Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nyalandu awataka Watanzania kuwaombea Mbowe, Matiko

29811 Nyalandu+pic TanzaniaWeb

Mon, 3 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Waziri wa zamani Lazaro Nyalandu leo Jumapili Desemba 2, 2018 amewataka Watanzania kuwaombea watu waliowekwa kizuizini nchini Tanzania akiwemo mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter, mbunge huyo wa zamani wa Singida Kaskazini ameandika, “Jumapili  ya leo tuungane sote kumwombea mwenyekiti Mbowe, Matiko na wote waliowekwa kizuizini popote Tanzania.”

“Kwa sababu moja, au nyingine imeandikwa haki huinua Taifa. Wenye Mamlaka wakaone fahari kutenda haki bila kukawia zaidi. Kama Taifa, tusimame pamoja nao.”

Mbowe na Matiko walifutiwa dhamana na Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri, anayesikiliza kesi hiyo Novemba 23, 2018 kutokana na maombi ya upande wa mashtaka yaliyodai wameshindwa kuhudhuria mahakamani bila sababu za msingi katika kesi yao iliyopangwa kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali.

Viongozi hao wamekata rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam chini ya hati ya dharura wakipinga uamuzi wa Mahakama ya Kisutu kuwafutia dhamana katika kesi ya jinai inayowakabili mahakamani hapo.

Juzi, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ilisimamisha usikilizaji wa rufaa ya Mbowe na Matiko hadi rufaa ya Serikali itakapoamuliwa na Mahakama ya Rufani.

Uamuzi huo uliotolewa na Jaji Sam Rumanyika unamaanisha kwamba, Mbowe  ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na Matiko ambaye ni mhazini wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) wataendelea kusota gerezani kwa siku zisizojulikana wakisubiri Mahakama ya Rufaa kupanga siku ya kusikiliza rufaa hiyo.



Chanzo: mwananchi.co.tz