CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimemtaka mgombea wa urais Zanzibar kwa tiketi ya chama cha ACT- Wazalendo Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad kuacha kubumbabumba hoja ili kutafuta kiki kwa kuwasema vibaya viongozi wa chama hicho.
Akizungumza na vyombo vya habari, makao makuu ya CCM, Dodoma, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Humprey Polepole alisema anatoa rai kwa mara ya mwisho kwa Maalim Seif aache kutaja majina ya viongozi wa CCM.
Polepole alisema Zanzibar wapo wahasimu wao ambao hawawatakii mema, lakini akasema chama hicho kimefanya mambo mengi na hivyo ni rahisi kwao kupata ushindi.
"Natoa rai mzee huyu aache kutaja majina ya viongozi wetu. Aache CCM ifanye kazi zake, Zanzibar CCM tumefanya kazi nzuri. Itakuwa vigumu kwa vyama vingine kupata ushindi," alisema na kuongeza;
"Wajipange wasitengeneze hoja za kubumbabumba zisizo na mshiko. Kwani amekuwa akisema mambo ya uongo hadharani kutafuta tumshitaki kwa kutuchafua, sisi hatatufanya hivyo," alisema.
Alisema CCM haitamshitaki mwanasiasa huyo, lakini afanye siasa zake na akiachie chama hicho mambo yake.
Alisema CCM imejipanga, vijana wengi wameshaandaliwa kupiga kura na wazee wamerudishwa kwa lengo la kushauri kwa ajili ya chama kusonga mbele.
Alimuonya Maalim Seif kuwa iwe mara ya mwisho, akiendelea kuwachafua viongozi hao watashughulika naye.
"Tumeunda timu ya ushindi ya kwenda kubadilisha na kufanya mabadiliko makubwa kisiwani Zanzibar. Hatutaki kufanya habari za kubumbabumba," alisema Polepole.
Gazeti hili jana liliandika habari kuhusu kauli za Maalim Seif za kudaiwa kuwatia hofu wapigakura.
Umoja wa Vijana wa CCM umelaani kauli zinazodaiwa kutolewa na mwanasiasa huyo mkongwe Zanzibar.
Kwa mujibu wa UV-CCM, kauli za Maalim Seif zinaashiria uvunjifu wa amani wakati huu wa kujiandaa kwa ajili ya uchuguzi mkuu na zinakiuka tamko la vyama vya siasa la kuendelea na kampeni za kistarabu.
Naibu Katibu Mkuu UVCCM, Mussa Haki Mussa aliwaeleza waandishi wa habari kuwa kauli zilizotolewa na mgombea huyo zina lengo la kuwatia hofu wananchi, wasijitokeze kupiga kura na hazikubaliki.
Mussa alisema malalamiko ya kiongozi huyo kuwa baadhi ya wagombea wa ubugne wa ACT-Wazalendo wamewekewa pimgamizi na vyama vingine vya siasa, hayana msingi kwa sababu ni jambo la kawaida kwa wagombea kuwekeana pingamizi na kwamba utaratibu unaotakiwa kufuata ni kukata rufaa.
Mussa alizitaka taasisi zinazoratibu mchakato wa uchaguzi mkuu ikiwemo Tume ya Uchaguzi, Jeshi la Polisi na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, kukemea kauli hizo za Maalim Seif, zinazoenda kinyume na tamko la vyama vya siasa na maadili.