Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ni mwendo wa kukata majina uchaguzi CCM

Chongolo New Ni mwendo wa kukata majina uchaguzi CCM

Fri, 15 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Chama cha Mapinduzi (CCM), kimetoa onyo kali ‘la kukata majina’ wale wote wanaoonekana kupanga safu za uongozi.

Onyo hilo limetolewa na Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo wakati dirisha la uchukuaji na urejeshaji fomu za kuwania uongozi ngazi ya wilaya, mikoa, mikutano ya Taifa likiendelea nchi nzima.

Tayari joto la chaguzi hizo limepamba moto, ambapo mpaka sasa waliojitokeza kuchukua fomu ni watoto wa vigogo, wabunge na mawaziri wa zamani pamoja na wenyeviti wa mikoa na wilaya wanaotetea nafasi hizo wakichuana vikali.

Mikoa ambayo inatarajiwa kuwa na mvutano mkali ni Shinyanga, Mbeya, Mwanza, Dodoma, Dar es Salaam, Arusha na Kilimanjaro ambako dalili zinaonyesha itakuwa ni vuta nikuvute.

Vita hiyo ya uongozi ni kuelekea uchaguzi mkuu ujao mwaka 2025, ambako tayari pilikapilika za kujipanga zimekwishaanza.

Jana, Chongolo akifungua kongamano la mafunzo ya uongozi kwa viongozi wa matawi wa Wilaya ya Dodoma mjini alisema kuna jambo kubwa linasikitisha la baadhi ya watu wenye ndoto ya nafasi nyingine kupanga safu na wapo bize kuhakikisha wanashinda.

Advertisement Alisema hadi mwaka 2025 ndio watakuwa na mawazo ya kufungua milango katika nafasi za ubunge, udiwani na urais, ila hawatasita kuwachukulia hatua wale wanaovunja utaratibu kuanza mipango kabla ya wakati.

“Tunawajua, tunawaona na mnayoyafanya tunayajua na mimi ni kijana, nitakuwa katibu mkuu muda mrefu, poleni mnaofikiria 2025 nitakuwa sina fursa au siyajui mliyokuwa mkiyafanya, ‘tuta-deal’ na wao kwa kiwango kinachowastahili,” alisema Chongolo.

Chongolo alisema atawalinda kwa nguvu zote wabunge na madiwani, hivyo mwenye nia ama kutamani wasubiri mwaka 2025.

“Mfano huyu (Anthony) Mavunde ndio Mbunge mpaka 2025, wewe uwe unamwona mfupi, mrefu ndio huyu, huyo huna nafasi ya kumchokoza wala kumwingilia, hiyo ni kwa ajili ya wabunge wote Tanzania na mimi ndio kazi yangu kuwalinda,” alisema Chongolo.

Kuhusu baadhi ya viongozi na makada wanaopanga safu, Chongolo alisema waache mara moja, kwani mambo hayo ndiyo yanayokigawa chama.

Aliwataka madiwani wawe na wivu na nafasi zao na wasiruhusu watu wenye nia ovu kuwaingilia katikati kabla ya muda wa kufanya hivyo.

Hata hivyo, alionya madiwani waache kupanga safu, wale wanaopanga kwa ajili ya kuwaangusha waache, kwani wanatengeneza mambo ya kuvuruga na kusababisha chama kisipate watu wenye uwezo.

Hata hivyo, Makamu Mwenyekiti wa CCM-Bara, Abdulrahman Kinana amewahi kunukuliwa akisema chama hicho kitasimamia haki kwenye uchaguzi huo wa ndani ili kuhakikisha wanaokubalika majina yao hayaondolewi.

Uchaguzi

Chongolo alitumia fursa hiyo kuagiza, “Naagiza vikao vitakavyojadili majina kwenye ngazi husika kutoona aibu au kuchukua hatua kwa waliokiuka maagizo, hatuwezi kuwa chama kinatoa maelekezo kwa ajili ya kutoa fursa kwa watu wote kuwa sawa katika uchaguzi, lakini baadhi wao wana pembe ndefu kuliko mmiliki wa ngombe husika,” alisema Chongolo.

Chongolo alisema yeye ndio mkurugenzi mkuu wa uchaguzi ndani ya CCM, hivyo atahakikisha anasimamia na kukemea kwa nguvu zote suala la rushwa na kuwaomba wafanye kampeni za kistaarabu bila chuki wala fitina.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka aligeuka mbogo kwa wanaCCM ambao wanawaingiza wakuu wa wilaya katika majungu, fitina na chuki kwa wagombea wa nafasi mbalimbali ndani ya chama.

“Msituingize kwenye majungu yenu, hakuna mkuu wa wilaya, mkoa mwenye mgombea,” alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live