Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polepole awaibua wabunge upinzani

22860 Pic+polerpole TanzaniaWeb

Sat, 20 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Kauli ya katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Humphrey Polepole kuwa dirisha la wanaohama kutoka vyama vya upinzani litafungwa Desemba, imewakera wabunge wa CUF, NCCR-Mageuzi na ACT-Wazalendo.

Baada ya Polepole kuitoa kauli hiyo Oktoba 7, wabunge watatu wa Chadema; James Ole Milya aliyekuwa Jimbo la Simanjiro, Joseph Mkundi (Ukerewe) na Pauline Gekul (Babati Mjini), walijiuzulu ubunge na kujiunga na CCM, ikitafsiriwa kuwa ni kuwahi ‘usajili’ huo.

Kuhama kwao kumefanya idadi ya wabunge wa Chadema waliohamia CCM kufikia sita huku wa CUF wakiwa wawili, wakati idadi ya madiwani waliohama inatajwa kufikia takribani 130.

Lakini wabunge wa upinzani waliohojiwa na Mwananchi walisema kuna kasoro katika siasa hizo zinazofanywa na chama tawala hasa baada ya tamko hilo la Polepole.

“Siasa hizi zinazofanywa katika mfumo wa vyama vingi hazina tija kwa Taifa lenye umri wa zaidi ya miaka 53,” alisema mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe.

“Kila uchaguzi mdogo gharama yake ni sawa na ujenzi wa hospitali mbili za wilaya. Kusema kwamba sijui kuna dirisha, hizi ni siasa za kilaghai ambazo nazichukia hata kuzitolea maoni. Hakika CCM wamechoka.”

Wabunge CUF watema cheche

Maoni kama hayo yalitolewa na mbunge wa Tanga Mjini (CUF), Mussa Bakari Mbaruku ambaye alisema haelewi kama Polepole anajua maana ya demokrasia.

“Hizi ni siasa za kutishana. Ni kama vile hataki uwepo wa vyama vya upinzani. Hiki wanachokifanya CCM ni kama haikutaka mfumo wa vyama vingi uwepo nchini, bali walikubali kwa shingo upande kipindi cha mchakato wa kuupitisha,” alisema Mbaruku.

“Ninaamini katibu mkuu wao, Dk Bashiru Ally hakubaliani na hiki kinachoendelea kwa sababu tayari kinaleta minong’ono ndani ya makada wa CCM wakihoji wanavyopewa nafasi bila kura ya maoni.”

“Hiki kinachoendelea ni kichekesho cha karne. Naamini hata mataifa yaliyoendelea yanatucheka. Wabunge wa upinzani wawe na subira na tumuogope mwenyezi Mungu.”

Mbunge huyo alidai kuwa anachokifahamu ni kwamba hata hao waliowahi usajili huo hawatateuliwa kugombea 2020 kwa vile wana CCM wameshaanza kuja juu wakitaka utaratibu wa kura za maoni.

Kwa upande wake, mbunge wa Malindi (Cuf), Ally Saleh alidai kauli ya Polepole ni vitisho vinavyolenga kuvuna wabunge na madiwani wengi kadri iwezekanavyo kabla ya muda wa kisheria kumalizika.

“Ukifanya hesabu, Polepole anacheza na akili za watu kwa sababu muda wa kisheria wa kufanya chaguzi ndogo ni mwakani. Ukihesabu ile miezi 18 maana yake ni Desemba,” alisema Saleh.

Mbunge huyo alisema anachofanya Polepole hivi sasa ni kujaribu kuwashawishi wabunge wa upinzani walio mguu mmoja ndani na mguu mwingine nje wasaliti vyama vyao wakiamini kwamba wakishachukua kata au majimbo sasa, 2020 yatakuwa yao.

“Wanachoshindwa kuelewa ni kuwa wanaweza kushinda katika majimbo hayo 2020, lakini wakashindwa majimbo mengine mengi tu. Majimbo mengi ya kusini upinzani unaweza kushinda,” alisema.

“Ninachokiona mimi ni kuwa wanataka kufanya uharamia wa kikatiba wa kupata ile theluthi mbili wanapotaka kufanya mabadiliko ya Katiba. Haya yote Watanzania wanayaona na wanayajua.”

Mwananchi lilipojaribu kuwatafuta wabunge wengine wa chama hicho wanaotajwatajwa kuwa huenda nao wakahamia CCM kuwahi usajili huo wa dirisha dogo, hawakuweza kupatikana kuzungumzia minong’ono hiyo.

Naye mbunge wa Vunjo (NCCR-Mageuzi), James Mbatia alisema Taifa likishajiwekea utaratibu wa kikatiba kama ulivyo mfumo wa vyama vingi, usipofuatwa mara zote matokeo yake ni fujo. “Taarifa ya Global Index kwa mwaka 2018 imesema Watanzania tunashika nafasi ya 153 kati ya 156 ya watu wenye furaha duniani. Yaani tumewashinda Yemen, Syria na Burundi tu,” alisema.

Mbatia ambaye pia ni mwenyekiti wa Taifa wa NCCR-Mageuzi na mwenyekiti mwenza wa Ukawa, alisema mbegu zinazopandikizwa na Polepole zinaligawa Taifa.

Chanzo: mwananchi.co.tz