Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nondo atetea nafasi yake uenyekiti ngome ya vijana ACT Wazalendo

Abdul Nondo Ushindii Nondo atetea nafasi yake uenyekiti ngome ya vijana ACT Wazalendo

Thu, 29 Feb 2024 Chanzo: Mwananchi

Ni huzuni na furaha imetawala baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa ngome ya vijana ya ACT- Wazalendo yaliyompa ushindi Abdul Nondo aliyefanikiwa kutetea hicho kwa mara ya pili mfululizo.

Nondo amefanikiwa kushinda kiti hicho, baada ya kuwashinda wapinzani wake Julius Massabo, Petro Ndolezi na Ruqayya Nassir baada ya kupata kura 66 sawa asilimia 55.4. Kwa mujibu wa Joran Bashange ambaye ni mwenyekiti wa kamati maalumu ya uchaguzi ACT- Wazalendo, aliyemfuatia Nondo ni Massabo 45, sawa na asilimia 37.8, Ndolezi kura saba sawa na asilimia 5.8 na Nassir kura moja sawa na asilimia 0.8.

Nyuso za baadhi ya wagombea wa uenyekiti, ujumbe wa halmashauri kuu na mkutano mkuu zilionekana kuwa na huzuni wakati matokeo hayo yakitangazwa na Joran Bashange ambaye ni mwenyekiti wa kamati maalumu ya uchaguzi wa chama hicho.

Wakati Nondo na wafuasi wake wakifurahi wakati wote kabla ya matokeo kutangazwa na baadhi walionekana na furaha zaidi baada ya kuruhusiwa kuingia ndani ya ukumbi kusikiliza matokeo.

Abdul Nondo amefanikiwa kutetea nafasi yake ya uenyekiti wa ngome ya vijana ya ACT-Wazalendo katika uchaguzi uliohudhuriwa na wajumbe 119 waliopiga kura za kuwachagua viongozi hao.

Katika uchaguzi wa mwaka 2020 Nondo alimshinda Wiston Mogha. Lakini leo Februari 29, 2024 amemshinda mpinzani wake karibu Massabo ambaye katika uchaguzi wa mwaka 2020 alikuwa namba tatu.

Awali Mwanasiasa machachari na mbunge wa Embakasi ya Mashariki nchini Kenya, Paul Owino maarufu 'Babu Owino' amewataka vijana wa Kitanzania kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika chaguzi zinazofuata.

Mwanasiasa huyo, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mkutano huo amesema mwaka huu na mwakani kuna uchaguzi hivyo lazima vijana wajitokeze kuwania viti kwenda bungeni na kwenye mabaraza ya madiwani.

"Najua tunatoka katika familia zisizojiweza na masikini lakini ni wewe kijana utakaoibadilisha familia yako na Taifa kwa ujumla kwa kuhakikisha Serikali inaboresha huduma za jamii, kuanzia leo vijana mkitaka kitu pigania usingoje kupewa, kwa sababu hautapewa lazima usimame upiganie," amesema Babu Owino.

Babu Owino amesema Tanzania na maeneo mengine vijana hawana ajira na kwa nyakati tofauti kundi la vijana limekuwa likiambiwa ni ndio viongozi wa kesho, lakini amewataka kuwaachana na msemo na kutambua wao ni Taifa la leo, kesho na keshokutwa.

"Hakikisheni nyie ni viongozi wa leo kesho, keshokutwa, lazima vijana tuamke na kujipigania na tujinasue na mnyororo wa umasikini na uongozi mbovu, jambo hilo litafanywa na viongozi kama nyinyi.

"Lazima tuwe na viongozi bora, sio bora viongozi piganieni nchi yenu, Julius Nyerere, Kwame Nkurumah na Rashid Kawawa walianza wakiwa vijana, Babu Owino bado kijana wewe unangoja nini? Kama kijana.

Kuhusu ACT- Wazalendo

Katika hatua nyingine, mwanasiasa huyo amewapongeza viongozi wa ACT - Wazalendo kwa namna wanavyokiongoza chama hicho tangu kilipoanzishwa mwaka 2014 hadi hivi sasa.

"ACT- Wazalendo ina mizizi katika nchi ya Tanzania, Kenya tunakitambua ndio maana nimekuja, nisingekitambua nisingekuja leo hapa, kuwepo kwangu leo hapa najisikia bashasha na furaha tele kama kibogoyo aliyefanikiwa kupata jino moja tu

"Chama cha ACT-Wazalendo, kinazingatia hoja na masilahi ya Watanzania na vijana ndio maana kuna baraza kivuli linalowasaidia na kuwajenga kuwa viongozi wa leo na kesho," amesema Babu Owino.

Katibu Mkuu wa ACT- Wazalendo, Ado Shaibu amesema chama hicho, kinawategemea vijana na hakiwezi kutekeleza malengo pasipo kushirikisha kundi hilo lenye watu wenye weledi, maarifa, shupavu, walio tayari kwa mapambano na wenye mioyo ya kujitolea kufanya kwa ujenzi wa chama na Taifa.

Chanzo: Mwananchi