Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

‘Nikishinda uchaguzi nitakomboa wakulima’

2912341261af3c3aebae0696382d8c7c ‘Nikishinda uchaguzi nitakomboa wakulima’

Wed, 9 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MGOMBEA ubunge kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika Jimbo la Sumbawanga Mjini mkoani Rukwa, Shadrack Malila ameahidi kufanya mapinduzi makubwa katika kilimo.

Alitoa ahadi hiyo wakati akizindua kampeni zake na kuahidi kuwakomboa wakulima katika umasikini wa kipato kupitia kilimo. Malila alizindua kampeni katika uwanja wa Ndua uliopo Kata ya Kizwite katika Manispaa ya Sumbawanga.

Katika mkutano huo alitaja vipaumbele vinane. Alisema tayari amezungumza na Kampuni ya OCP - Tanzania ya Mfalme wa Morocco na imekubali kupima bure afya ya udongo kwenye mashamba ya wakulima.

Malila alisema, mtambo wa kupima afya ya udongo utawekwa katika Kijiji cha KatumbaAzimio mwishoni mwa Oktoba. “Wakulima tutawafuata huko huko mliko mtapimiwa bure ili ifahamike udongo unahitaji aina ipi ya mbolea au unahitaji chokaa peke yake... nina mtandao mkubwa ndani na nje ya nchi nimesomea digrii yangu ya pili Amerika nako nina wadau kibao,” alisema.

“Nje ya bunge nimeyafanya mengi pamoja na kuwapeleka wafanyabiashara nchi jirani ya DRC, je, nikiwa Mbunge.. .naomba kura zenu na za madiwani wote 18 ili tutekeleze haya,” alisema Malila.

Alisema kama atachaguliwa atawasiliana na kampuni ya Chamwino Lime ya Dodoma inayotengeneza chokaa ya kilimo ili iwasambazie chokaa wakulima ambao udongo katika mashamba yao utabainika kuwa na tindikali nyingi.

Alisema endapo atachaguliwa, kipaumbele kingine kitakuwa kuanzisha Benki ya Wananchi Rukwa itakayotoa mikopo kwa wanawake na vijana kwa riba nafuu.

“Tutahamasisha ujenzi wa maghala ya kuhifadhi nafaka vijijini kwa gharama nafuu, ujenzi wa barabara zitakazounganisha kijiji na kijiji ambazo zitapitika mwaka mzima na kuhimiza kilimo cha maharage ili wakulima walime mara tatu kwa mwaka,” alisema.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema katika Mkoa wa Rukwa, Zeno Nkoswe, aliwaomba wananchi wamchague Malila kwa kuwa ana uwezo wa kuwavusha kimaendeleo.

Chanzo: habarileo.co.tz