Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polepole adai Chadema ilimpausha Waitara

Fri, 7 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Katibu Itikadi na Uenezi wa CCM, Hamphrey Polepole amesema mgombea ubunge wa Ukonga, kupitia chama hicho, Mwita Waitara alipotoka Chadema alikuwa amepauka lakini baada ya kuhama ameanza “kudamshi” (kupendeza).

Polepole alisema juzi katika Kata ya Mzimuni Ukonga wakati akimnadi Waitara katika kampeni za ubunge zinazoendelea.

Awali Polepole alimsimamisha Waitara huku akiuliza wananchi “kadamshi hajadamshi” akimaanisha amependeza, na wananchi walijibu kwa kusema “kadamshi” huku wakishangilia

Polepole aliwataka wananchi wa jimbo hilo kumchagua Waitara ili apeleke mawazo yao serikalini kwa kuwa atakuwa huru kuongea na kila kiongozi.

“Mkichagua upande wa pili imekula kwenu kwa sababu hawataki hata kuongea na CCM, sasa mnafikiri watawawakilisha vipi naaendeleo ataleta lini wakati amefungwa mdomo,” alisema.

Kwa mujibu wa Polepole, amepita maeneo mbalimbali kuangalia jimbo hilo na kubaini changamoto kadhaa ambazo anaamini zitatauliwa na Serikali kupitia ilani ya CCM.

Alisema kwa sasa chama chake kimefanya mapinduzi makubwa na kuongeza kuwa jambo hilo linawapa nguvu.

“Siku hizi CCM hakuna figisu kila kitu kitakwenda sawa Waitara alikimbizwa na figisu huko,” alisisitiza.

“Sasa tumepata jembe ambalo linakimbiza na si mwingine ni Rais John Magufuli ambako kwa miaka miwili amefanya mambo yaliyokwama kwa miaka 20,” alisema.

“Lakini watu wanasema hakuna tunachokifanya. Mimi nawaangalia tu na kucheka, treni ikikamilika itarahisisha biashara zenu ambazo zinachelewa kwa ajili ya foleni, lakini watu wanasema hakuna tunachokifanya,”.

Polepole aliwataka wananchi hao kupiga kura kwa wingi na kuichagua CCM.

Katika hatua nyingine, Waitara aliwahakikishia wananchi wa jimbo hilo kuwa atatatua kero zao kwa kuwa yupo chama ambacho hakina shida ya fedha kwa ajili ya kufanya miradi ya maendeleo.

Alisema suala la kuambiwa kuwa amenunuliwa halipo, “Mimi na ujanja huu ninunuliwe, kweli jamani”.

“Mimi nimechoshwa na chama cha kisanii, unaambiwa uende bungeni ukafunge mdomo na plasta hivi kweli ndicho walochonituma wananchi? Amehoji Waitara.

Kwa mujibu wa Waitara, amekuja kwenye chama cha mwalimu wenzake, tena wa masomo ya sayansi ya kemia na hisabati.

“Mimi sina maneno mengi ila nawaahidi uchaguzi ukiisha nakwenda kujenga shule kwa ajili ya wana Ukonga ili watoto wetu wasome.”

Waitara alisema wakati yuko Chadema kipindi cha kampeni hakumuona mwenyeki wa chama hicho, Freeman Mbowe wala mbunge wa Arusha mjini Godless Lema na kwamba alilazimika kufanya mwenyewe tofauti na CCM ambayo vionozi wake wakuu wamemuunga mkono.

“Msiwe na hofu na mimi nimefanya maamuzi sahihi, nimeondoka kule nimechoka kuziba mdomo kwa plasta.

Wakati naondoka Chadema sikumwabia hata mke wangu, niliogopa asije akapata mshtuko. Nilienda mwenyewe Lumumba halafu baadaye nikampigia simu kuwa mimi nimeshahama.”

Aliwataka wana Ukonga wasijali kwani Serikali imesema italeta maji na kuhakikisha maendeleo yanapatikana.

Chanzo: mwananchi.co.tz