Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nondo za Mpina bungeni

Nishatipic Data Mpina Nondo za Mpina bungeni

Wed, 8 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

‘Hajawahi kupoa.’ Hilo ni neno unaloweza kulitumia pale unapomtaja Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina ambaye ameendelea kuwa mwiba kwa mawaziri bungeni tangu hajawa waziri na hata alipoteuliwa na kisha kutenguliwa nafasi yake.

Mpina amekuwa akipeleka moto kwa mawaziri na karibu kila mkutano wa Bunge, hulipua mijadala mikubwa inayotawala kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Hata hivyo, mwenyewe anasema moto wake siyo wa mabua tena hatarajii kufumbwa mdomo alimradi anawatetea wananchi na hamuonei mtu katika kila jambo analoibuka nalo, bali hujiepusha na mambo ya uzushi na yanayoharibu taswira ya nchi.

Baadhi ya mawaziri wanamuona Mpina kama shubiri kutokana na hoja zinazowagusa katika wizara zao, ambazo nyingi huhitaji utulivu ili kuweza kulipatia jambo husika ufumbuzi wake bila kukurupuka.

Miongoni mwa mawaziri waliowahi kuingia ‘anga’ za Mpina ni wale wa sekta za fedha, ujenzi na miundombinu, kilimo, nishati na wa katiba na sheria.

“Ndugu yangu sitaki kukurupuka na wala sitapenda kuwa mkurupukaji; nasimamia ninachoona kinamaslahi kwa watu wangu na Tanzania kwa ujumla, kwa hiyo nitaendelea kuhoji ili kwa pamoja tulisaidie Taifa na chama chetu,” alisema Mpina aliyezaliwa Mei 5, 1975.

Alieleza hayo alipoulizwa na gazeti hili mwishoni mwa wiki kuhusu mwendelezo wake wa kuibua hoja bungeni, ambapo mara kadhaa zimekuwa zikikinzana na mawaziri, huku kukiwa na dhana kuwa amekuwa shubiri kwa Serikali kwa sababu ya kukosa uwaziri.

Mpina aliingia bungeni kwa mara ya kwanza mwaka 2010 akitokea katika nafasi ya mtendaji wa kata na tayari.

Katika Serikali ya awamu ya tano chini ya hayati John Magufuli, Mpina aliteuliwa kuwa Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira kabla ya kupewa jukumu la Waziri wa Mifugo na Uvuvi, anakokumbukwa kwa sakata la upimaji wa samaki kwa kutumia rula kwenye mgahawa wa Bunge jijini Dodoma.

Mbali ya kupima samaki kwa rula, kitu kilichowaacha watu wengi midomo wazi, aliingia pia katika mgogoro na wavuvi waliolalamika kuhusu kuporwa na kuchomewa nyavu zao, sambamba na ufilisi wa vyombo vilivyotumika kusafirisha samaki ambao hawakuruhusiwa.

Moto wa Mpina bungeni

Baadhi ya mitandao ya kijamii inamtaja mbunge huyu kuwa amekuwa akiishambulia Serikali, kwa hasira za kukosa uteuzi, ingawa mwenyewe anapinga hilo kwa madai halima uhusiano na anachokisimamia kwa ajili ya wananchi.

Cheche zake zilianzia katika Bunge la 10 ambalo lilikuwa chini ya Spika Anne Makinda pale alipoamua kuigomea bajeti ya Serikali, kwa alichokieleza kuwa mambo hayakuwa yakienda sawa ikiwemo matumizi serikalini.

Katika sakata hilo, aliyekuwa Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa (sasa ni marehemu) alikutana na joto kali, baada ya kushindwa kumjibu hoja alizokuwa ameuliza jambo lililozua mjadala mrefu kiasi cha kutofikia mwafaka.

“Siku ile nilikuwa tayari kwa lolote alimradi niisaidie nchi yangu, lakini ulitumika ujanja wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, alinitoa nje kisha milango ikafungwa nami nikashindwa kupiga kura,” anasema Mpina alipoeleza kuhusu misimamo yake.

Anakiri mara nyingi amekuwa akionekana kama mtu mwenye hasira au anaewatega wengine, lakini kwake mawazo ya namna hiyo hayajawahi kumjia katika kipindi chote, bali anatamani kuwa mkweli na kuusimamia.

Mbali na uamuzi huo, amekuwa mwiba mchungu kwa wawaziri baada ya kusimamia hoja zake ikiwemo masuala ya tozo, malipo katika kampuni ya Symbion na ukomo wa deni la Serikali.

Hoja nyingine alizoibua ndani ya Wizara ya Fedha, ni matumizi kupita ukomo wa bajeti ya Serikali, kesi 1,097 zilizokalia Sh360 trilioni na matumizi anayotaja kuwa hayana tija ndani ya Serikali wakati umasikini ukizidi kwa wananchi.

Wizara nyingine zilizopitia tanuri la Mpina ni Ujenzi na Miundombinu, hasa kuhusu mikataba ya ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) .

Aliomba ufanyike ukaguzi maalumu kutokana na namna zabuni zilivyotolewa kwa baadhi ya makandarasi.

Kwa sekta ya nishati, aliwahi kuichachafya kwa sababu ya kukatikatika kwa umeme na ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere.

