Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Pinda, Makongoro watauweza mfupa wa Waitara Ukonga?

16376 Pinda+pic%255C TanzaniaWeb

Sun, 9 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kwa muda mrefu Chama cha Mapinduzi (CCM) kimekuwa kikiwatumia viongozi wastaafu na makada maarufu wa chama hicho kwenye chaguzi hususani zile za marudio.

Kupitia utaratibu huo ndipo walisikika akina, John Malecela, wakati akiwa makamu mwenyekiti wa CCM na hata baada ya kuachia wadhifa huo.

Kutokana na mafanikio aliyokuwa anapata katika chaguzi hizo Malecela alibatizwa jina la tingatinga.

Nguli huyo alitumia kila aina ya ushawishi akisaidiwa na ukongwe wake kwenye masuala ya siasa, alifanya mikutano ya hadhara, mikutano ya ndani na kampeni za nyumba kwa nyumba na kufanikiwa kushinda upinzani mkali wa vyama vya upinzani.

Hata baada ya mzee huyo kupumzika, CCM bado inatumia mbinu hizohizo katika uchaguzi mdogo wa Ukonga. Imeamua kuwateua tena makada wake wakongwe, Waziri mkuu mstaafu Mizengo Pinda na Makongoro Nyerere kulibeba jahazi.

Makada hawa licha ya kuwa kimya kwenye siasa kwa muda, wana ushawishi na uzoefu kwenye siasa, na pengine ndio kisa wakaibuliwa hivi karibuni na kuteuliwa kuwa wajumbe wa halmashauri kuu.

Ni siku chache tu baada ya uteuzi huo, wamekabishiwa jukumu la kumnadi Mwita Waitara kuhakikisha anashinda.

Makongoro Nyerere

Nyerere amekabidhiwa jukumu la kuwa mlezi wa kuhakikisha anapita katika kila kona kusaka wapiga kura, ili kuhakikisha jimbo lililokuwa mikononi mwa Chadema linarudi CCM.

Kama yalivyo matarajio ya chama chake, Nyerere ana haiba kwenye medani za siasa huku akibebwa na jina la baba yake, Mwalimu Julius Nyerere.

Katika kampeni na ucheshi wake na vitendo vyake vinamwongezea mvuto na ushawishi huko watu wakijaribu kumfananisha na baba yake.

“Kohoa kama baba wa Taifa, anaambiwa na akiwa jukwaani, naye anacheka, “haa haa... nitakohoa kikohozi kikija, baba wa taifa, yaani baba yangu alikuwa anakisubiri kikohozi ndiyo anakohoa,” anasema Makongoro.

Kufahamika ni karata muhimu kwenye uchaguzi huu, kama inavyofahamika yeye ndiyo mtoto wa Mwalimu Nyerere anayeonekana na kutajwa kwenye majukwaa ya siasa.

Makongoro pia amewahi kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya CCM ukiwamo uenyekiti wa chama hicho katika Mkoa wa Mara kuanzia mwaka 2007–2012, Mbunge wa Afrika Mashariki na sasa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM.

Kada huyu pia anaifahamu siasa akiwa na uzoefu pia wa upinzani baada ya mwaka 1995 kutoka CCM, chama kilichomlea na kuhamia NCCR-Mageuzi, ambako alishinda Ubunge wa Jimbo la Arusha Mjini.

Baada ya kumaliza muda wake wa kuongoza jimbo hilo alikaa kimya katika ulingo wa siasa hadi mwaka 2000 alipojiunga tena CCM. Pia, Rais Mkapa akamteua kuwa mbunge mwaka 2004 – 2005.

Anajua mbinu za kupambana ili kushinda kama ambavyo waliomteua kusimamia uchaguzi wa jimbo hilo wanavyotarajia, mwaka 2012 alichaguliwa kuwa Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki.

Mbali na hayo hivi karibuni ameteuliwa tena na Rais John Magufuli, yeye pamoja na Pinda kuwa wajumbe wa NEC.

Tumetoka benchi

Akizungumza katika moja ya kampeni za kumnadi Waitara katika uwanja wa Shule ya Msingi Kivule, ambao mgeni rasmi alikuwa Pinda, anasema alikuwa benchi la ufundi kwa miaka saba na sasa amerudi.

“Nimerudi natokea benchi la ufundi la chama ambako nilikuwa naangalia mchezo unavyokwenda, wapinzani wataweza?” aliwahoji wananchi kwenye mkutano huo na kujibiwa...”Hawaweziiii”.

Anasema aliporudi CCM alisota benchi miaka saba bila kuteuliwa hata kuwa katibu kata, lakini amerudi mstari wa mbele na watalichukua jimbo hilo mapema.

“Mimi na Pinda tulikuwa benchi, yaani wachezaji wa akiba kwa muda mrefu sana, Rais Magufuli ameona tumeusoma mchezo ndiyo maana tumepewa jukumu hili,” anasema.

