Mbunge wa Viti Maalum, Cecilia Pareso amedai alipokea wito wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa njia ya WhatsApp na sio kwa njia ya barua pepe, akiwa Dodoma.
Pareso ametoa madai hayo jana Jumanne Novemba 8, 2022, mbele ya Jaji Cyprian Mkeha, wakati akihojiwa maswali mbalimbali na jopo la mawakili wa Chadema, likiongozwa na Peter Kibatala.
Amedai baada ya kupokea wito huo uliotoka kwa Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, aliomba kuongezewa muda wa wiki moja ili aweze kuangalia mazingira yaliyopo ya kwenda kwenye Kamati hiyo, maana kulikuwa na taharuki.
Mawakili hao wa Chadema wamemhoji Pareso kuhusiana na ushahidi wake aliyouwasilisha mahakamani kwa njia ya viapo, katika kesi yake na wabunge wenzake 18, waliyoifungua Mahakama Kuu Masjala Kuu, kupinga kuvuliwa uanachama.
Katika kesi hiyo wabunge hao wanapinga uamuzi wa Baraza Kuu la Chadema wa Mei 11, 2022, kutupilia mbali rufaa walizozikata wakipinga uamuzi wa Kamati Kuu wa Novemba 27, 2020 kuwafukuza uanachama kwa tuhuma za kuapishwa kuwa wabunge bila ridhaa ya Chama.
Wabunge hao 19 wanapinga uamuzi huo kwa utaratibu wa Mapitio ya Mahakama (Judicial Review), wakidai kuwa walifukuzwa isivyo halali kwa kuwa hakwakupewa haki ya kusikilzwa, hivyo wanaiomba mahakama hiyo iutengue.
Akihojiwa na Wakili Peter Kibatala, shahidi huyo amedai kuwa Novemba 25, 2020 alipokea wito kwa njia ya Whatsapp akitakiwa kwenda Kamati Mkuu ya Chadema kwenda kuhojiwa sababu ya yeye na wenzake 18 kuapishwa bungeni jijini Dodoma, bila idhini ya chama hicho.
Pareso amedai baada ya kutumiwa ujumbe huo nae aliujibu kwa njia ya WhatsApp kama alivyotumiwa.
"Shahidi kama katika barua zako hujaifahamisha Chadema kuwa wewe uko Dodoma na si Dar es Salaam kama ambavyo barua ya wito ilivyokuandikia kwa anuani yako ya Dar es Salaam, Kamati Kuu ingejuaje kuwa wewe uko Dodoma? alihoji Kibatala.
Akijibu swali hilo, Pareso amedai kupitia kwa barua ya Chadema waliyomwandikia hawakutaka kujua yeye yupo wapi.
Pia, alihojiwa iwapo kama ni kweli katika kiapo hicho kuna aya inayoeleza kuwa John Mnyika alifanya mkutano na waandishi wa habari siku moja kabla ya kukutumia wito wa barua na kueleza kuwa wabunge hao wapewe notice.
Akijibu suala hilo, Pareso amedai "Mheshimiwa Jaji kwa mujibu wa kiapo changu Mnyika alieleza kuwa tupate public notice ya kikao cha Kamati Kuu," amedai.
Alipoulizwa kuhusu nyaraka ipi itathibitisha kuwa ulikuwa Dodoma, Pareso amedai kuwa ameandika kwenye kiapo chake alichowasilisha mahakamani hapo.
Baada ya kumaliza kuhojiwa na mawakili wa Chadema, Pareso aliulizwa maswali ya kusawazisha na mawakili wake kuhusiana na maswali aliyoulizwa na mawakili wa Chadema.
Baada ya maelezo hayo, mawakili wa Chadema waliiomba Mahakama hiyo, kesho Mbunge wa Viti Maalumu, Jesca Kishoa aitwe mahakamani hapo ili wamfanyie mahojiano kuhusiana na ushahidi wao huo.
Jaji Mkeha baada ya kusikiliza maelezo hayo, ameahirisha kesi hiyo hadi Novemba 9, 2022 itakapoendelea.
Wengine walioitwa kuhojiwa ni aliyekuwa mwenyekiti wa Bawacha, Halima Mdee; aliyekuwa makamu mwenyekiti Bawacha, Hawa Mwaifunga; aliyekuwa Katibu Bawacha, Grace Tendega, na aliyekuwa mweka hazina Bawacha, Ester Matiko; Ester Bulaya, Jesca Kishoa, na Cecila Pareso.
Viongozi wa Chadema wamekuwa wakidai kuwa hawakuwahi kupendekeza, kusaini na kuwasilisha katika Tume Taifa ya Uchaguzi (Nec) orodha ya majina ya wabunge hao kuteuliwa kuwa katika nafasi hiyo, kama sheria inavyoelekeza.
