Handeni. Polisi wilayani Handeni mkoani Tanga nchini Tanzania wamemuachia Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba baada ya kukamatwa na kuhojiwa kutokana na kukutwa akifanya mkutano.
Akifafanua suala hilo kwa niaba ya kamanda wa polisi mkoa wa Tanga Edward Bukombe, Kamanda wa polisi wilaya ya Handeni, William Nyero amesema walimkuta Profesa Lipumba na viongozi wengine leo asubuhi Jumapili Januari 26, 2020 wakifanya mkutano wa nje badala ya ndani kama walivyokubaliana.
Amesema wanasiasa wote wanatakiwa kufanya mikutano ya ndani na sio nje ila mwenyekiti huyo na viongozi walikutwa nje wakifanya mkutano.
Nyero amesema, "utaratibu uliopo kwa sasa hakuna kufanya mikutano ya nje kwa mwanasiasa yeyote lakini pia wiki hii wananchi wapo kwenye zoezi la kitaifa la uandikishaji wapiga kura hivyo hakuna ruhusu kufanyika mikutano mingine ambayo itasababisha usumbufu kwenye zoezi hilo."
Hata hivyo, Profesa Lipumba amesema wamekubaliana na polisi kwamba wasiendelee na kazi ya kufungua matawi na kupandisha bendera na badala yake wafanye tu mikutano ya ndani.
Amesema kwa kuwa wameruhusiwa kuendelea na vikao ataendelea na ziara yake kwani amepoteza muda mwingi kwa sababu ambazo polisi walitakiwa tu kumpa maelekezo na sio mpaka kuwekwa ndani.