Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polepole awaonya viongozi wa kuchaguliwa

Mon, 22 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es salaam. Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole amesema wapo viongozi wanaojisahau wakishachaguliwa kuwa viongozi.

Amesema ushindi wanaoupata katika chaguzi zinazoendelea unatokana na imani ya wananchi kwa viongozi wa serikali akiwamo Rais John Magufuli.

Kauli hiyo ameitoa leo Jumapili Oktoba 21,2018 wakati wa mkutano uliofanyika Temeke jijini Dar es Salaam wa kumpokea aliyekuwa diwani wa Mtoni (Chadema), Bernard Mwakyembe aliyejizulu Septemba 25, 2018 na kuhamia CCM

Polepole amesema ili chama hicho kiendelee kuaminiwa na kushinda chaguzi zijazo ni lazima viongozi wakubali kukosolewa na kuheshimu wanachama ambao ndiyo waliowachagua.

"Ni lazima viongozi kuheshimu wanachama ambao ndiyo msingi wa chama, mkishachaguliwa msijisahau kwakuwa wapo baadhi wanaojisahau kama ni watumishi" amesema Polepole.

"Lazima mjue sababu za kuendelea kushinda kwenye chaguzi mbalimbali zinazofanyika, ni kutokana na wananchi kuendelea kuwa na imani na utendaji wa Serikali akiwamo Rais Magufuli," amesema

Naye Mwakyembe amesema yale yote aliokuwa anategemea kufanyika akiwa Chadema tayari Rais Magufuli ameshatekeleza hivyo haoni sababu yakuendelea kubaki.

"Wanaosema nimenunuliwa siyo kweli, CCM hawajanipa hata shilingi mia kilichonifanya niondoke ni utendaji kazi wa Rais na utekelezaji wa yale yote niliotegemea kuyafanya ndani ya Chadema," amesema Mwakyembe

 

Mwakyembe ambaye pia alikuwa mwenyekiti wa Chadema Temeke amesema sababu nyingine iliyomfanya ahamie CCM ni namna Serikali ilivyoondoa watumishi hewa waliokuwa wakiisababishia Serikali hasara.

"Mmeona Serikali imedhibiti mishahara hewa, imenunua ndege mpya na kufufua shirika la ndege, kupunguza matumizi ya Serikali na kuboresha huduma za afya kwa kujenga vituo vya afya, zahanati na hospitali kubwa ya Mloganzila," amesema

Katika mkutano huo, wapo viongozi wa mbalimbali kutoka vyama vya upinzani waliojiunga na CCM akiwamo Katibu wa ACT- Wazalendo Mkoa wa Pwani, Amina Batashi ambaye amesema ndani ya chama hicho haoni kinachofanyika.

"Nimeamua kuungana na CCM kutokana na kazi anazozifanya Rais, amekuwa akifanya kazi zinazowagusa wananchi nikaona sina ninachokifanya ndani ya ACT- Wazalendo  nikaona huku ndio sahihi" amesema Batashi.

Septemba 15, wakati wa kampeni za uchaguzi wa marudio Jimbo la Ukonga jijini Dar es salaam, Mwakyembe alijivua uwanachama wa Chadema na kujiunga na CCM wakati wa mkutano wakufunga kampeni.

Chanzo: mwananchi.co.tz