Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ni mwanzo mpya au mwisho wa Kalist Lazaro kwenye siasa za Arusha?

85570 Mwanzomwishopic Ni mwanzo mpya au mwisho wa Kalist Lazaro kwenye siasa za Arusha?

Sat, 23 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ilikuwa ni vigumu kuzielezea siasa za upinzani katika Jiji la Arusha bila kutaja jina la Kalist Lazaro.

Lazaro, maarufu kwa jina la Bush katika jiji la Arusha, baada ya uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2004 alikuwa mwenyekiti pekee wa serikali ya kijiji kupitia Tanzania Labour Party (TLP) katika wilaya ya Arusha Mjini.

Umaarufu wake jijini Arusha ulianza kuonekana katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, akiwa kwenye timu ya kampeni za Godbless Lema kuwania ubunge kupitia TLP.

Ingawa hawakufanikiwa kushinda, walionyesha upinzani wa nguvu kwa mgombea wa CCM, Felix Mrema kwa kupata kura 47,000 dhidi ya 51,000.

Lazaro akiwa na Lema wakajiunga na Chadema na katika uchaguzi mkuu mwa mwaka 2010 nyota ya wanasiasa hawa iling’ara zaidi ambapo, Lema alifanikiwa kushinda ubunge.

Katika uchaguzi mkuu mwaka 2015, vilevile Lazaro aliongoza timu ya kampeni ya Lema na kufanikiwa kushinda ubunge na kuichukua halmashauri ya jiji la Arusha na yeye (Lazaro) akachaguliwa diwani wa Kata ya Sokoni One na hatimaye meya wa jiji.

Licha ya nafasi hizo, Lazaro alichaguliwa kuwa katibu wa Chadema mkoa wa Arusha na baadaye mjumbe wa kamati kuu, akiwakilisha wenyeviti wa halmashauri na majiji nchini.

Kujiuzulu, kujiunga na CCM

Novemba 19, Lazaro aliandika historia mpya ya kujiuzulu umeya na udiwani na kujiunga na CCM.

Lazaro ambaye mara kadhaa amekuwa akipongezwa na Rais John Magufuli kutokana na kushiriki katika shughuli za kiserikali bila kujali itikadi yake, anasema sababu za kujiuzulu ni migogoro ndani ya chama hicho, hasa kwa uamuzi wake wa kuunga mkono jitihada za serikali ya awamu ya tano na kushiriki katika shughuli mbalimbali za serikali.

Anasema pia ameamua kujiuzulu baada ya kupinga maamuzi ya Kamati kuu ya Chadema, kutangaza kujiondoa katika uchaguzi wa serikali za mitaa na hivyo kukosa viongozi muhimu ngazi za chini.

Lazaro alitangaza uamuzi huo akiwa ofisi ndogo za CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam, akiwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole.

Uamuzi wa kushangaza

Uamuzi huo umewaibua viongozi wa vyama vya siasa wakisema Lazaro umechangiwa na dhamira yake ya kutaka kuwa mbunge Arusha Mjini, lakaini akabaini ni vigumu jina lake kupenya ndani ya chama dhidi ya Lema.

Lema na Philemon Mollel, kamanda wa vijana wa CCM mkoa wa Arusha waliochuana katika uchaguzi uliopita wanatajwa chinichini kugombea tena nafasi hiyo mwakani.

Ingawa Lazaro anasema bado muda wa uchaguzi haujafika na akiwataka wana Chadema kutokuwa na hofu, anasisitiza kuwa yeye ndiye anajua sababu za kufikia uamuzi huo.

“Muda wa ubunge bado, wao wanawaza hivyo mimi sifikirii hivyo kwa sasa. Najua walikuwa na hofu na mimi na wamekuwa wakinipiga vita sana hadi kuniandikia barua mbili za kunipa onyo,” anasema.

Lakini Aman Golugwa, mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, anasema hawajashangazwa na uamuzi wa Lazaro kujiunga na CCM kwa kuwa alikuwa hajihusishi tena na shughuli nyingi za Chadema kwa muda mrefu.

“Lazaro licha ya kuwa meya, alikuwa mjumbe wa kamati kuu na aliwahi kuwa katibu wangu wa mkoa. Kwa muda mrefu mwenendo wake tulianza kuutilia shaka, hasa ushiriki mdogo katika vikao vya chama, hivyo tunamtakia heri huko alipokwenda, sasa amekuwa mpinzani wetu,” anasema Golugwa.

Anasema meya huyo alikuwa haudhurii hata vikao vya kamati kuu na alikuwa hatoi taarifa zozote, jambo ambalo lilikuwa linaonyesha hakuwa pamoja na viongozi wa kitaifa wa chama hicho.

Golugwa anasema Kalist ana malengo yake binafsi ambayo Chadema haiwezi kumzuia na hata kuondoka kwake kumechangiwa na mapendekezo wao (Kanda) kwa kamati kuu, kuomba achukuliwe hatua kutokana na kushindwa kutimiza wajibu wake.

“Kanda ya kaskazini tulimwandikia barua kadhaa, kumtaka kujieleza na tulipendekeza achukuliwe hatua na Kamati Kuu, sasa kuondoka ni jambo ambalo tulitarajia,” anasema.

