Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ni Waitara jukwaani, mitaani kwa wana Ukonga

15125 Pic+waitara TanzaniaWeb

Sun, 2 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ni majuma mawili kamili kabla ya uchaguzi mdogo jimbo la Ukonga unaotarajiwa kufanyika Jumapili ya Septemba 16, 2018.

Ni uchaguzi wa mvutano baina ya vyama kadhaa vya siasa, hasa kwa wagombea wa Chadema, Asia Msangi na Mwita Waitara wa CCM.

Wakati Waitara, mbunge aliyejiuzulu Chadema na kada mpya wa CCM amezindua kampeni zake katika kata yake ya Kivule jana, Msangi amekuwa na kampeni tangu Agosti 25.

Ukiacha umaarufu wa vyama husika, jina la Waitara ndilo limekuwa masikioni mwa wengi mitaani na katika mikutano ya kampeni katika jimbo hilo – haijalishi anatajwa kwa mema au mabaya.

Mwita Waitara alichaguliwa mbunge wa jimbo hilo katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kupitia Chadema. Kabla ya hapo alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa mtaa wa Kivule, mwaka 2014.

Lakini, Julai 28, 2018 alitangaza kujiuzulu nafasi ya ubunge na nyadhifa nyingine ndani ya Chadema na kujiunga na CCM ambayo imemsimamisha kuomba nafasi ileile aliyojiuzulu na katika jimbo lilelile. Pengine hatua yake hiyo ndiyo inavutia zaidi mjadala juu yake.

Wakati anajiuzulu nafasi hiyo alitoa sababu kadhaa, ikiwamo kutofautiana na viongozi wa ngazi ya juu wa Chadema baada ya kuhoji kuhusu matumizi ya ruzuku pamoja na demokrasia ndani ya chama, madai ambayo chama hicho kinayakana.

Si Waitara pekee, pamoja naye wapo wabunge wengine wawili wa Chadema wamekwishajiengua na kujiunga na CCM na wengine wawili wa CUF. Pia, wapo madiwani zaidi ya 150 waliochukua uamuzi kama huo.

Mkutano wa Chadema

Katika kampeni za Chadema katika jimbo hilo jina la Waitara linatamkwa kila mtu anapopanda jukwaani, atatajwa kwa jina au kutajwa kama ‘msaliti’.

Katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni hizo uliofanyika Agosti 25, 2018, jina lake lilitawala midomoni mwa viongozi wa Chadema waliokuwa wakimnadi Msangi.

Diwani wa Kata ya Kitunda, Nice Gisunte anaanza kwa kuwatia moyo akisema pamoja na mbunge huyo kuhama Chadema, wanachama wa chama hicho hawapaswi kurudi nyuma kwa kuwa ndiyo waliomchagua na ndiyo watakaomwangusha.

Lakini, diwani mwenzake wa Kata ya Tabata, Patrick Asenga anasema kufanyika uchaguzi huo ni kipimo kwa wananchi kama wana uwezo wa kufikiri.

Alisema hakuna kilichobadilika hapa nchini, bado maisha magumu, barabara mbovu mbunge ameamua kudanganya umma kuwa anaunga mkono jitihada za Serikali katika kuleta maendeleo.

Fedha za wananchi

Katika mkutano mwingine wa kampeni uliofanyika kwenye viwanja vya Italian vilivyopo Buyuni, Chanika, mkuu wa idara ya usalama na ukufunzi wa Chadema, Singo Kigaila anasema Waitara anachezea fedha za wananchi.

Anasema kitendo chake cha kuhama chama kwa tamaa za tumbo lake, kimesababisha kurudiwa kwa uchaguzi na kusababisha fedha zinazosadikiwa kufika Sh2 bilioni kutumika katika uchaguzi huo.

“(Miaka ya nyuma) Tulifanya uchaguzi katika majimbo kadhaa kwa sababu wana Chadema kama Chacha Wangwe walifariki dunia, lakini leo hii tuliyemhangaikia, tukalinda kura akatangazwa mshindi na kuingia bungeni ameuacha ubunge bila sababu, halafu anarudi tena. Hii si sawa,” anasema.

Anasema kumpigia kura na kumpa jimbo tena, ni sawa na kumpokea mtu wa dini, anakaa kwenye dini yake anaasi kisha anarudi kanisani au msikitini na anapokelewa.

Anawataka wananchi waachane na kazi ya kumchagua Waitara kila siku katika jimbo la Ukonga, kama aliuchoka ubunge akae pembeni aingie mwingine ambaye ni Asia Msangi.