Mbali na Chadema kupitia Bodi yake ya Wadhamini, wadaiwa wengine ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ambaye pia anasimama kwa niaba ya Bunge la Tanzania na Nec.
Mpaka sasa tayari wabunge wanne wa Viti Maalumu ambao ni Hawa Mwaifunga, Grace Tendega, Nusrati Hanje na Cecilia Pareso wamehojiwa na mawakili wa Chadema kuhusiana na ushahidi wao waliouwasilisha mahakamani hapo kwa njia ya kiapo.
Sehemu ya mahojiano baina ya kiongozi wa jopo la mawakili wa Chadema, Peter Kibatala na Pareso na pia Pareso na mmoja wa mawakili wao, Edson Kilatu, akimwongoza kutoa ufafanuzi kwa baadhi ya majibu ya maswali ya dodoso ilikuwa kama ifuatavyo:
Wakili Kibatala: Shahidi katika kiapo chako unasema wito wa kufika kwenye Kamati Kuu ulitolewa chini ya kanuni gani? (kanuni za Chadema)
Pareso: Kanuni ya 6.5.1d
Kibatala: Ni sahihi kanuni hiyo uliyoitaja inaipa Kamati Kuu mamlaka kushughulika baadhi ya mambo kwa dharura?
Pareso: Mheshimiwa Jaji ni kweli kwamba kwa mujibu wa Katiba hii Kamati Kuu inaweza kushughulika mambo kwa dharura.
Kibatala: Shahidi umesema ulipata wito ukiwa Dodoma ni sahihi?
Pareso: Ni kweli
Kibatala: Ni wapi au ni katika nyaraka ipi itathibitisha kuwa ulikuwa Dodoma?
Pareso: Mheshimiwa Jaji hata kwenye kiapo changu nimeandika.
Kibatala: Shahidi umuhimu wa documentary proof (ushahidi wa nyaraka) unafahamu au huufahamu? Au unakumbuka katika majibu chako dhidi ya kiapo kinzani cha Chadema ulisema kuwa Chadema hawajaleta documentary proof kuthibitisha kuwa kuna gharama huwa inaingia kuendesha kikao cha Kamati Kuu?
Pareso: Mheshimiwa Jaji kwa mujibu wa kiapo changu ni kweli.
Kibatala: Kwa hiyo pamoja na kwamba Chadema wameapa kama wewe ulivyoapa lakini umeona ni bado ni muhimu kuleta document?
Pareso: Anayeleta ndio anapaswa kuthibitisha
Kibatala: Kwa nini unataka kuwe na kanuni mbili kwamba wewe kusema tu kwenye kiapo kuwa ulikuwa Dodoma inatosha ila Chadema licha ya kusema kwenye kiapo kuwa wameingia gharama unataka walete na uthinitisho?
Pareso: Kwa sababu ndio utaratibu.
Jaji Mkeha: Shahidi hili swali limezalishwa na jibu lako kwamba wakati unaletewa wito ulikuwa Dodoma, waandishi wa hukumu waangalie nini wajiridhishe kuwa kweli ulikuwa Dodoma?
Katika jibu lako ukasema umeandika kwenye kiapo, na Chadema wakaleta kiapo kinzani wakisema wameingia gharama mkasema (kwenye kiapo chao cha pamoja) haitoshi ilibidi walete ushahidi, sasa kwa nini ninyi mnasema kiapo kinatosha kusema nyinyi mlikuwa Dodoma?
Pareso: Mheshimiwa Jaji wao hawakupinga kwamba mimi sikuwa Dodoma kama ambavyo sisi tulipinga kiapo cha Chadema.
Kibatala: Anampa Pareso kiapo kinzani cha Chadema anamtaka asome aya ya 16 kisha akamtaka aseme kama Chadema walipinga kwamba alikuwa Dodoma au hawakupinga?
Pareso: Anasoma aya hiyo kisha wakili Kibatala akamuuliza:
Kibatala: Sasa ni sahihi Chadema wanasema kuwa wewe hujaleta uthibitisho kwamba ulikuwa Dodoma siku unapokea wito kuhudhuria kikao cha Kamati kuu?
Pareso: Mheshimiwa Jaji kwa mujibu wa kiapo chao wamesema hivyo lakini hawajasema nilikuwa wapi.
Kibatala: Katika barua yako uliyoileta hapa mahakamani ukimjibu Mnyika kuhusu sababu za kushindwa kufika kwenye kikao Tarehe 27/11/2020 kuna mahali umeandika kuwa moja ya sababu ni kwamba wewe upo Dodoma?