Golugwa anasema kama lengo lake kujiuzulu ni kugombea ubunge, basi watapambana naye majukwaani kwani amekuwa mpinzani wao kisiasa.

“Atalipa gharama mwenyewe, watu walimpa dhamana kwa kumchagua kama diwani na chama tulimpa dhamana kubwa, ameamua kutundika jezi. Tunamsubiri kama akijiingiza katika harakati za ubunge mimi siwezi kumsema vibaya Lazaro,” anasema.

Diwani wa Kata ya Ngarenaro katika jiji la Arusha, Isaya Doita anasema wanajua moja ya dhamira za Kalist ni kuwa mbunge wa jimbo la Arusha lakini asifikiri itakuwa ni jambo rahisi kwake.

“Tunajua michakato ndani ya CCM na baadaye kupitisha, sisi tunamsubiri na kama uchaguzi ukiwa huru na haki hawezi kuwa mbunge wa jimbo la Arusha,” alisema

Doita akiwa mmoja wa madiwani wa muda mrefu wa Chadema, anasikitika kuona marafiki zake kadhaa kuhama chama, jambo ambalo anasema hajawahi kuliwaza.

“Meya yeye alihama muda mrefu kiroho kutokana na hali ya ilivyokuwa ndani ya chama lakini hakuna chama ambacho hakina msuguano, kikubwa ni kuheshimu kanuni na taratibu,” alisema.

Swahiba mkubwa wa Lazaro alikuwa Lema tangu uchaguzi mkuu wa mwaka 2009, naye ana neno juu ya Lazaro.

Anasema tangu mwaka 2016, meya huyo alikuwa ameondoka Chadema kutokana na kutoshiriki shughuli za chama hicho.

Lema kupitia ujumbe mfupi katika ukurasa wake wa twitter amesema “Wakati Yesu Kristo anateseka msalabani, Wayahudi walikuwa wanapiga kelele wakisema ‘amekwisha’, ‘amekwisha’. Lakini yeye alisema Imekwisha... Wanafikiri tumekwisha na kumbe imeisha. Ni baraka kubwa kwa Chadema Meya wa Arusha Mjini, Kalist Lazaro kwenda CCM. Bado rafiki yake mmoja.”

Kalist anavyokumbukwa Arusha

Katika jiji la Arusha, katika uongozi wa Kalist atakumbukwa na mambo kadhaa ikiwapo kuongeza makusanyo na mapato kutoka Sh10 bilioni mwaka 2014/15 hadi Ch20.7 bilioni mwaka 2018/19 na Jiji la Arusha kuendelea pata hati safi katika mahesabu yake.

Jeremiah Silayo, mkazi wa Arusha anasema katika kipindi cha uongozi wa Kalist, kwa kushirikiana na madiwani na watendaji wa jiji, wameondoa tatizo la upungufu wa majengo katika shule za sekondari na msingi lakini pia kuna miradi mikubwa inaendelea.

“Jiji la Arusha mwaka juzi lilishinda tuzo la majiji bora, kutokana na uwazi na uwajibikaji kwa watendaji lakini pia limeanza kujenga hospitali na vituo vya afya na kuondoa adha ya upatikanaji wa huduma,” anasema Silayo.

Naye mkazi wa Sokoni One, Jumanne Kilenga anasema wanampongeza Lazaro kwa kuondoka upinzani na kujiunga na CCM na wanajiandaa kumpokea ili kuendeleza kazi za maendeleo ambazo amekuwa akifanya.

“Amefanya uamuzi mzuri kurudi nyumbani kwani tunajua aliwahi kuwa CCM na huku sasa atafanya kazi vizuri kwa kushirikiana na serikali kuliko alipokuwa kwa wanaopinga kila jambo,” anasema.

Ni mwisho au mwanzo wake kisiasa?

Wakati kila upande ukivutia kwake, baadhi wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema huu unaweza kuwa mwisho wake kisiasa.

Ismail Seleman na Julius Munga, kwa nyakati tofauti wanaeleza kuwa kujiuzulu kwa meya kuna kuwa na athari mbaya na ukawa mwisho kwake wake wa kuvuma katika siasa za Arusha.

Seleman anasema ilikuwa ni dhahiri kuwa ipo siku Kalist angeondoka Chadema hasa kutokana na kutokuwa na mahusiano mazuri na viongozi wenzake.

“lilikuwa ni suala la muda tu, kama viongozi wenzake walikuwa hawamuungi mkono ni uamuzi sahihi kuondoka ila hatujui hatima yake,” anasema.

Munga kwa upande wake anaeleza kuwa, uamuzi wa Kalist unaweza kuwa mwanzo wake mpya wa kushika nyadhifa za juu za kisiasa ikiwepo ubunge Arusha.

“Ukweli upo wazi, Kalist asingeweza kuteuliwa kugombea ubunge Arusha mjini kupitia Chadema, lakini pia hata kama Lema asingegombea, kwa siasa za sasa Chadema kushinda CCM Arusha ni kazi ngumu,” anasema.

Pamoja na mjadala huo, swali linabaki palepale kuwa kujiuzulu umeya na kujiunga CCM ni mwanzo mpya wa kupaa kisiasa au mwisho wa umaarufu wa Kalist Lazaro? Tusubiri tuone.

Chanzo: mwananchi.co.tz