Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ni vita vya CUF, ACT ubunge wa EALA

Bunge La E Ni vita vya CUF, ACT ubunge wa EALA

Tue, 20 Sep 2022 Chanzo: Mwananchi

Ni vita kati ya Chama cha Wananchi (CUF) na ACT Wazalendo katika kuiwania nafasi moja ya ubunge wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EALA).

Vyama hivyo vya upinzani vitachuana kuwania nafasi hiyo ya uwakilishi katika uchaguzi utakaofanyika wiki hii.

Katika kinyang’anyiro hicho, Chama cha Mapinduzi (CCM), ACT Wazalendo na CUF ndivyo vitakavyoshiriki baada ya Chama cha Demokrasia a Maendeleo (Chadema) kujiondoa kwa kutoyatambua matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 yaliyokuwa na kasoro.

Katika uchaguzi wa mwaka 2017, CUF na Chadema vilichuana kuwania nafasi tatu kati ya tisa zilizopo kwa kila Taifa mwanachama wa Jumuiya ya Afrka Mashariki (EAC) baada ya CCM kuchukua nafasi sita wakiwamo wawili kutoka Zanzibar na wanne wa Bara.

Kwa uwiano wa Bunge mwaka huu, CCM itakuwa nafasi nane huku ACT-Wazalendo na CUF wakinyang’anyana moja.

Uchaguzi wa kuwapata wabunge wapya wa EALA utafanyika Septemba 22 baada ya kuteuliwa kesho, saa 10 jioni.

ACT-Wazalendo wamemteua Ado Shaibu ambaye ni katibu mkuu wao wakati CUF kikipitisha majina 12 akiwamo Sonia Magogo ambaye ni mbunge wa EALA tangu mwaka 2017 na Habib Mnyaa anayewania nafasi hiyo kwa mara nyingine.

Wengine ni Jafar Mneke, Zainab Mndolwa, Mashaka Ngole, Queen Lugembe, Adui Kondo, Thomas Malima, Mohammed Ngulangwa, Zainab Abdul, Anderson Ndambo na Husna Mohemed Abdallah.

Akizungumza na gazeti hili jana, Magogo alisema “nimeshaanza kuomba kura nje ya Bunge baada ya kuchaguliwa na chama changu.”

Akizungumzia uchaguzi huo, Katibu wa Uenezi na Mawasiliano kwa Umma wa ACT- Wazalendo, Salim Bimani alisema mgombea wao ni Shaibu baada ya Pavu Abdallah kuridhia kujiondoa.

“Kwa sasa tunamuunga mkono Ado kwa kila hali na tunafanya kampeni usiku na mchana ili kijana wetu ashinde. Tunawaomba wabunge wamuunge mkono kwa sababu ataiwakilisha vema Tanzania ndani ya Eala,” alisema Bimani.

Tofauti na ACT-Wazalendo, CUF wao wamepeleka wagombea 12 na kuwagawa katika makundi manne kwa mujibu wa kanuni namba 6(2) za EALA ambayo ni wanawake, wagombea wa Zanzibar na wagombea wa Tanzania Bara.

Katika kundi la vyama vya upinzani, ndilo litakalotoa mwakilishi mmoja wa upinzani kwenye bunge hilo la EALA.

Uchaguzi huu unafanyika huku ACT-Wazalendo ikiunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), nafasi iliyokuwa ya CUF kwa miaka mingi kabla ya uchaguzi wa mwaka juzi hivyo huenda wakanufaika.

CCM imeshapitisha majina manane ya wagombea watakaowania nafasi za makundi yote muhimu ukiondoa la upinzani.

Waliopitishwa ni Nadra Juma Mohamed, Dk Abdulla Hasnuu Makame na Machano Ali Machono. Wengine ni Angela Kizigha, Dk Shogo Mlozi, James Ole Millya, Dk Ng’waru Maghembe na Anar Kachambwa.

Akizungumzia hatua hiyo, wakili wa kujitegemea, Jebra Kambole alisema kwa hali ilivyo, wabunge wa CCM ndiyo watakaomua hatima ya mgombea wa CUF na ACT Wazalendo kwenda Bunge la EALA.

Chanzo: Mwananchi