Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ni kipindi cha Bashiru kujijengea heshima CCM

71839 Bashiru+pic

Sat, 17 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kuna neno la Kiingereza lenye kutafsirika ndani ya maneno mawili ya Kiswahili; imani na heshima, credibility. Neno moja pekee halitoshi kubeba maana yake na kueleza mantiki yake.

Tafsiri nzuri zaidi ni hali ya kuaminika na kuheshimika. Umahiri wa mtu katika eneo fulani, humjengea kuaminika na kuheshimika. Credibility ni daraja la juu katika mafanikio. Kwamba mtu si tu anakuwa amefanikiwa, bali pia anaheshimika na kuaminika, hivyo maneno na matendo yake hayatiliwi shaka.

A blessing in disguise ni kifungu cha maneno ya Kiingereza, chenye maana ya jambo lenye kuonekana la shari, lakini linakuwa na heri kubwa ndani yake. Huhitaji utulivu, subira na matendo chanya ili kuziona faida husika ndani shari inayoonekana.

Maneno hayo; ‘credibility’ na ‘blessing in disguise’ na tafsri zake, ni mtaji muhimu kwa Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally, ndani ya chama hicho kwa kipindi cha sasa, kama atavaa utulivu na subira na akaiongozwa na matendo chanya.

Tangu makatibu wakuu wastaafu CCM, Abdulrahman Kinana na Yusuf Makamba watoe waraka, wakilalamika kuchafuliwa heshima zao na mtu anayejiita mwanaharakati, kisha mamlaka za chama (CCM) kukaa kimya, bila kuwatetea maneno mengi yameibuka.

Kumekuwa na wimbi la wana CCM, hasa wabunge, wakiwajia juu Makamba na Kinana. Hali hiyo imesababisha wengine watamke kuwa CCM inapitia kipindi kigumu.

Pia Soma

Yenye kusemwa yote na mapito ya CCM kwa sasa, jumlisha waraka ambao uliandikwa na Kinana na Makamba, ndio mtaji wa Bashiru kujitengenezea heshima na kuaminika kama Katibu Mkuu CCM, ikiwa atachukulia hali hiyo ndani ya chama chake ni heri kwake iliyopitia mlango wa shari.

Nyakati za mvurugano na mifarakano huwa nzuri kujenga heshima na kuaminika kwa anayevaa hadhi ya usuluhishi. Hivyo, Bashiru kwa nafasi yake, akiwa ndiye injini ya chama, ana kipindi bora mno kujenga heshima na imani yake kwa wanachama pamoja na Watanzania.

Bashiru ndiye mtendaji mkuu wa CCM, mwenyekiti wa benchi la ufundi la chama, yaani sekretarieti, vilevile ni mratibu mkuu wa vikao vyote na mshauri mkuu wa mwenyekiti CCM.

Kwa mantiki hiyo, Katibu Mkuu CCM ni kipenyo ndani ya duara la kila mafanikio na changamoto za chama. Hivyo, ana wajibu wa kuzikabili changamoto zote, vilevile kujitengeneza kuwa daraja la mafanikio ya chama. Maeneo hayo mawili ndiyo yatampa hadhi ya kuheshimika na kuaminika nyakati zote kwa wanachama na Watanzania.

Katikati ya upepo mkali wa kisiasa baada ya Makamba na Kinana kutoa waraka wao, Bashiru alionya na kuwataka wana CCM kujiweka mbali ili wasijadili alichokiita “upumbavu wa wapumbavu”. Alitishia kuwa watakaotetea upumbavu wa wapumbavu watafukuzwa uanachama.

Kwa vile Bashiru alirusha jiwe gizani, hakusema upumbavu ni nini na wapumbavu ni akina nani, watu wakajenga kiulizo; ni kwa nini upumbavu wa wapumbavu umetamkwa kipindi cha waraka wa Kinana na Makamba?

Vema kuishia hapo kwenye kiulizo, kwani si vizuri kumlisha maneno mdomoni ambayo hakuyatamka. Hata hivyo, kwa jinsi alivyoonya wana CCM wasijadili upumbavu wa wapumbavu, tumkumbushe kuwa Mwenyekiti wa kwanza wa Tanu na CCM, Mwalimu Julius Nyerere, alipata kusema, tatizo halitatuliwi kwa kujidanganya kuwa halipo.

Waraka wa Makamba na Kinana pamoja na mashambulizi ambayo wamepokea kutoka kwa wana CCM, ni kipimo kwamba ndani ya CCM kuna tatizo. Dawa yake ni kukubali kuwa tatizo lipo na kutumia njia bora za kulitatua.

Bashiru hashindwi kufanya vikao na Makamba pamoja na Kinana. Yeye ndiye mwenye nafasi ya kukituliza chama pale kinapopitia misuguano. Wazungumze kiutu uzima na kupata dira ya pamoja.

Makamba na Kinana ni watu wazima, walikalia kiti ambacho Bashiru amekalia leo. Hawawezi kuitwa na Bashiru wazungumze kiutu uzima halafu wamkaidi. Hata waraka wao ukiusoma katikati ya mstari, utaona namna wanavyoheshimu mamlaka za chama. Kilio chao ni kutelekezwa na viongozi wa chama, kipindi wakipewa uhusika mbaya na kuchonganishwa na Rais John Magufuli.

Bashiru atambue kuwa uhusika wake katika malalamiko ya Kinana na Makamba, utaamua namna ambavyo yeye atakuwa akitajwa baada ya kuondoka kwenye cheo hicho cha ukatibu mkuu CCM. Akitengeneza maridhiano, atakumbukwa na ataimbwa kwa mapambio, akiwa ukuta wa mwafaka, atakuwa simulizi mbaya.

Bashiru ajiulize; kesho akiwa si Katibu Mkuu CCM angependa watu wamkumbuke kwa lipi? Mpatanishi au mtazamaji wa mifarakano pasipo kufanya chochote? Historia ina tabia ya kuhukumu.

Kesho akiwa si Katibu Mkuu CCM, wanaweza kutokea watu wakamtupia mashambulizi. Naye atashangaa kuona mamlaka za chama hazimtetei wala kuingilia kati. Endapo atalalamika, atakumbushwa kuwa waumini wa Buddha hufundishwa kuhusu “Karma” kwamba uhusika wako leo, huakisi matokeo ya maisha yako kesho.

Rais wa kwanza wa Afrika Kusini, Nelson Mandela wakati anakaribia kuondoka madarakani, aliulizwa angependa akumbukwe kwa lipi katika uongozi wake, alijibu: “Ningependa nikumbukwe kama binadamu mwenye makosa mengi, lakini ninayejitahidi kutenda yaliyo sahihi.”

Ni ushauri kwa Bashiru kuwa akiwa Katibu Mkuu CCM, abebe hekima za Mandela. Ajione ni binadamu anayepaswa kujitahidi kutenda yaliyo sahihi. Kuketi na wastaafu Makamba na Kinana, atakuwa amefanya tendo la kujitahidi kama binadamu kutenda yaliyo sahihi. Na historia itamkumbuka.

Chanzo: mwananchi.co.tz