Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Panda shuka miaka 30 ya CHADEMA

Chademapic Kutoshiriki Panda shuka miaka 30 ya CHADEMA

Sat, 21 Jan 2023 Chanzo: Mwananchi

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kinatimiza umri wa miaka 30 tangu kipate usajili wa kudumu, kikiwa na historia ya pekee kulinganisha na vyama vyote vilivyozaliwa baada ya marejeo ya mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992.

Sifa kuu ya Chadema ni kuwa hakikuanza kama tishio kitaifa, ila rekodi zinaonesha kwamba sio tu kilidhihirisha uwepo wake kila uchaguzi mkuu, bali kilijipambanua kwa ukuaji mdogo kila baada ya muhula wa miaka mitano mpaka kiliposhika ukiranja wa vyama vya upinzani Tanzania.

Tathmini yenye usawa ya safari ya Chadema katika miaka 30, inakupa jawabu moja tu kwamba “ukuaji ni mchakato”, chama hicho kimekuwa kikiamini katika kujijenga chini kwa chini, na matokeo ya jumla yamekifanya kuwa chama kikuu cha upinzani kwa zaidi ya muongo mmoja na robo sasa.

Kiuchambuzi, Chadema urefu wa mafanikio yake unaileta kwenye muktadha, nadharia ya Mwanzi wa Kichina (Chinese Bamboo Tree). Wiki sita za kuchomoza kwake, Mwanzi wa Kichina hufikia urefu wa futi 80. Chadema katika safari yake, kilivitambuka vyama vingi ambavyo hivi sasa vimekuwa vifupi, vipo vilivyofutika kabisa.

Nadharia ya Mwanzi wa Kichina ina maajabu yake. Unapanda mbegu leo, inapita miaka minne pasipo kuchomoza. Huoni hata dalili ya mche kutoka ardhini. Mwaka wa tano huchomoza kisha kufikia futi 80 ndani ya wiki sita. Kuanzia mwaka 2010, Chadema kilianza kurefuka haraka, lakini kilishapitia nyakati ndefu za unyonge.

Kasi ya kurefuka kwa mwanzi wa Kichina inatajwa ni urefu wa senimita 91 (inchi 36) ndani ya saa 24, kwa uwiano wa sentimita 4 (inchi 1.6) kwa saa au milimita moja kila sekunde moja. Ndivyo ilivyokuwa kwa Chadema baada ya Uchaguzi Mkuu 2010, wabunge 48, kutoka 11 mwaka 2005. Nyongeza ya viti 37 kwa mkupuo.

Uchaguzi Mkuu 2015, Chadema walivuna wabunge 73, nyongeza ya viti 25. Kimahesabu, ndani ya mihula miwili, walitengeneza viti vipya 62. Endapo utarudi kutoka mwaka 2005 hadi 1995, ndio utagundua namna ambavyo chama hicho kilitengeneza ukuaji mdogo.

Mwaka 1995, Chadema walipata wabunge watatu wa kuchaguliwa na mmoja wa viti maalumu, jumla wanne.

Mwaka 2000, walivuna wabunge wanne wa kuchaguliwa na mmoja viti maalumu, hivyo kuwa watano.

Mwaka 2005, wabunge wa kuchaguliwa watano na viti maalumu sita, jumla 11.

Kutoka mwaka 1995 mpaka 2000, Chadema waliongeza mbunge mmoja wa jimbo, vivyo hivyo mwaka 2005. Hata hivyo, mwaka 2010, Chadema walitengeneza viti vipya 18 vya majimbo, hivyo kufikisha 23, kutoka vitano.

Uchaguzi Mkuu 2015, Chadema walifikisha viti vya majimbo 36, ikiwa ni nyongeza ya viti 13 kutoka 23 mwaka 2010. Vilevile, chama hicho kilikuwa na wastani mzuri wa kura za ubunge, ndiyo maana kiliongeza viti maalumu, kutoka kimoja mwaka 2000 hadi sita mwaka 2005, kisha 25 mwaka 2010 na 37 mwaka 2015.

Upekee wa Chadema Uchaguzi Mkuu 1995, kilijitosa kikiwa sio tishio. Hakikuwa na mgombea urais, zaidi kiliamua kumuunga mkono Augustino Mrema, aliyegombea urais kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi.

Katikati ya Uchaguzi Mkuu 1995 na Julai Mosi, 1992, uliporuhusiwa mfumo wa vyama vingi vya siasa, kulifanyika uchaguzi mdogo kwenye majimbo matano. Kwahani (Zanzibar), Ileje (Songwe, wakati huo ikiwa Mbeya), Kigoma Mjini (Kigoma), Tabora Kaskazini na Igunga (Tabora).

Majimbo manne, CCM waliyatetea kwa urahisi, lakini Kigoma Mjini ambako Chadema walimsimamisha Dk Aman Walid Kabourou, CCM walipata tabu.