Kuhusu kilimo, aliwahi kutaja ufisadi uliomo kwenye mchakato wa ununuzi wa mbolea ambayo kwa madai yake, ulisababisha kupanda kwa gharama za ununuzi wa mbolea nchini.

Mbali na hoja hizo, Mpina alishaibuka na hoja za matumizi ya fedha kupita ukomo wa bajeti ambapo alishawishi iundwe tume kuchunguza matumizi yasiyofuata kanuni za Bunge.

Aidha, aliwahi kusema ni aibu kuchekelea Sh1.3 trilioni za mkopo wa Uviko- 19 wakati kuna kesi zimekalia zaidi ya Sh360 trilioni, ambazo kama zingesimamiwa kusingekuwa na haja ya mkopo.

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Wakili Frederick Kalonga anasema kinachofanyika kwa mawaziri siyo kumkomoa Mpina lakini wanaoumizwa ni Watanzania wanaotaka kusikia ukweli.

Kalonga alisema ni haki ya mbunge kutumia nafasi yake kuibua hoja na Serikali inapaswa kujibu, kwani hoja haijibiwi kwa kusema maneno binafsi na udhaifu wa mtu badala yake hoja inajibiwa kwa hoja.

“Kwanza yule ni mbunge, anajitambua na alishawahi kuwa serikalini, kwa hiyo hakuna asichokijua mbunge huyu. Anapouliza anapaswa kujibiwa, kuacha kujibu hawatendi haki na anayeumia ni Mtanzania,” anasema Kalonga.

Anaeleza kuwa kumekuwa na tabia kwa baadhi ya mawaziri kutojibu hoja, huku wakikimbilia kumsema mtu, lakini uongozi wa Bunge unaacha jambo linalofifisha uhuru wa mawazo kwa wengine na akamuomba Mpina kutokata tamaa wakati wote.

Kauli zake bungeni

Akizungumza kuhusu kauli zake ndani ya Bunge, Mpina mwenye shahada ya uzamivu ya sayansi ya fedha aliyoipata Chuo Kikuu cha Strathclyde nchini Uingereza mwaka 2010, anasema hazina maana tofauti na wala hafikirii kumchukia mtu bali anaipenda Serikali na chama chake, ambacho hapendi kionekane kikipoteza mvuto kwa kushindwa kuisimamia Serikali.

Mpina ambaye hupendelea vazi la kaunda suti wakati wote awapo bungeni, alisema moto huo ataendelea kuwa nao hadi mwisho wa utumishi wake kwa wananchi na Watanzania na nia yake ni kutaka mawaziri wajikite katika kujibu hoja lakini siyo mambo binafsi.

“Siwazuii kusema wanachotaka kusema.Mimi nasimama na Tanzania na Watanzania wenzangu, ningependa watu watambue kuwa nilianza kupinga maombi maovu hata kabla ya kuwa Waziri na nilipovua joho la uwaziri nikarudia misimamo hiyo,” anasema Mpina.

Mbunge wa Liwale (CCM), Zuber Kuchauka alisema si kila hoja inayopelekwa bungeni inakuwa na mashiko bali zingine huwa za kutafutia alichokiita kiki.

Kuchauka alisema baadhi ya wabunge wamekuwa na mtindo wa kubeba hoja hata ambazo zilishapatiwa majibu ilimradi wasikike katika vyombo vya habari ingawa akasisitiza mawaziri nao kuwa na majibu yenye kuwa na mfanano wa kweli.

“Pande zote zinaweza kuwa na shida, mtoa hoja na mjibu hoja, lakini tuzungumze kuhusu matumizi nje ya bajeti, hivi mnasahau kuwa Mpina alikuwa Waziri katika Serikali ya awamu ya tano ambayo iliongoza kwa matumizi makubwa nje ya bajeti, hili la juzi kila Mbunge anajua ila nashangaa kaja nalo ukumbini,” alisema Kuchauka.

Kuhusu majibu ya Waziri alisema huenda yalitokana na mambo yao wawili hao lakini kwa taratibu za kibunge hakupaswa kumjibu hivyo.

Mbunge wa Viti Maalum, Conchesta Rwamlaza alisema mawaziri ndiyo wamekuwa na matatizo wakati wa kujibu hoja za wabunge kwani hata kama Mbunge angeuliza au kuibua hoja isiyokuwa na mashiko ipo namna ya kumjibu.

“Badala yake Mawaziri wetu hawajibu hoja wao wanachokitazama ni nani kauliza, sasa hiyo siyo nzuri tena haina Afya kwa bunge, mawaziri wanatakiwa kujibu hoja,”alisema Rwamlaza.

Mbunge wa zamani wa viti maalum (Chadema), Roda Kunchela alisema tatizo linalowasumbua mawaziri ni Bunge kuwa la upande mmoja ambapo wanatamani kusikia kila kitu kiwe Cha ndiyo hivyo wakipata kinyume na hapo ndipo inapoanzia shida.

Kunchela alisema muundo wa bunge unawanyima nafasi watu wenye uwezo kuzungumza baadhi ya mambo ya kuisaidi Serikali yao kwa sababu ya hofu kwamba wataonekana wasaliti.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live