Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nyalandu akomalia tume huru ya uchaguzi

28266 Pic+nyalandu TanzaniaWeb

Thu, 22 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kada wa Chadema, Lazaro Nyalandu ameitaka Serikali kuifumua Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kabla ya chaguzi kubwa zijazo.

Nyalandu ambaye kabla ya kuingia Chadema alikuwa mbunge wa Singida Kaskazini (CCM), ametaka uteuzi wa viongozi wa juu wa Nec ufanywe na chombo kingine kilicho huru badala ya mfumo wa sasa ambao unampa mamlaka Rais kuteua mwenyekiti, makamu mwenyekiti na mkurugenzi.

Viongozi hao hufanya kazi kwa kushirikiana na wakurugenzi wa uchaguzi katika ngazi ya halmashauri ambao pia ni wateule wa Rais.

Nyalandu ambaye wadhifa wake wa mwisho serikalini ulikuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, alisema mfumo wa sasa hauna tofauti kama mtu akisema CCM ndiyo inateua viongozi na watendaji wa Nec.

Nyalandu ambaye ngazi yake ya kwanza ya uwaziri ilianzia Novemba, 2010 alipoteuliwa kuwa naibu waziri wa viwanda na biashara, alisema hoja yake ya kudai tume huru ya uchaguzi haihusiani na madai ya Katiba Mpya, akisema iliyopo inaweza kufanyiwa marekebisho madogo na Bunge kwa kuridhia kipengele cha mabadiliko kitakachoruhusu kuwapo kwa tume huru.

“Namna pekee ya kupata tume huru ni kupitia Constitutional Amendment (mabadiliko ya Katiba). Katiba yetu hii tunaweza kufanya marekebisho mahsusi yanayohusiana na tume ya uchaguzi, yakapelekwa bungeni na yatakayopitishwa na Bunge yawe ni utashi wa wananchi wengi ili tusiwe na malalamiko tena juu ya tume hiyo,” alisema Nyalandu.

Alisema kwa hali iliyopo sasa nchini, Serikali inatakiwa kurejesha imani juu ya mfumo na uendeshaji wa chaguzi kwa kuwa ni jambo linaloungwa mkono na wabunge wengi bila kujali tofauti ya vyama vyao.

Alisema tume huru ndiyo itakayoamua kwa haki kwamba, nani mshindi wa nafasi ya uongozi kuanzia ngazi ya serikali za mtaa, udiwani, ubunge hadi urais katika chaguzi hizo.

Alipendekeza pia kuanzishwa kwa mjadala wa madai ya tume huru akisema hiyo inachagizwa na mahitaji ya Watanzania wenye itikadi na wasiokuwa na itikadi za vyama, mashirika ya haki za kiraia, taasisi za dini ya kutaka mabadiliko.

Jana, katika ukurasa wake wa Tweeter Nyalandu aliandika: “Tujiandae kushiriki chaguzi za 2019 na mwaka 2020. Refa katika mechi yoyote sharti awe huru na asiegemee upande wa timu yoyote. Tanzania ipate tume huru ya uchaguzi. Wenye mamlaka (Serikali ya CCM) wasiogope ushindani wa kisiasa, ukiwa unapendwa (na wananchi) hakika utashinda.”

Alipotafutwa ili kutoa ufafanuzi kuhusu ujumbe wake huo, Nyalandu alisema kiongozi yeyote anayefanya kazi yake kwa weledi, hana wasiwasi na kuchaguliwa kwake na kwamba uchaguzi ni sauti ya Mungu isiyodhihakiwa na mwanadamu yeyote.

“Huwezi kuwa na uchaguzi sahihi, wa haki na huru bila kuwa na tume huru ya uchaguzi. Kama kiongozi ameteuliwa na Kamati Kuu ya CCM, akawa na weledi, anafaa na akasimamishwa (kushindana) na kiongozi mwingine wa upinzani ambaye anaahidi kushinda, wenye mamlaka wasiogope,” alisema Nyalandu

Alisema katika karne ya 21, hakuna chama chochote cha kisiasa kitakachoendelea kushinda kwa kutegemea msaada wa nguvu ya dola bila kutekeleza matakwa ya wananchi.

Nyalandu ambaye hajatangaza nia katika uchaguzi ujao alipendekeza vyama upinzani kuungana badala ya kupanga kususia kushiriki chaguzi hizo zijazo.

Kususia chaguzi

Kuhusu hatua ya Chadema kususia chaguzi kutokana na madai ya hujuma, Nyalandu alisema pamoja na kwamba matukio hayo yamekuwa yakijitokeza, ipo haja ya kuja na mkakati wa kudumu wa kukabiliana na hali hiyo.

“Tumeshuhudia matumizi ya nguvu za dola katika chaguzi za madiwani, wabunge hata hizi za marudio na kila mtu ameshuhudia, sasa ili tusiendelee katika hali hii tunaomba tume huru ya uchaguzi, utakaosimamia ngazi zote,” alisema Nyalandu.

“Ningefurahi kama Chadema wakishirikiana na vyama vingine ili kuwa na nguvu zaidi, wapinzani kwa pamoja wana uwezo mkubwa wa kushinda viti vya kutosha vya ubunge, udiwani na hata urais, tunachotakiwa kutambua ni kwamba anayeshinda ni Mtanzania, kwa hiyo sitegemei hata Chadema wakishinda urais wawe na ushindi wa milele, CCM inaweza kabisa ikashindwa na upinzani kama kuna tume huru ya uchaguzi,” alisema.

Tume ya Jaji Warioba

Wakati wa mchakato wa Katiba Mpya, Tume ya Jaji Joseph Warioba ilikuja na mapendekezo ikiwamo kubadili jina la tume na kuwa Tume Huru ya Uchaguzi.

Pia, Tume ya Warioba ilipendekeza sifa za wajumbe wa tume huru ya uchaguzi ziwekwe kwenye Katiba huku ikielekeza kuwa wajumbe wake watapatikana kutoka miongoni mwa watu wenye sifa zilizoainishwa ndani ya Katiba kwa kuomba.

Kwa mujibu wa mapendekezo ya tume ya Warioba, majina ya waombaji yatachambuliwa na kamati ya uteuzi ambayo mwenyekiti wake atakuwa Jaji Mkuu na wajumbe wengine sita ambao ni majaji wakuu wa nchi washirika, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, maspika wa mabunge wa nchi washirika na Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu.

Tume hiyo ilipendekeza kwamba kamati ya uteuzi itapendekeza majina ya watu wanaofaa kwa Rais ambaye atateua mwenyekiti, makamu mwenyekiti na wajumbe wengine. Bunge litathibitisha uteuzi wao.

Pia, tume hiyo ya Warioba ilipendekeza kuwa tume hiyo huru ya uchaguzi ndiyo iwe na majukumu ya kusimamia masuala ya uchaguzi, kura ya maoni na usajili wa vyama vya siasa.



Chanzo: mwananchi.co.tz