Awali, mgombea wa CCM, Azim Premji alitangazwa mshindi, lakini alivuliwa ubunge muda mfupi baada ya kuapishwa. Jimbo lilibaki wazi kusubiri uchaguzi mkuu.

Uchaguzi Mkuu 1995 ulipofanyika, Chadema walivuna majimbo matatu; Kigoma Mjini kupitia Dk Kabourou, Karatu alikoshinda Dk Willibrod Slaa na Rombo kwa tiketi ya Justin Salakana. Walipata kiti kimoja cha viti maalum, alichoketi Mary Kabigi.

Vyama vingine vilivyopata wabunge mwaka 1995 ukikiweka CCM pembeni ni Cuf (viti 28), NCCR-Mageuzi (19) na UDP (4). Kisha, mwaka 2000, Chadema waliongeza jimbo na kufikisha manne, wakitetea mawili; Karatu (Dk Slaa) na Kigoma Mjini (Dk Kabourou), wakapata mapya mawili, Hai (Freeman Mbowe) na Moshi Mjini (Philemon Ndesamburo). Viti maalumu walipata kimoja kupitia kwa Grace Kiwelu.

Kutoka mwaka 1995 mpaka 2000, UDP walibaki palepale, walivuna wabunge wanne, NCCR-Mageuzi walishinda kiti kimoja na kupoteza 18. Cuf nao walipoteza viti saba, kutoka 28 hadi 21. TLP waliingia kwa kishindo mwaka 2000, walishinda wabunge watano.

Mwaka 2005, UDP walikuwa na kiti kimoja, sawa na 2010. TLP nao walipata kiti kimoja 2005, vivyo hivyo 2010. NCCR-Mageuzi waliibuka mwaka 2010 kwa viti vinne vya ubunge na kimoja cha kuteuliwa, lakini mwaka 2015, walipata kimoja.

Muhtasari huo, unaonesha kuwa Chadema ndio chama pekee cha upinzani chenye mwendelezo chanya wa matokeo ya ubunge. Jedwali lake la matokeo linaonesha ukuaji tangu kilipoanza harakati, tofauti na vingine ambavyo hali yake ni sawa na bahari, maji kupwa maji kujaa.

Muundo wa kitaasisi Kutoka mwaka 2005 hadi sasa, Chadema kimepitia misukosuko mingi. Lawama kubwa ni muundo unaomtazama mtu mmoja, Mbowe, kuliko taasisi. Kwamba kila aliyewahi kuutamani uenyekiti wa chama hicho, aliunguzwa na moto.

Hata hivyo, rekodi zinaibeba Chadema kuwa wakati vyama vingine vimewahi kukutana na dhoruba kwa sababu ya kujiweka kwenye mabega ya watu, chenyewe hakijawahi kuporomoka.

NCCR-Mageuzi kilidondoka kutoka viti 19 mwaka 1995 mpaka kimoja mwaka 2000, baada ya mgogoro, chama kikasambaratika, Mrema akajiunga na TLP, kilichovuna viti vitano mwaka 2000. Mwaka 2005, nguvu ya Mrema ilikuwa imeshuka, wakapata kimoja. Mwaka 2010, TLP walivuna kimoja kupitia Mrema mwenyewe. Mwaka 2015, wakabaki na sifuri.

Cuf baada ya mgogoro wa uongozi, uliosababisha aliyekuwa Katibu Mkuu, Seif Sharif Hamad, ajiondoe na kutimkia ACT-Wazalendo, kimepoteza nguvu kubwa. Hivi sasa ACT wanashiriki Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Zanzibar.

Rejea Chadema, wenyeviti wawili walistaafu kwa amani; Edwin Mtei na Bob Makani, hivi sasa usukani ameshikilia Mbowe tangu mwaka 2003. Pengine, aina ya uondokaji wao ulikuwa bora ambao ulijenga msingi wa mabadilishano ya uongozi.

Ukirejea nafasi nyingine za juu; Katibu Mkuu wa pili wa Chadema, Dk Kabourou, alihama na kujiunga na CCM. Wakati Kabourou anahamia CCM alikuwa Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara. Kuhama kwake hakukuiteteresha Chadema.

Kadhalika, mwaka 2008, Chadema waliingia kwenye mgogoro wa nafasi ya Mwenyekiti. Aliyekuwa mbunge wa Tarime na Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara, Chacha Wangwe, alitofautiana na Mbowe. Chacha alisema chanzo cha mgogoro ni yeye kutaka kuwa Mwenyekiti.

Julai 2008, ikiwa ni katikati ya mgogoro huo, Chacha alifariki dunia kwa ajali ya gari na kusababisha minong’ono mingi kuhusu njama za mauaji. Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Democratic (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, alitoa simulizi kuwa mhusika wa kifo cha Chacha ni viongozi wa Chadema.

