Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ni kweli hoja za Muungano zimepungua mwaka mmoja wa Samia?

SAMIA SULUHU12 Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania

Thu, 3 Mar 2022 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Katika mwaka wake mmoja madarakani, Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuhakikisha Muungano unaendelea kulindwa, kudumishwa, kuendelezwa na kuimarishwa huku hoja 11 kati ya 18 za Muungano zikitatuliwa.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dk Selemani Jafo alisema hayo jana Dodoma alipoelezea mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kipindi cha mwaka mmoja.

Dk Jafo alisema vimefanyika vikao kadhaa vya kujadili masuala ya Muungano katika ngazi mbalimbali ambavyo vilijadili kwa kina hoja 18, na hoja 11 kupatiwa ufumbuzi na kuondolewa kwenye orodha ya hoja za Muungano.

Alitaja hoja zilizopatiwa ufumbuzi na kuondolewa katika orodha ya hoja za Muungano ni ya uingizaji wa maziwa kutoka Zanzibar, usimamizi wa ukokotoaji na ukusanyaji wa kodi kwenye huduma za simu unaofanywa na Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRB) na Mkataba wa Mkopo wa fedha za ujenzi wa Barabara ya Chake chake hadi Wete-Pemba.

Alisema pia mkopo wa fedha za Mradi wa Ukarabati wa Hospitali ya Mnazi Mmoja, Mkataba wa mkopo wa fedha za ujenzi wa Bandari ya Mpigaduri, Uvuvi kwenye Ukanda wa Uchumi wa Bahari Kuu na uteuzi wa Mjumbe wa Bodi ya Bima ya Amana (DIB) kutoka Zanzibar.

Dk Jafo alizitaja hoja zingine kuwa ni ajira kwa watumishi wa Zanzibar katika taasisi za Muungano, Mgawanyo wa mapato yatokanayo na misaada kutoka nje ya nchi, Mapato yanayokusanywa na Uhamiaji kwa upande wa Zanzibar na uteuzi wa Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Rufani ya Kodi Tanzania (TRAT) kutoka Zanzibar.

Kuhusu miradi ya maendeleo inayotekelezwa pande mbili za Muungano, alisema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimeendelea kushirikiana katika miradi mbalimbali ya maendeleo.

Alizitaja miradi na programu hizo kuwa ni Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili uliozinduliwa Februari, 2020 ambako jumla ya Sh bilioni 112.9 zitatumika Zanzibar.

Mingine ni Mradi wa Kuongeza Tija na Uzalishaji wa Zao la Mpunga (ERPP); Mradi wa Udhibiti Uvuvi na Maendeleo Shirikishi Kusini Magharibi ya Bahari ya Hindi (SWIOFish); Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA); Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (EBARR), Mkakati wa Kudhibiti Sumu Kuvu Tanzania na Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha.

Dk Jafo alitaja mafanikio mengine kuwa ni usogezaji wa huduma za mawasiliano maeneo ambayo yana mawasiliano hafifu au hayana mawasiliano kabisa, ambako Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) na Kampuni ya Mawasiliano Zanzibar (Zantel) wameingia makubaliano Januari, 2022 ya kujenga minara ya simu 42 katika shehia 38 kwa lengo la kuboresha huduma ya mawasiliano Zanzibar.

Alisema pia Zanzibar ilipatiwa jumla ya Sh bilioni 230 zilizotokana na mkopo nafuu kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kukabiliana na athari za Covid-19, ambako fedha hizo zimeelekezwa kwenye huduma za kijamii zikiwemo afya, elimu, miundombinu na ujenzi wa masoko.

Chanzo: www.habarileo.co.tz