Jina la Waitara halikuishia hapo, liliendelea kuibuka pia katika mkutano wa kampeni uliofanyika mwishoni mwa wiki katika Uwanja wa Gulukwalala, Gongo la Mboto ambapo Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani, Frederick Sumaye anaeleza kushangaa hatua ya Waitara.

“Hivi kweli hatuna akili kiasi hiki, mtu tulimpa kura hapahapa na amekana hadharani na bado tunampa tena,” anahoji Sumaye.

Sumaye anasema hakuna haja ya kumwendekeza mtu anayeendekeza tumbo na kusahau maisha ya wananchi.

Mbunge wa zamani wa jimbo hilo, Dk Makongoro Mahanga akiwa katika mkutano huo, anawataka wananchi wa jimbo la Ukonga kumfukuza Waitara kwa sababu mwaka 2015 aliwaomba kura za kuwatumikia kwa miaka mitano lakini hajafanya hivyo.

Anasema makosa kafanya mbunge, lakini wanaotukanwa ni wananchi kwa sababu wao ndiyo wapigakura.

“Mnaonekana mandondocha na yeye anawafanya mandondocha kwa kumpigia kura, msikubali cheo hicho, ninyi mna akili timamu fanyeni maamuzi kwenye sanduku la kura,” anasema Mahanga ambaye ni mwenyekiti Chadema Mkoa wa Dar es Salaam.

Mahanga ambaye pia alitoka CCM kwenda Chadema kabla ya uchaguzi 2015, anasema kinachofanyika sasa kwa chama hicho tawala ni kukusanya shahada za wapiga kura (vitambulisho vya kura) kwa wananchi kwa kutumia mabalozi ili kufanikisha wizi wa kura.

“Juzi nililisema hili kuwa tulikuwa tunatumia mabalozi kuiba kura na kununua shahada kwa wananchi, wenyewe wamekasirika wanatamani kupasuka.

“Nasisitiza huo ndiyo ukweli, wakija majumbani mwenu wafukuzeni na kingine cha kuwafanya mnakijua,” anasema Mahanga bila kufafanua.

Mwanasiasa huyo wanawabeza watani zao kuwa CCM kama chama kimekwisha imebaki ya polisi na ya Tume ya uchaguzi kwa sababu bila taasisi hizo hakuna kinachofanyika.

Vilevile diwani Kata ya Kipawa, Kenedy Simioni anasema Waitara amekosa fikra yakinifu na anawafanya mtaji wananchi wa Ukonga.

“Akiwa Chadema mmempa ubunge, anahamia CCM anataka mumpe tena,” anasema Simioni.

Pamoja na kauli za mikutanoni, Wiki iliyopita Chadema iliitisha mkutano na wanahabari na kumshutumu Waitara kuwa amehamasisha vurugu kupitia mtandao wa kijamii unaohusisha watu wa kabila lake la Wakurwa.

Kigaila katika mkutano huo, anasema chama hicho kimempeleka mgombea huyo kwenye kamati ya maadili.

Anasema kwa kutumia simu yake ya kiganjani aliandika kwamba Wakurya wa ukoo wa Wairegi wanoe mapanga yao na kumwaga damu katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi jimbo la Ukonga, madai ambayo Waitara ameyakana akisema ujumbe wake umepotoshwa.

Alifafanua kuwa hajawahi kufanya mkutano na kusema maneno hayo bali alituma ujumbe unaotajwa wakati akichangia mada kwenye kundi la WhatsApp liitwalo Mara Unity, ambako alisema kwa Kikurya kuwa “wanoe vitendea kazi kwa maana ya shahada za kupigia kura”.

Anasema mdai ya Chadema yanatokana na woga kwa sababu wanajua hawana namna wanavyoweza kumshinda kwenye jimbo la Ukonga.

Alisema wanajua amefanya vitu vingi kwenye jimbo la Ukonga ikiwa ni pamoja na kuwa na wananchi wenye shida na raha.

“Wao ndiyo wanaweweseka, ndiyo maana walikuja na suala la ukabila, wakaniunga kwenye hilo group linalohusu watu wanaoishi Mkoa wa Mara wakanitukana sana.

“Nimewaambia viongozi wangu wa CCM waachane na hayo mambo tuendelee kujipanga kwa ajili ya ushindi,” anasema Waitara.

Waitara alifafanua kuwa amepuuza taarifa hizo kwa sababu hakuna jopo la Wakurya waliotafsiri maneno hayo, hivyo hata aliyeyatafsiri alifanya hivyo kwa masilahi yake.

“Mwenye klipu (video) yenye hayo maneno wanayonituhumu ailete, najua wamepanga kunipeleka kwenye kamati ya maadili sipingani nao, ila waje na hiyo klipu,” anasema Waitara.

Chanzo: mwananchi.co.tz