Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ngeze, wasomi watoboa siri ya mafuriko CCM

CCASMBARA Ngeze, wasomi watoboa siri ya mafuriko CCM

Sun, 20 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MGOMBEA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais John Magufuli ametajwa kuwa hotuba zake zinagusa watu mbalimbali.

Kwa upande wake, Mwanasiasa mkongwe nchini, Pius Ngeze amemtaja kuwa Magufuli ni kivutio cha wananchi kwenye mikutano kutokana na mambo makubwa, aliyoyatekeleza katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake.

Katika mahojiano maalumu na gazeti hili, Ngeze ambaye ni mwanasiasa mkongwe mwenye umri wa miaka 76, mkazi wa mjini Bukoba, alisema Rais Magufuli ni kivutio kwa wananchi, kwa sababu wameona yanayotendeka katika maeneo yao huku kukiwa hakuna sekta ambayo haijaguswa.

Ngeze ni mwandishi na mchapishaji wa vitabu anayemiliki Kampuni ya Tanzania Educational Publishers LTD (TEPU). Aliwahi kuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kagera kwa miaka 25, Mbunge wa Ngara kwa miaka mitano na Mjumbe wa NEC ya CCM kwa miaka 25.

“Wanamsikia na wanaona uwajibikaji katika huduma za jamii, hivyo wanakusanyika kwa wingi kuona huyu ni nani? Wanakuja kuonyesha bashasha mbele zake na hiyo ndiyo siri ya Magufuli kuwa na maelfu ya wananchi katika mikutano yake,” alisema Ngeze.

Alisema mwaka 2015, CCM ilikuwa imepoteza nuru na umaarufu, kiasi cha baadhi ya watu kuona aibu kuvaa sare za chama hicho. Lakini, tangu alipoingia Magufuli kimekuwa na wapenzi na wanachama wengi, ambao hawaoni aibu ya kuvaa kijani na njano.

Akianisha mambo mbalimbali yaliyotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli, Ngeze alisisitiza kuwa amefanya vitu vikubwa vya kushangaza dunia, ambavyo havikutegemewa.

“Mwaka 2015 alijitambulisha, akaomba wamuamini na wakampa kura na baadhi hawakumpa kwa sababu hawakumuamini. Lakini baada ya kupewa uongozi amefanya vitu vikubwa vya kushangaza dunia na walimwengu ambavyo hawakujua kama vitafanyika,” alisema Ngeze.

Alisema mbali na miradi ya kitaifa, ipo miradi katika maeneo ya watu kama vile kujenga vituo vya afya, zahanathi kila kata, hospitali za wilaya, elimu bure, miradi ya maji, barabara za mitaa, dawa na huduma nyingine zinazogusa binadamu.

“Hata ambao hawakuwa wanaguswa naye katika uchaguzi mkuu uliopita (2015) wanaguswa naye moja kwa moja katika uchaguzi huu,” alisema. Alipopongeza Ilani inayonadiwa sasa akisema imegusa vijiji vyote, miradi ya kitaifa na mwananchi mmoja mmoja wa kijijini na mjini.

“2015 lilitumika neno niamini nitafanya,nitaleta mabadiliko , mwaka 2020 linatumika neno nitaendelea kutekeleza, kwa sababu aliaminiwa na ametenda hivyo hakuna mashaka. Kila mmoja anajua atatekeleza na wanaojitoa fahamu wanajua kuwa anatekeleza,” alisema Ngeze. Alisisitiza kwamba vyama vingine vya siasa, vina jambo la kujifunza katika utendaji wa Magufuli.

Wengine wamtathimini JPM

Licha ya Ngeze, wananchi wengine wametathimini mwenendo wa kampeni za Rais Magufuli, wakimpongeza kwa hotuba za kistaarabu zinazogusa maisha ya watu; zinazofafanua mambo yaliyotekelezwa na uhusiano wake na maisha ya wananchi wa kawaida na zinazozungumzia matatizo yaliyo katika jamii kuanzia ngazi ya chini hadi juu.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Utalii ya Kiroyera Tours ya mjini Bukoba, Mary Kalikawe, akieleza alivyoguswa na kuvutiwa na hotuba za Magufuli, alisema ni kitendo cha kuelewa na kuonesha nia thabiti ya kutatua matatizo ya wananchi katika kila eneo nchini kuanzia kijiji hadi mkoa.

“Mfano alivyokuja Bukoba, alijua moja kwa moja kwamba tuna matatizo ya stendi, soko, mafuriko, akataja wilaya ambazo hazina hospitali, mahakama…Yaani ni mtu wa kushangaza na analeta hamasa, maana hakuna kitu kinatufurahisha sisi kama wananchi kuona kiongozi anajua matatizo yako yanayokuzunguka,” alisema Kalikawe.

Kiongozi wa Waendesha Pikipiki katika mtaa wa Katatolwans Kata ya Kashai, Boniface Edson, alisema hotuba zake zinavutia hata vijana, kwa sababu mengi waliyotamani yatekelezwe yamefanyika.

Edson alisema katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, alikuwa kiongozi mkuu wa misafara ya bodaboda mjini Bukoba, akishawishi wenzake wakichague chama cha upinzani, kwa sababu alitaka mabadiliko na utatuzi wa changamoto mbalimbali za vijana, ikiwemo kukamatwa hovyo kwa bodaboda, jambo ambalo sasa halipo.

Wasomi wazungumza

Wachambuzi wa siasa na wasomi waliozungumza na gazeti hili, wamepongeza kile walichosema ni kampeni za kistaarabu, zilizojaa sera na mambo ambayo Magufuli atawafanyia wananchi.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Mbunda alisema kwa tathmini yake, inaonesha wagombea wengi hawajajipanga huku ilani zao zikiwa zimeandaliwa kimkakati, hali inayowafanya waishie kuzungumzia upungufu kwenye mikutano, badala ya kueleza watakachowafanyia wananchi.

“Ukweli ni kwamba watanzania wa sasa ni waelewa sana wanajua kutofautisha sera na porojo …matokeo ndiyo yatakayoonesha nani alikuwa anamwaga sera na nani alikuwa anapiga porojo,” alisisitiza.

Mwanasiasa aliyewahi kuwa mbunge kwa upande wa upinzani, David Kafulila, alisema mgombea wa CCM yuko kwenye nafasi nzuri ya kujenga hoja kutokana na ukweli kuwa mambo mengi aliyoahidi mwaka 2015 ameyatekeleza.

Chanzo: habarileo.co.tz