Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polepole mguu nje, ndani CCM

Polepolepic Data Humphery Polepole

Thu, 16 Dec 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ni saa 72 ngumu! Ndivyo unavyoweza kusema juu ya hatima ya Humphrey Polepole, katibu wa zamani wa Itikadi na Uenezi wa CCM, hali ambayo kutokana na mazingira yaliyopo, inaweza kuamua ama awe mguu ndani au nje ya chama hicho.

Mbunge huyo wa kuteuliwa kwa siku za karibuni ametoa kauli tata zenye tuhuma mbalimbali dhidi ya watendaji wa Serikali na makada wenzake wa CCM.

Kauli hizo zimezua mijadala mikali ndani na nje ya chama hicho, huku baadhi ya makada wenzake wakitaka achukuliwe hatua kwa kuwa anakivuruga chama na Serikali.

Mbunge huyo sasa ana uwezekano wa kukabiliwa na kibano kutoka katika vikao vya juu vya CCM vitakavyoanza kuketi leo na kuhitimishwa Desemba 18, 2021 jijini Dodoma, chini ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan.

Polepole, aliyejipambanua ni mkosoaji wa Serikali inayoongozwa na chama chake kupitia mitandao ya kijamii, amekuwa anatoa maudhui na kuyarusha mitandaoni, ambayo vilevile yamemweka matatani.

Taarifa kwa umma ya Katibu wa Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka ilieleza kuwa kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa cha Jumamosi, saa 72 kutoka leo, kitatanguliwa na vikao vya Kamati Kuu na kikao cha sekreterieti ya Halmashauri Kuu.

Advertisement Ingawa taarifa hiyo ya Shaka ilieleza kuwa vikao hivyo vi vya kawaida vinavyofanyika kwa mujibu wa Katiba ya CCM, lakini macho na masikio ya wengi yataelekezwa katika kujua hatima ya Polepole ambaye siku chache zilizopita aliweka wazi hatang’oka CCM labda wakubwa wamng’oe na pia hataacha kuikosoa Serikali ikivurunda.

Yote hayo yanatokea huku kukiwa na kiporo cha hatua za chama baada ya mbunge huyo pamoja wengine wawili – Askofu Josephati Gwajima (Kawe) na Jerry Silaa (Ukonga) kuhojiwa na kamati za maadili za Bunge na nyingine ya wabunge wa CCM na hatima ya suala hilo haijawekwa wazi.

Wakati Gwajima na Silaa walitiwa hatiani na Kamati ya Bunge kwa kusema uongo, kudhalilisha Bunge na kulishushia heshima na kufungiwa mikutano miwili ya Bunge, Polepole aliunganishwa nao akituhumiwa kushabikia mambo kwenye mitandao.

Soma zaidi: Bulembo amvaa Polepole

Mzizi wa mambo yote ni agizo la Kamati kuu ya CCM iliyoketi Julai 29, 2021 Ikulu Jijini Dar es Salaam, ambayo “ilielekeza kuanza kuchukuliwa hatua wale wote wanaokiuka mienendo, taratibu na kanuni za maadili na uongozi kwa mujibu wa katiba ya Chama Cha Mapinduzi.”

Aitwa TCRA

Wakati majibizano yakiwa yamepamba moto mitandaoni, Desemba 11 Polepole alikutana na waandishi wa habari na kudai kuwa ameitwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuhojiwa juu ya maudhui ya “Shule ya Uongozi’” anayoyarusha kupitia mtandao wa ‘You Tube’ na kuwashambulia baadhi ya watu aliowaita ni wahuni wasiojali masilahi ya Taifa.

Katika mkutano huo, Polepole alisema hangekubali kufungwa mdomo na TCRA au kiongozi yeyote wa Serikali, kwa kuwa Katiba ya nchi inatoa uhuru wa kujieleza na kutoa maoni.

Alisema tayari chama kimeshamhoji juu ya tuhuma zinazomkabili na aliwajibu huku akiweka wazi vitisho na amri anazozipata za kumtaka akae kimya, kwamba havitamzuia kuendelea kukemea hadharani kila Serikali au mtendaji anapokosea.

“Mhuni ni mhuni tu, habadiliki, nitoe rai kwa viongozi wawe macho na wahuni. Awamu ya jana alitukana Serikali leo anakaa upande wa Serikali, sasa naongea, mtu mwingine anaibuka. Hivi mimi niite wahuni halafu mtu na akili zake timamu anasimama na kujijumuisha au kufurahia?” alisema Polepole.

Aliyekuwa mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, Abdallah Bulembo alisema Polepole hamheshimu Rais Samia hivyo Kamati ya Maadili inayoongozwa na Philiph Mangula, makamu mwenyekiti wa CCM (Bara) imuite na kumhoji.

Bulembo alimtaka Polepole kama anataka kutoka ndani ya chama hicho kwenda kuanzisha chama kingine afanye hivyo badala ya kuendelea kuzungumza mambo yasiyoeleweka.

Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye naye amekuwa katika majibizano ya mtandaoni na Polepole ambako alimtaka atoe orodha ya wahuni aliosema walishindwa kumalizwa wakati wa utawala wa John Magufuli, aliyefariki Machi 17, 2021.

Baadhi ya wazee wa mikoa ya Kanda ya Ziwa, wakiongozwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Shinganya, Hamis Mgeja wamemtaka Polepole anyamaze na achukuliwe hatua kwa kukivuruga chama na Serikali.

NEC isikurupuke

Akizungumzia hali hiyo, mchambuzi wa masuala ya siasa, Dk Faraja Kristomus alisema huenda kikao cha NEC kitakachoketi keshokutwa hakitakurupuka kutoa uamuzi au adhabu dhidi ya Polepole, badala yake watafanya tathmini ya nguvu aliyonayo.

“Busara yangu inanielekeza huenda kamati isitoe adhabu kwa haraka, badala yake watafanya tathmini kujua kama nyuma ya Polepole kuna watu wa aina gani na nguvu zao zikoje? Je, wana ushawishi wa kukitingisha au kutetemesha chama?

“Kama watabaini yupo peke yake kwenye harakati anazozifanya basi watamchukulia hatua zinazostahili, lakini kama kinyume chake hawatafanya haraka kama watu wanavyotarajia. Lazima wajiridhishe na mtandao ulioko nyuma ya Polepole,” alisema msomi huyo.

Dk Kristomus ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema anaiona CCM katika maeneo matatu, ikiwemo baadhi ya wafuasi wa Hayati John Magufuli wanaona hawaridhiki na mwenendo wa chama hicho tawala, sintofahamu kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025 na watu kujipanga kwa ajili ya uchaguzi wa ndani wa CCM mwakan.

Wakili Jebra Kambole alisema ingawa hajui ajenda za kamati kuu ya CCM, lakini kikao kina mamlaka pia kuwajadili na kuwachukulia hatua wanachama wanaokwenda kinyume na utaratibu.

“Huenda wakamjadili (Polepole), wakamchukulia hatua endapo watamkuta na hatia kulingana na makosa yanayomkabili, lakini haki itendeke, ikiwemo kumpa nafasi mhusika kujieleza na kusikilizwa kabla ya kutoa uamuzi dhidi yake.

“Mwisho wa siku lazima kuwepo watu wanaokosoa mwenendo wa Serikali, haijalishi watatoka ndani ya chama tawala au upinzani. Kukosoa mwenendo wa Serikali ni jambo la kawaida,” alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live