Kama kawaida ya Nyerere lazima afanye mzaha anapohutubia, alitumia mzaha kueleza namna walivyotolewa benchi kuingizwa mchezoni.

Alisema wakati Rais Magufuli anawanusuru alikuwa na chombo kimoja na boya moja, hivyo akamtupia Pinda, alieleza huku anacheka.

“Akidhani amemaliza, akaniona mimi nikiwa natapatapa na mafuriko yanataka kunifikia na boya ni moja na ambalo tayari amelitumia Pinda na amebaki na ndoano.

“Rais Magufuli akawa hana jinsi kwa sababu anataka kuniokoa akanitumia ndoano, ndoano inauma, lakini nilivumilia maumivu ya ndoano kuliko ya kukaa benchi la ufundi,” anasema.

Anasema hakuogopa kudaka ndoano kuokolewa, licha ya kuwa inaumiza kwa sababu alijua kuna mshipi imara wa CCM ambao haukatiki.

“Leo nipo nanyi huku Ukonga hadi kieleweke, nitapita nanyi kata hadi kata mwanzo mwisho kurudisha jimbo lilikotoka. Mimi na Waitara tulikuwa upinzani, hivyo tunajua vitu vingi na tunatambua kuwa kila kitu ni CCM, hakuna anayeweza kuongoza kwa haki na usawa zaidi ya huku tuliko,” anasema Nyerere.

Mkakati wake

Nyerere anayataja mambo matatu atakayoyasimamia ili kuhakikisha jimbo la Ukonga linarudi CCM, kuwa ni kusema ukweli, kuhimiza wananchi kupiga kura na kampeni ya nyumba kwa nyumba.

“Tunakwenda kulichukua jimbo hili mchana kweupe, tukifanya kazi rahisi kabisa, kuwaeleza wananchi ukweli usio na shaka. Watanzania wamedanganywa sana kwa kupewa ahadi za uongouongo, sasa imetosha ni kusema na kutenda, kusema na kuonyesha kilichofanyika,” anasema Nyerere.

Nyerere anafafanua kuwa mkakati mwingine ni kuhakikisha wanapita nyumba kwa nyumba kusaka kura.

“Inawezekana wapo ambao kwa sababu mbalimbali wanashindwa kuhudhuria mikutano ya hadhara ambako tunanadi sera zetu, tutakutana nao hukohuko majumbani kwao.

“Tutalifanya hili kwa amani na upendo mkubwa kwa sababu Watanzania siku hizi wanaelewa hawahitaji nguvu, matusi wala kutokwa jasho, wanahitaji kueleweshwa kidogo tu,” anasema.

Anasema silaha nyingine watakayoitumia ambayo ni muhimu ni kuwahimiza wananchi kujitokeza kupiga kura.

“Hakuna chama kitakachoshinda iwapo wakati wa upigaji kura wananchi hawatajitokeza, hivyo msisitizo wa yote upo hapa, hili tumelichukulia kama jukumu kuu la wakazi wa Jimbo la Ukonga,” anasema Nyerere.

Mizengo Pinda

Licha ya kufanya kazi kwa muda mrefu Ikulu, ikiwamo kwenye uongozi wa awamu ya pili, tatu na ya nne, Pinda anaifahamu vema siasa.

Kada huyu aliyewahi kushika nyadhifa za ubunge wa Katavi kwa vipindi viwili kimoja akipita bila kupingwa, mwaka 2001 alikuwa Naibu Waziri Tamisemi na baadaye waziri kamili.

Hivyo pilikapilika za kisiasa anazijua ipasavyo, ndio kisa chama chake kilichompa jukumu la kuzindua kampeni za Waitara.

Akizindua kampeni hizo, Pinda anasisitiza mbinu ya kuwapa nafasi mabalozi wa nyumba 10 kwa sababu wao ndiyo shina la chama.

Anafafanua kuwa mabalozi ndiyo wanawajua wananchi wanaoishi kwenye maeneo yao, hivyo wao ndiyo kila kitu na wapewe nafasi ya kusikilizwa.

“Wakati mwingine hawahitaji makuu, wanahitaji heshima tu kutambulika na kusikilizwa maoni yao, tufanyeni hivyo kwani hawa ndiyo tunakwenda kufanya nao uchaguzi,” anasema Pinda.

Pinda pia alitumia mkutano huo kuwataka wapinzani kujitafakari wanakwama wapi badala ya kulalama wanachama wao kununuliwa.

“Anunuliwe nani, ushauri wa bure nawapa wajitafakari maana ukigeuka huku huyu kahama, ukirudi huku mmepigwa uchaguzi.

“Labda wangesema hawa wanaorudi walikuwa kwao kufanya ushushushu. Mnafahamu ushushushu?, lakini dhana kuwa wananuliwa haina mashiko, wajitafakari,” anasema.

Chanzo: mwananchi.co.tz