Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi waombwa kukomesha vurugu kwenye kampeni

7c0a947819aefad5d5da39a442ec2a7f Polisi waombwa kukomesha vurugu kwenye kampeni

Tue, 22 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MGOMBEA Ubunge Jimbo la Rombo, Profesa Adolf Mkenda (CCM), ameliomba jeshi la polisi kudhibiti baadhi ya vitendo vya vurugu katika mikutano ya hadhara ya kampeni.

Kauli hiyo inatokana na malalamiko ya baadhi ya wagombea kupitia mitandao ya kijamii, kwamba misafara yao imepigwa mawe na kuharibu mali.

“Mimi kama mmoja wa wagombea ubunge katika jimbo letu la Rombo siungi mkono kwa namna yoyote vurugu katika kampeni, niombe jeshi la polisi kudhibiti na wahusika wachukuliwe hatua kali za kisheria,”alisema.

Mgombea huyo alitaja baadhi ya vipaumbele vyake ni kuanzisha vyama vya ushirika wa mazao mbalimbali yanayolimwa wilayani humo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkenda alisema wananchi wategemee mambo makubwa katika kuinua uchumi wao, ambayo yapo katika vipaumbele vyake ikiwemo kupigania uhuru wa vyama vya ushirika, kuungana na kutawala masoko pasipo kuingiliwa.

Alisema wananchi hawatakuwa na maendeleo iwapo watapuuza suala la ushirika na kuwa na viongozi wa ushirika wasio waadilifu.

Profesa Mkenda alisema mbali na ushirika, pia atashughulikia tatizo la maji kwani vyanzo vilivyopo havitoshelezi mahitaji ya kila siku ya wananchi.

Alisema kipaumbele chake kingine ni kushughulikia ujenzi wa barabara ya kutoka Tarakea hadi Holili inayopita karibu na mpaka wa Tanzania na Kenya.

Alisema anataka barabara hiyo ijengwe kwa kiwango cha lami kutokana na umuhimu wake. Alitaja kipaumbele chake kingine ni kuhakikisha umeme unapatikana katika vijiji vyote vya jimbo hilo, kutokana na baadhi ya vijiji havijapata huduma hiyo kuwepo kwa mradi wa REA.

Alisema wananchi wa Rombo wanahitaji kiongozi, ambaye ni chachu ya maendeleo na mwenye uwezo wa kuwaunganisha na kuhimiza shughuli mbalimbali za maendeleo na kukuza uchumi wao.

Chanzo: habarileo.co.tz