Maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za mitaa mwakani na uchaguzi mkuu 2025 ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), yanatarajiwa kuanza rasmi wiki hii kwa uzinduzi wa operesheni maalumu yenye jina ‘+255 Katiba mpya'.
Operesheni hiyo itakayozinduliwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe Mei 13 mwaka huu mkoani Kigoma, itakuwa ya saba tangu chama hicho kilipozindua operesheni ya kwanza mwaka 2004.
Operesheni nyingine zilizofanyika kwa nyakati tofauti ni “Operesheni Kata Funua”, “Operesheni Chadema ni Tawi”, “Sangara”, “Chadema ni Msingi”, “Vuguvugu la Mabadiliko (M4C)” na “Operesheni Mshike Mshike.”
Chadema kimetangaza kuzindulia operesheni hiyo kanda ya Magharibi ya chama hicho yenye mikoa ya Katavi, Rukwa na Kigoma huku mkutano wa kwanza ukitarajiwa kufanyika Kigoma Mjini, Jumamosi hii na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama akiwamo Mbowe.
Ingawa Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema hakuwa tayari kuweka wazi jina la operesheni hiyo alipozungumza na waandishi wa habari, gazeti hili limejuzwa na mmoja wa wajumbe wa kamati kuu kuwa, 'operesheni hii itaitwa +255 Katiba mpya'.
Hata hivyo, katika mkutano wake na waandishi wa habari Mei 5, mwaka huu, Mrema alisema operesheni hiyo itaanza katika mikoa ya kanda ya Magharibi...“na itakuwa operesheni kwelikweli na maalumu.’’
Mrema alisema tayari timu ya baadhi ya viongozi akiwamo Naibu Katibu Mkuu-Bara, Benson Kigaila imeshatangulia Kigoma pamoja na baadhi ya wajumbe wa sekretarieti kukamilisha maandalizi ya oparesheni hiyo.
“Baada ya Kigoma, operesheni itaendelea katika Kanda ya Victoria yenye mikoa ya Mwanza, Geita na Kagera. Kisha Kanda ya Serengeti yenye mikoa ya Mara, Simiyu na Shinyanga.
“Wakati maandalizi yanakamilika katika mikoa hiyo, mengine yanakamilishwa visiwani Zanzibar ambako Naibu Katibu Mkuu-Zanzibar (Salum Mwalimu), atasimamia suala hilo,’’ alifafanua.
Akizungumzia operesheni hiyo mmoja wa wajumbe wa Kamati Kuu ambaye hakuwa tayari jina lake kuandikwa gazetini alisema: “Tumeamua kutumia +255 badala ya neno Tanzania na ni maalumu kwa kudai Katiba Mpya ambayo tumekuwa tukiipigania kwa miaka zaidi ya 10 sasa. Dalili njema tunaiona chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.’’
Alisema operesheni hiyo itafanyika nchi nzima ikianzia Kanda ya Magharibi, na itakwenda mikoa, wilaya, majimbo, kata, vijiji na vitongozi vyote nchi nzima. Tutaifanya kwa mwaka mmoja hadi Mei mwakani na kila ngazi tutakuwa tunafanya chaguzi. “Tunatarajia hadi Mei mwakani tuwe tumekwishafanya uchaguzi ngazi ya Taifa, ili kujiandaa na uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwaka 2025. Hii itakuwa ni operesheni ya kipekee sana itakayokwenda sanjari na usajili wa wanachama kwa njia ya kidijitali,” alisema.
Mchakato Katiba Mpya
Mchakato wa Katiba mpya uliokwama mwaka 2014 kwa hatua ya Katiba Pendekezwa,umeonyesha ishara ya kufufuliwa na Rais Samia Suluhu Hassa na tayari mwishoni mwa wiki, alikutana na viongozi mbalimbali wa Serikali na kumwagiza Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi kuitisha mkutano wa Baraza la Vyama vya Siasa ili kujadili suala hilo.
Mbali na Katiba, baraza hilo linalojumuisha vyama vyenye usajili wa kudumu litajadili maboresho ya sheria mbalimbali za uchaguzi.
Walichosema wachambuzi
Akizungumzia kinachokwenda kufanywa na Chadema, Mhadhiri wa Rasilimali watu na Utawala Bora, kutoka Chuo Kikuu cha Tumaini tawi la Dar es Salaam (TUDARCo), Dk Lazzaro Swai alisema kinachofanywa na Chadema ni mbinu ya kuipa ajenda yao ya kisiasa sura na mvuto kwa umma. “Unajua siasa inaendeshwa kimkakati kama ilivyo kwenye mambo mengine, hapa wanachokifanya ni kulipa jambo sura na mvuto mbele ya jamii. Katika siasa kunatafutwa uungwaji mkono na mvuto pekee,’’ alisema
Dk Swai alifafanua mbinu hiyo inarahisisha ufikishaji ujumbe kwa haraka kwa jamii, akirejea kilichowahi kufanywa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere katika kilimo.