Pareso: Kwa mujibu wa barua hii haipo
Kibatala: Shahidi kama katika barua zako hujaifahamisha Chadema kuwa wewe uko Dodoma na si Dar es Salaam kama ambavyo barua ya wito ilivyokuandikia kwa anuani yako ya Dar es Salaam, Kamati Kuu ingejuaje kuwa wewe uko Dodoma?
Pareso: Mheshimiwa Jaji kupitia kwa barua yao waliyoniandikia hawakutaka kujua mimi niko wapi?
Kibatala: Unafahamu kuwa Kamati Kuu ya Chadema Kuna mazingira inaweza kuendelea na shauri upande mmoja? (bila upande mwingine, yaani malalamikiwa kuwapo)
Pareso: Kulingana na mazingira ninakubali.
Kibatala: Unafahamu kuwa msingi wa huo wito kukutaka wewe kwenda Kamati Kuu ilikuwa ni kwenda kujadili kwa nini wewe na wenzako mlikwenda kuapishwa?
Pareso: Mheshimiwa Jaji kwa mujibu wa barua hii ulikuwa ni wito wa kufika mbele ya kikao.
Kibatala: Unafahamu kuwa mpaka leo Chadema wanasisistiza kuwa hawajawahi kukuteua kuwa mbunge wa viti maalum, ni kweli au si kweli?
Pareso: Mheshimiwa Jaji kwa mujibu wa kiapo chao, lakini kwa mujibu wa taratibu hakuna mtu ambaye anaweza kujiteua mwenyewe.
Kibatala anarudia swali hilo na Pareso anajibu kuwa hafahamu.
Jaji: Shahidi nimeshakurekodi kuwa ni kweli lakini ukafafanua kuwa katika hali ya kawaida hakuna mtu anaweza kujiteua, sasa niandike lipi? Maana sasa kuna majibu mawili.
Pareso: Mheshimiwa Jaji ni kweli wameandika hivyo kwenye kiapo chao lakini katika hali ya kawaida hakuna mtu anaweza kujiteua.
Kibatala: katika kiapo chako kuna chochote ulichoambatanisha kuhusu nani walikuwa wajumbe wa Kamati Kuu waliokuvua uanachama tarehe 27/11/2020?
Pareso: Nimeeleza kwenye kiapo.
Kibatala: Hizo miniti za kikao cha Kamati Kuu unazitambua au huzitambui?
Pareso: Sizitambui.
Kibatala: Ni kweli kuwa hamkupewa haki ya kusikilizwa kwenye rufaa yenu?
Pareso: Ni sahihi.
Kibatala: Hizo minute za Baraza Kuu la Chadema za Mei 11/2022 unazitambua au huzitambui?
Pareso: Baadhi ya vitu navitambua baadhi sivitambui
Kibatala: Katika paragrafu ya 27 (ya kiapo chake) unasema kwamba hukupewa haki ya kusikilizwa bali ulipewa nafasi ya kuomba msamaha tu, katika hizo aya unazozitambua (za muhtasari wa kikao Cha Baraza Kuu) ni aya zipi mahakama ikiangalia itaona kwamba ulipewa nafasi ya kuomba msamaha tu?
Pareso: Mheshimiwa Jaji mimi niliitwa kuitambua tu rufaa kisha nikaambiwa nitoke nje.
Pareso: Kwa mujibu wa miniti zao ni aya ya 9.2.e
Kibatala: Hizi aya nyingine za minutes za Baraza Kuu ambazo umesema huzitambui Chadema walizi-forge (walighushi) au zilifikaje?
Pareso: Mheshimiwa Jaji mimi sikuwa sehemu ya kikao hicho.
Kibatala: Katika aya ya 7 ya kiapo chako umeorodhesha maneno aliyoyasema Katibu Mkuu wa Chadema, kabla ya kikao kilichokuvua uanachama hayo maneno yana uhusiano gani?
Pareso: Maneno aliyoyatoa yalinihukumu kabla ya kutusikiliza.
Kibatala: Jaji ataona wapi kuwa Mnyika naye alikaa kwenye kikao cha (Kamati Kuu) kukuhukumu?
Pareso: Mheshimiwa Jaji mahakama yako itaangalia kwenye affidavit (kiapo) ya Chadema.
Kibatala: Hebu soma paragrafu ya 29 ya kiapo chako kisha utuambie ulikuwa unasema nini wewe uliyeapa?
Pareso: Mheshimiwa Jaji hapa nasema waliofanya maamuzi katika kikao kilichotufukuza ndio hao walikuwa sehemu ya kikao cha Baraza Kuu ambako nilikata rufaa yangu.