Mtikisiko wa Chacha ukiwa haujapoa, ukaibuka mwingine wa Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe, ambaye alikuwa mmoja wa wabunge nyota, walioitangaza na kuipa hadhi Chadema. Zitto alitangaza kumkabili Mbowe kuwania uenyekiti wa chama hicho.

Pamoja na baadaye Zitto kujitoa kwenye kinyang’anyiro, hali ya kisiasa ndani ya Chadema haikuwahi kurudi kuwa sawa tena. Kwa muda mrefu, tangu mwaka 2009 mpaka 2014, chama kilionekana kina makundi mawili, timu ya Mbowe na Zitto.

Baada ya Uchaguzi Mkuu 2010, ikiwa dhahiri Chadema walipata wabunge wengi na walikuwa wanaelekea kuunda kambi ya upinzani bungeni, Mbowe na Zitto, kwa pamoja walitangaza kuwania uongozi wa kambi.

Uamuzi wa wabunge wa Chadema ilikuwa kutazama uandamizi kwenye chama, Mbowe kwa vile alikuwa Mwenyekiti, akawa Kiongozi wa Upinzani na Zitto kwa nafasi yake ya Naibu Katibu Mkuu, alichaguliwa kuwa Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani.

Novemba 2013, waraka wa siri ulioandikwa na waliokuwa viongozi wa Chadema, Profesa Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba, ukimsigina Mbowe na kumkweza Zitto kwamba ndiye angefaa kuwa Mwenyekiti, ulivuja.

Matokeo ya waraka huo yalisababisha Kitila, Mwigamba na Zitto watimuliwe uanachama. Uanachama wa Zitto uliendelea kwa muda kwa sababu alikimbilia mahakamani ambako ilitolewa amri ya kuzuia ajadiliwe na chama mpaka kesi ya msingi ambayo aliifungua ipatiwe majibu. Zitto alipinga uamuzi wa awali wa kumvua nafasi zake za uongozi.

Pamoja na Zitto kuondoka Chadema kuelekea Uchaguzi Mkuu 2015, bado chama hicho hakikuyumba kwenye matokeo. Zitto, Kitila na Mwigamba, wote walijiunga na ACT-Wazalendo.

Chadema kilipata mapigo mengi kuelekea Uchaguzi Mkuu 2015, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema Tanzania Bara, Said Arfi, alijiondoa kwenye chama na kwenda kujiunga na CCM.

Pigo kubwa zaidi lilikuwa la Dk Slaa, aliyetangaza kujitenga na uamuzi wa Chadema, kumpokea Waziri Mkuu wa Nane wa Tanzania, Edward Lowassa, na kumfanya kuwa mgombea urais. Slaa alitangaza kujiuzulu siasa na kujivua uanachama.

Matokeo ya Uchaguzi Mkuu 2015, yalionyesha kuwa Chadema walifanikiwa zaidi kulinganisha na ilivyokuwa mwaka 2010, hivyo ni rahisi kupitisha jawabu kuwa kuondoka kwa Slaa na viongozi wengine tajwa, haikuwa na athari hasi.

Kisha, kuelekea Uchaguzi Mkuu 2020, Chadema iliwapoteza wabunge wengi waliorejea CCM kwa kauli ya kuunga mkono juhudi za aliyekuwa Rais, Dk John Magufuli. Vilevile wajumbe wa Kamati Kuu, Lowassa, Waziri Mkuu wa Saba, Fredrick Sumaye, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara, Profesa Abdallah Safari na wengine.

Msingi wa Chadema Heshima kwa Mtei na Makani maana waliiasisi na kuiongoza Chadema katika nyakati za unyonge, kwa ruzuku duni, bila kuwa na wabunge wengi.

Mbowe baada ya kushika uongozi wa Chadema, alitambua kuwa ushiriki wa vijana kwenye siasa za nchi ulikuwa mdogo. Alitambua pia kuwa ukiwa na chama ambacho ni kivutio cha vijana hapo umeua.

Mbowe alitengeneza na falsafa za uwekezaji wa chama kwa vijana vyuoni. Kati ya mwaka 2003 na 2005, Chadema kilipitia mabadiliko kutoka kuwa chama chenye taswira ya kujengwa na wazee na kugeuka chama cha vijana wa kizazi kipya cha siasa.

Hadi sasa, Chadema kimekuwa chama kinachovutia zaidi vijana, hasa wasomi. Mkondo huo umebebwa na vyama vingine. Hivyo, ni rahisi ‘kubeti’ na kushinda ukisema kuwa Chadema, kwa miongo miwili sasa, kimekuwa chama chenye kukua ndani ya vijana, kuliko kubebwa na majina maarufu ya wanasiasa. Ndio sababu kipo.

Swali je, baada ya kile kinachoitwa na wengi kwamba ni uchafuzi wa Uchaguzi Mkuu 2020, bado Chadema ni imara? Ruhusa ya mikutano ya hadhara uzinduzi wao Mwanza leo, utatoa majibu.

Chanzo: Mwananchi