Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ni mwendo wa vikumbo tu huko CCM

Uvccm Pic Data Vikumbooo Ni mwendo wa vikumbo tu huko CCM

Tue, 19 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Joto la uchaguzi wa ndani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na jumuiya zake, limeendelea kuongezeka ambapo zaidi ya vijana 100 wamejitosa kuwania uenyekiti wa Jumuiya Umoja wa Vijana (UVCCM).

Uchaguzi huo umefikia hatua ya wilaya, mikoa na Taifa ambapo dirisha la uchukuaji lilifunguliwa Mei 29 na litahitimishwa Agosti 10 mwaka huu.

Nafasi ya Mwenyekiti wa UVCCM ipo wazi tangu Juni, 2021 baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kumteua Kheri James kuwa Mkuu wa Wilaya ya Ubungo.

James alikuwa Mwenyekiti huku Makamu wa UVCCM, Tabia Mwita naye akiteuliwa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi kuwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo.

Pamoja na nafasi nyingine zinazogombewa, wadhifa wa Mwenyekiti wa UVCCM taifa, ndiyo unaotajwa kuwa na wagombea wengi zaidi ya nyingine.

Taarifa ambazo Mwananchi imezipata ni kwamba watu 100 wamejitokeza kuwania nafasi hiyo huku watatu kati yao ndiyo wanaotajwa kuchuana vikali

Kwa muda mrefu uchaguzi wa viongozi wa UVCCM umekuwa na mtifuano kila unapowadia kutokana na jumuiya hiyo kutegemewa na chama kusaka kura za viongozi katika chaguzi.

Miongoni mwa wagombea wanaotajwa kutoa upinzani mkali ni Vian Nchimbi, Japhari Kubecha na Rashid Mohamed.

Akizungumza kuhusu uchaguzi huo, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka alisema umekuwa na mwamko mkubwa ukilinganisha na chaguzi zilizotangulia.

“Mambo yapo vizuri kwa mara ya kwanza wanachama wamepata hamasa kubwa na wameitikia mwito wa kwenda kuchukua fomu kugombea,” alisema.

Alipoulizwa kuhusu idadi ya waliochukua fomu ngazi ya taifa kuwania nafasi mbalimbali, alisema ni vigumu kuwahesabu kwa sasa, kwa kuwa bado mchakato wa uchukuaji fomu unaendelea.

Hata hivyo, Shaka alisema siku za uchaguzi huendana na ngazi husika na kwamba, utafanyika hadi Desemba kulingana na ngazi hizo.

Naye Katibu Mkuu wa UVCCM, Kenani Kihongosi alisema mchakato wa uchukuaji fomu unaendelea, uchambuzi haujafanyika na atatoa taarifa zote pindi kazi hiyo itakapokamilika.

Said Msonga ni Mchambuzi wa Masuala ya Siasa, alisema mwamko wa wagombea wa nafasi hasa ya uenyekiti wa vijana umetokana na unyeti wa wadhifa husika.

Alisema nafasi hiyo inampa kijana nafasi ya kuonekana na kuwa karibu na viongozi wakubwa, jambo ambalo ni hutamaniwa na wengi.

“Vijana wanaonyesha kuwa wana dhamira ya kutumika nafasi ndani ya chama chao, kwa upande mwingine nafasi hiyo ni kama fursa,” alisema.

Pamoja na mwamko huo, Msonga alisema wadhifa huo unahitaji kijana mwenye uwezo mkubwa kuitumikia.

Kwa kuwa CCM imebadili mwelekeo wa siasa zake, alisema anahitajika kijana mwenye uwezo wa kufanya siasa za ushindani na kushawishi wengine kutoka ndani na nje ya chama hicho kukipenda.

“Uchaguzi huu ni mwanzo kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa na uchaguzi Mkuu, anahitajika kijana atakayeweza purukushani za chaguzi zote hizo,” alisema.

Naye Mhandiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Muhidin Shangwe alisema kuaminiwa kwa vijana na kupewa nafasi mbalimbali za uongozi ni mojawapo ya sababu zinazowafanya wajitokeze kuwania nafasi hiyo.

“Kwa miaka ya hivi karibuni kumekuwa na tabia ya viongozi kuwasifu vijana mbele ya umma, pengine hili ni moja ya jambo linalowashawishi kuwania uongozi kwa kasi inapotokea nafasi,” alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live