya kashfa, kuzingatia muda wa mkutano ambao unatakiwa kuisha Saa 12 jioni.

Pia amekitaka kuhakikisha hakuna maandamano kabla na baada ya mkutano huo ili kuruhusu barabara za jiji hilo kupitika vizuri bila kuathiri shughuli za wananchi wengine wasiyohusika na mkutano huo.

Kwa upande wake, Katibu wa Chadema Kanda ya Victoria, Zakaria Obad amesema maandalizi ya mkutano huo ambao Mwenyekiti wa Chadema taifa, Freeman Mbowe anatarajiwa kuwa mgeni rasmi yamefikia asimilia 90 huku akisema asilimia 10 zimesalia za ukamilishaji wa utaratibu ndani ya chama.

"Wakazi mkoa wa Mwanza wa wajitokeze kwa wingi kesho kuanzia Saa 3:00 asubuhi katika uwanja wa Furahisha ambapo wazungumzaji wanatarajiwa kuanza Saa 7 mchana. Polisi wametuhakikisha ulinzi kuhakikisha mkutano wetu unakuwa wa amani," amesema.

Obad amesema wanachama wa Chadema katika mikoa ya kanda hiyo wameendelea kuwasili mkoani Mwanza kwa ajili ya mkutano huo ambapo amewataka wafanyabiashara kuchangamkia fursa hiyo kwa kutengeneza bidhaa zinazokidhi maahitaji ya watu hao.

"Tunampongeza Rais Samia kwa kutii sheria kupitia kufungua mikutano ya kisiasa ambayo kwa miaka zaidi ya sana ilizuiwa. Hii itatoa fursa siyo tu kwa vyama vya upinzani bali wafanyabiashara watanufaika kutokana na uwepo wa mikutano hii," amesema

Bila kuwataja majina yao, Obad amesema viongozi wa juu wa chama hicho wamewasili mkoani humo wakiwemo viongozi wa Kamati Kuu, Manaibu Katibu Mkuu, wakurugenzi wa chama na wanachama kutoka katika mikoa ya kanda hiyo.

Chadema inatarajia kuzindua mikutano yake ya kisiasa kesho Jumamosi Januari 21, 2023 katika uwanja wa Furahisha wilayani Ilemela mkoani Mwanza kisha Jumapili mkoani Mara ambapo hoja 10 zinatarajiwa kuwasilishwa na viongozi wa chama hicho kwa kupitia mikutano hiyo kwa Umma.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live