Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi wadaiwa kuvuruga kongamano CHADEMA

Pambaluu Ed Polisi wadaiwa kuvuruga kongamano CHADEMA

Sun, 5 Sep 2021 Chanzo: ippmedia.com

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimedai Jeshi la Polisi limefunga ofisi zake za wilaya ya Musoma Mjini na kubeba mahema na viti vilivyoandaliwa kwa ajili ya kongamano.

Mkurugenzi wa Itikadi, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa CHADEMA, John Mrema, alisema jana kulikuwa na kongamano la katiba mpya lililokuwa limeandaliwa na Baraza la Vijana Chadema (BAVICHA) wilayani humo.

Alisema Alhamisi Mkuu wa Mkoa wa Mara alitangaza siku ya jana ni kwa ajili ya usafi mkoani humo na kwamba mwananchi ambaye hatashiriki atalipa faini ya Sh. 50,000.

“BAVICHA waliwatangazia wanachama wake na wananchi waje na vifaa vya usafi ili washiriki kufanya usafi na mkuu wa mkoa baadaye wataendelea na kongamano  lililokuwa lifanyike katika ofisi za chama wilaya,” alisema.

Mrema alidai usiku wa kuamkia jana majira ya saa 7:30 usiku, polisi walivamia ofisi hizo na kuchukua mahema na viti vilivyokuwa tayari kushiriki kongamano hilo.

“Leo (jana) asubuhi polisi wamezingira na kufunga kwa kofuli lao geti la kuingilia ofisini na hakuna dalili kuwa wanafanya usafi na badala yake wamewakamata wananchi ambao walikuwa tayari kushiriki ufanyaji usafi,” alidai.

Aliwataja waliokamatwa kuwa ni watu sita ambao ni Patrick Nyabagwe, George Rubare Nahima Seleman, Magret Emanuel, Musila Juma na Medard Shija.

Mrema alisema CHADEMA inafuatilia tukio hilo na kulaani kitu walichokiita ni ukiukwaji na ukandamizaji wa haki dhidi ya raia unaoendelea kufanywa na Jeshi la Polisi.

Akizungumza na Nipashe jana kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara, Longinus Tibishubwamu, alikanusha madai hayo ya CHADEMA kuwa polisi imechukua vitu vyao.

“Leo (jana) tulikuwa na programu ya usafi iliyohusisha vyombo vyote vya ulinzi na usalama, mashirika ya umma, asasi zisizo za kiserikali, wananchi, polisi tulipangiwa eneo la Nyakato ambako ofisi za CHADEMA zipo na eneo lingine ambalo tunaendelea na usafi sasa hivi.

“Kwenye mtandao tuliona mambo mengi wanaandika kuhusu kufanya kongamano la katiba mpya, inaonekana ni kama wanataka kuleta vurugu, nilitoa tamko kama kitu hiki kipo kwenye mkoa huu hatutakubali kifanyike tutakizuia kwa nguvu zote, lakini kwamba tumekwenda kuchukua vitu ofisini kwao si kweli.”

Kuhusu kukamata watu, Kamanda huyo alisema tangu juzi (Alhamis) walikuwa na operesheni ya kukamata vitu vya wizi na kueleza yawezekana na hivyo vimechukuliwa katika mtiririko huo.

“Labda mahema yamechukuliwa kwa kutuhumiwa kuwa ni vitu vya wizi, tumefanya operesheni sehemu nyingi,” alisema.

Alipoulizwa kama ni kweli polisi walifika katika ofisi hizo na kuchukua vitu hivyo, Kamanda huyo alisema hata jambo likifanywa na ulinzi shirikishi au watendaji wa kata wanasema ni polisi.

Kuhusu madai kuwa kuna wananchi wamekamatwa alisema operesheni yao waliyoifanya imekamata watu sita kwa tuhuma za vitu vya wizi.

“Kwenye makosa ya wizi tunakamata mtu yeyote tunachunguza akionekana msafi tunamwachia lakini sasa mtu akikamatwa anajivalisha shati kuwa ‘mimi nimekamatwa kisiasa’ hatuko kisiasa muda wote,” alisema.

Chanzo: ippmedia.com