Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ngome Wanawake ACT- Wazalendo wazindua sera ya jinsia

Gfdtfcfg Ngome Wanawake ACT- Wazalendo wazindua sera ya jinsia

Sat, 2 Mar 2024 Chanzo: Mwananchi

Ngome ya Wanawake ya chama cha ACT Wazalendo imezindua sera ya jinsia itakayoweka misingi imara kwa wanawake wa chama hicho kushiriki kwenye nafasi za uongozi.

Sera hiyo imezinduliwa leo katika ukumbi wa Hakainde Hichilema makamo makuu ya chama hicho Magomeni Dar es Salam.

Akizungumza baada ya uzinduzi wa sera hiyo leo, mgeni rasmi kwenye mkutano huo, Dk Ananilea Nkya amesema chama hicho kimeonesha mfano mkubwa.

Dk Ananile ambae pia ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania amesema chama cha ACT-Wazalendo kimetoka nje ya boksi kuleta mabadiliko kwenye vyama vya siasa.

Amesema kwa muda mrefu amekua akitamani kuona wanawake wengi wakishiriki kwenye nafasi za uongozi, akiamini watachochea mabadiliko kwenye jamii kwa sababu wanawake ndio wenye kuishi na jamii kwa muda mrefu zaidi kuliko wanaume.

Ameeleza kuwa muda umefika kwa wanawake wengi zaidi kutobaki nyuma badala yake wanapaswa kusonga mbele na kugombea nafasi nyingi zaidi, huku wakiweka mbele vipaumbele muhimu kwa sababu ya jamii zao.

“Taifa lolote haliwezi kuendelea iwapo watakua na utaratibu wa kuacha nyuma baadhi ya matabaka ya watu kwa sababu ya jinsia zao. Wanawake nyinyi wa ACT-Wazalendo na wengine wote hamupaswi kuachwa nyuma,” amesisitiza Dk Ananilea.

Sambamba na hilo amewataka wanawake wa chama hicho kuifanyia kazi ipasavyo sera hiyo ambayo imeweka mkakati maalumu kuwainua wanawake na sio kubaki kwenye maktaba.

Katika hatua nyingine amewataka wanawake wa chama hicho kuitumia sera kama sehemu ya mkakati kuwajenga viongozi wapya wanawake wengi zaidi ili waweze kushiriki kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na kushinda.

Awali Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Tanzania Bara, Doroth Semu amesema wameamua kuweka sera hiyo kwa lengo la kuleta usawa kwenye nafasi za uongozi ambao umekosekana kwa muda mrefu kwenye vyama vya siasa nchini.

Amesema wakati wanazindua sera hiyo wanawake wa chama chao, wanapaswa kufahamu kuwa wana wajibu wa kuandaa wanawake wengine zaidi katika maeneo yao kuongeza mtaji pia kutengeneza viongozi wapya ambao watagombea uchaguzi mkuu 2025.

“Kuzinduliwa kwa sera ya jinsia leo hii, ni wazi kuwa tayari sasa wanawake wa chama chetu mmepata nyenzo ya kufanyia kazi hivyo nendeni mkajijenge zaid,” amesema.

Amesema ndani ya sera hiyo ambayo imeweka wazi kwenye kila viongozi 15 wa chama basi nafasi sita miongoni mwa hizo zinapaswa kushikwa na wanawake.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kikosi kazi Ngome ya Wanawake ya chama hicho, Pavu Abdallah amesema hakuna sababu ya kuwakatisha tamaa wanawake wa chama hicho.

Amesema wanawake lazima wajitambue kuwa hakuna maendeleo yoyote ya siasa ambayo yanaweza kufanyika bila mchango mkubwa wa wanawake wenye wenyewe ambao ndio wanakua mstari wa mbele.

Sambamba na hilo amesema wanawake wengi ndio waathirika wa majanga mbali mbali yanapotokea hivyo wana wajibu wa kusimama mstari wa mbele kudai mabadiliko kupitia jukwaa la chama chao.

Mkutano huo mkuu wa Ngome ya wanawake utatoa fursa kwa wajumbe 68 kutoka mikoa 39 ya kichama Tanzania kuchagua viongozi wapya kwa nafasi ya mwenyekiti wa ngome hivyo.

Chanzo: Mwananchi