“Baba wa Taifa alitumia mbinu kama hizi katika kilimo, alikiita kilimo cha kufa na kupona, kilimo ni uti wa mgongo na kauli mbalimbali, hawa wenzetu wanatumia operesheni ni mkakati wa kisiasa kufikisha ujumbe, lakini kuutengenezea mvuto,” alisema.
Aidha, kwa mujibu wa mchambuzi wa masuala ya siasa, Mwalimu Magabilo Masambu, operesheni hizo, zimetajwa kuwa chachu ya taswira mpya katika siasa na zinaongeza kujulikana kwa chama husika cha siasa.
“Hizo zinasaidia kuamsha ari ya wanachama wapya kujiunga kwa sababu wanakitambua chama, lakini zinaongeza utambulisho wa chama husika kwa wananchi,” alisema.
Alipendekeza operesheni hizo zifanyike baada ya utafiti utakaobainisha ukweli wa namna chama kinavyotambulika katika eneo husika. Pia, alisema zinapaswa kufanyika zaidi vijijini ambako aghalabu wachache ndiyo wanaotambua vyama vya upinzani, ili kuongeza utambulisho.
Katiba mpya bungeni
Jana, bungeni jijini Dodoma suala la Katiba na sheria za uchaguzi liliibuka wakati Mbunge wa Kiteto (CCM), Edward Ole Lekaita alipompongeza Rais Samia kwa kuendelea kusukuma suala la Katiba mpya, akisema siku za mwishoni mwa juma wameona vikao vinaendelea.
“Naomba Serikali mlete Sheria ya Tume ya Uchaguzi na Sheria ya Msajili wa vyama vya Siasa kwa ajili ya kujiandaa ,” alisema Lekaita wakati akichangia bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka 2023/24.
Akiendelea kuchangia, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama alisimama kutoa taarifa akisema kwa tamko la Rais Samia la Mei 6 mwaka huu hadi sasa Ofisi ya Waziri Mkuu, Msajili wa Vyama vya Siasa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), tayari wameshajipanga kuitisha kikao cha wadau kupitia Baraza la Vyama vya Siasa.
Alisema lengo ni kuhakikisha mchakato wa Katiba Mpya unaendelea.
“Na sheria hizi zilizozungumzwa na mbunge naomba kulihakikishia Bunge lako tunataka kabla ya mwaka huu kuisha ziwe zimeshafanyiwa kazi kusudi kila jambo liende kwa wakati,” alisema.
Hata hivyo, Naibu Spika Musa Zungu alitaka wabunge kumpongeza Rais Samia kwa kuridhia mchakato huo kuendelea. Kauli hiyo ilimfanya Ole Lekaita kusema namna bora ya kumpongeza Rais Samia ni Serikali kuleta sheria hizo ili wazipitishe kwa haraka.
Lissu atetema
Akihutubia mkutano wa hadhara Kibaigwa, Wilaya ya Kongwa, mkoani Dodoma, jana, Makamu Mwenyekiti wa Chadema-Bara, Tundu Lissu alisema utamaduni wa viongozi wengi kupita bila kupingwa ni sababu ya wananchi kutopata maendeleo katika maeneo yao.
“Sasa kama hujamchagua mbunge au diwani huyo kiongozi wa namna gani? Na atakuteteaje na kukusemea wakati hukumpigia kura, unapiganiwa na mtu uliyempigania,” alisema mwanasiasa huyo ambaye ni mwanasheria kwa taaluma.
Aliwaambia wananchi hao kuwa hata mbunge wao, Job Ndugai ambaye ni spika mstaafu wa Bunge ni miongoni mwa wabunge waliopita bila kupingwa.
“Ndugai amepita bila kupingwa katika mkoa wa Dodoma wenye majimbo 10. Kati ya hayo sita walipitishwa bila kupingwa, mkoa wa Morogoro wenye majimbo 17 wabunge saba wamepitishwa bila kupingwa.
Akiendelea kujenga hoja, alisema Bunge zima kuna wabunge wa majimbo 28 walipita bila kupingwa na kwa upande wa madiwani nchi nzima kata ziliopo ni 3,956 kati ya hizo madiwani 872 walipita bila kupingwa.
Alisema sheria ya uchaguzi ya Tanzania inasema baada ya uchaguzi mkuu kukamilika tume itatangaza matokeo ya Rais, jimbo kwa jimbo nchi nzima na kuyachapisha kwenye gazeti la Serikali.
“Hatua hiyo inakamilisha uchaguzi mkuu, mwaka 2015 walichapisha matokeo na yapo hadi kwenye mitandao wa tume, mwaka 2010 yapo lakini matokeo ya mwaka 2020 hayapo,” alisema Lissu ambaye mwaka 2020 aligombea urais
Alisema ugumu wa suala hilo unatokana na Katiba iliyopo inayoeleza matokeo ya uchaguzi yakishatangazwa hakuna kwenda mahakamani wala popote kupinga, hivyo wananchi wamekosa watetezi kote hadi ngazi ya Rais.