Kitabala: Ili mahakama ithibitishe Mwenyekiti na Katibu Mkuu wa Chadema walikaa kwenye kikao cha Kamati Kuu kilichowafukuza kisha wakakaa kwenye kikao Cha Baraza Kuu itabidi uangalie minutes ambazo wewe unasema huzitambui ni kweli au si kweli?
Pareso: Mwenyekiti na Katibu Mkuu kuwa sehemu ya wajumbe wa Baraza Kuu ni suala ambalo kilo kwenye Katiba.
Kibatala: Katiba ya Chadema ndivyo inawataja kwamba mwenyekiti na katibu mkuu?
Pareso: Kwa mujibu wa Katiba mwenyekiti na katibu mkuu ni wajumbe wa Baraza Kuu.
Kibatala: Kwa sababu tu Katiba inasema wajumbe wa Kamati Kuu ni sehemu ya wajumbe wa Baraza Kuu ni lazima wote hao walihudhuria siku hiyo ya Mei 11/2022?, kwani hawezi kuwa anaumwa au akakataa tu?, Ni kweli au si kweli kwamba ili kujua wajumbe wa Baraza Kuu waliohudhuria siku hiyo lazima twende kwenye chanzo kingine?
Pareso: Ni kweli lazima kuangalia mahudhurio.
Mahojiano na Wakili Kilatu ili kufafanua majibu ya maswali ya dodoso
Wakili Kilatu: Shahidi umeulizwa kama Kamati Kuu ya Chadema kwa mujibu wa Katiba inaweza kufanya mambo fulani kwa dharura ukajibu kuwa ndio, una nini zaidi cha kujieleza mahakama?
Pareso: Mheshimiwa Jaji ni kweli Katiba inaruhusu masuala ya dharura lakini katika hili hapakuwa na udharura, yaani kuapishwa kuwa mbunge hapakuwa na udharura huo
Kilatu: Pia uliulizwa swali kama kuna mazingira mahakama inaweza kuamua suala la mtu pasipo yeye kuwepo ukasema ndio, iambie mahakama ulikuwa unamaanisha nini?
Pareso: Nilikuwa namaanisha kwamba mpaka inafika hatua hiyo kuna hatua fulani zinakuwa zimefanyika.
Kilatu: Pia uliulizwa kuhusu miniti hapa za Kamati Kuu ukajibu kuwa huzitambui, ulikuwa kwa nini ulisema hivyo?
Pareso: Ni kama nilivyosema kuwa mimi sikuwa sehemu ya kikao hicho, lakini pia hiyo document haikuwa signed (haikuwa imesainiwa)
Wakili Jeremiah Mtobesya (Chadema) anasimama kupinga jibu hilo hasa document kutosainiwa
Jaji Mkeha: Shahidi jitahidi kujibu kwa kadri unavyoulizwa na usitoe majibu ambayo yanaibua mambo mapya ambayo hukuwa umeyasema awali. mfano hiyo ya document kutokuwa signed, maana hukuwa umeisema awali.
Kilatu: Pia ulionyeshwa miniti (za Baraza Kuu) ukaambiwa uonyeshe unayokubali na ukaulizwa Aya nyingine ambazo umesema huzitambui kama zilikuwa forged, unaniambia nini mahakama?
Pareso: Nilisema sizitambui kwa sababu sikuwa sehemu yake.
Kilatu: Pia uliulizwa kuhusiana na barua uliyoandikiwa na katibu mkuu Chadema Novemba 25, 2020 kwa anuani ya Dar es Salaam lakini ukasema ulikuwa Dodoma una nini la kusema?
Pareso: Ni kweli kwamba ninayo makazi Dar es Salaamm na Dodoma, ni kama ambavyo Raise ana Ikulu Dar es Salaam na Dodoma
Kilatu: Umeulizwa suala la documentary evidence kwamba Chadema hawakuleta proof lakini na kwamba na wewe hukuleta hiyo proof zaidi ya kiapo lakini unakataa kiapo chao unasemaje katika hilo?
Pareso: Mheshimiwa Jaji mimi nilikuwa Dodoma kwa sababu tarehe hiyo nilikuwa nimetoka kuapishwa Dodoma kuwa mbunge.
Kilatu: Hilo umejibu kwa upande wako na kwa upande wa Chadema kwamba hawakuleta proof?
Pareso: Mheshimiwa Jaji hapa wameandika tu kuwa gharama zinaweza kuwa beyond Sh160 milioni (kugharimia kikao cha Kamati Kuu) kwa hiyo hawajaleta specific figure (namba halisi ya gharama hizo).
Baada ya Pareso kumaliza kuhojiwa leo, kesho itakuwa ni zamu ya Jesca Kishoa