Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nguvu ya Maalim Seif yaathiri CUF

49788 Pic+cuf

Mon, 1 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tanga. Tukio la aliyekuwa katibu mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Hamd kuhamia chama cha ACT-Wazalendo limeonyesha kuathiri mkutano wa hadhara uliohutubiwa na wabunge watatu wa CUF katika Uwanja wa Tangamano jijini Tanga.

Tofauti na ilivyozoeleka kuwa Tanga ni ngome ya CUF, mkutano wa juzi ulihudhuriwa na idadi ndogo ya wananchi jambo lililozua hofu kuhusu hatima ya chama hicho wilayani hapa.

Mkutano huo ulioongozwa na mbunge wa Jimbo la Tanga, Mussa Mbarouk akiambatana wabunge wa viti maalumu wa chama hicho mkoa wa Tanga; Nuru Awadh Bafadhili na Sonia Magogo ni wa kwanza tangu Maalim Seif kukihama chama hicho.

“Nilikuwa siamini kama Maalim Seif ana nguvu hapa Tanga lakini leo naanza kuamini... haiwezekani mkutano huu wa hadhara uliotangazwa na gari la matangazo lililopita mitaa yote lakini waliojitokeza ni kama hakuna watu,” alisema Jamila Haji wa barabara ya 12.

Wakizungumza katika mkutano huo wabunge hao waliwataka wakazi wa Tanga kuendelea na msimamo ndani ya CUF kama awali bila kuyumbishwa na wanasiasa wasiokuwa na msimamo.

Mbarouk alisema CUF bado iko imara jijini Tanga na kwamba wanaodhani imeyumba wasubiri mikakati inayowekwa ambayo itahakikisha ni chama kitakachokuwa kimbilio la wananchi.

Alisema kuhama chama kwa kumfuata mtu (Maalim Seif) ni kutojitambua.

Aliwalaumu mawaziri wanaofanya ziara za kukagua miradi ya maendeleo wilayani Tanga kwamba wanakwenda bila kumpa taarifa jambo ambalo anaona ni hujuma dhidi yake na kutaka aonekane kwa wananchi kwamba hafanyi kazi.

“Katika hili sitakubaliana nalo, nitakwenda kuwashtaki kwa Waziri Mkuu kwa sababu alishatoa waraka kwamba waziri yeyote anayekwenda kwenye jimbo lazima amtaarifu mbunge husika,” alisema Mbarouk.

Machi 18, Maalim Seif alitangaza rasmi kuhamia ACT-Wazalendo.

“Hatua tunayochukua leo ya kuhamia ACT-Wazalendo ni ya kihistoria. Umma haujawahi kushindwa duniani kote. Na umma wa Watanzania hautashindwa. ShushaTanga Pandisha Tanga Safari iendele,” alinukuliwa Maalim Seif.

Tangu kuhamia kwenye chama hicho kipya tayari amefanya ziara Unguja na Pemba ambako mamia ya waliokuwa wanachama wa CUF wamehamia ACT-Wazalendo.

Kutokana na wimbi hilo la kuhama baadhi ya ofisi za CUF ziligeuzwa za ACT-Wazalendo huku wengine wakituhumiwa kuchoma bendera za chama hicho.

Hata hivyo, Machi 28 zoezi la kupokea wanachama wapya wa ACT-Wazalendo lililokuwa lifanyike ukumbi wa PR Taifa lilizuiwa na polisi kwa maelezo kuwa walipata taarifa za kiintelijensia kuwa wafuasi wa CUF walikuwa wauvamie kuleta vurugu.



Chanzo: mwananchi.co.tz