Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ngeze: Vyama vingi vilikwamisha jengo la CCM Bukoba

28104 Pic+nzege TanzaniaWeb

Wed, 21 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Jengo la kitega uchumi cha CCM mjini Bukoba lililotelekezwa zaidi ya miaka 25 halikuota kama uyoga, lilikuwa ni wazo la viongozi wa chama kwa wakati huo na utekelezaji wake ulipata baraka za vikao vya ngazi husika.

Hii ndiyo ilikuwa ndoto ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kagera wakati huo, Pius Ngeze pamoja na Katibu wake Nicodemus Banduka. Kwa pamoja walijenga hoja kwenye vikao juu ya umuhimu wa kuwa na jengo la aina yake katika mkoa huu.

Msukumo wao ulichagizwa na wivu wa majengo ya kisasa ya chama waliyoyaona katika mikoa ya Kilimanjaro, Iringa, Mwanza na Dar es Salaam.

Lengo la kwanza ilikuwa ni CCM kuwa na jengo lenye ofisi zenye hadhi zitakazobeba idara zote za chama na sehemu ya kufanya biashara kwa kukaribisha shughuli za mabenki na taasisi mbalimbali.

Hata hivyo, mradi huo ulianza kukwama mwaka 1992 baada ya kuanza kwa mfumo wa vyama vingi na haikuwezekana kumega tena fedha ya mauzo ya mazao ya wakulima kwa ajili ya ujenzi wa jengo la chama kimojawapo cha siasa, CCM.

Ngeze anasema kigingi kilianza baada ya mfumo wa vyama vingi kuanza.

“Vyanzo vya mapato kwa ajili ya ujenzi ilikuwa ni michango ya hiari na kukata sehemu ya fedha kwenye mazao ya wakulima, baada ya kuanza kwa mfumo wa vyama vingi haikuwezekana tena na mradi ukalala,” anasema Ngeze.

Anasema mwaka 1997 aliondoka kwenye uongozi wa chama Mkoa wa Kagera baada ya kuwa mbunge wa Jimbo la Ngara na hata aliporejea tena kwenye nafasi ya mwenyekiti mwaka 2002 ndoto yake ilikuwa ni ileile ya kufufua kitega uchumi hicho bila mafanikio.

Miongoni mwa michango mingi ya aina mbalimbali iliyotolewa kwa ajili ya uendelezaji wa jengo hilo, Ngeze anakumbuka zaidi mchango wa Nazir Karamagi ambaye wakati huo pamoja na kuwa mbunge wa Bukoba Vijijini pia alikuwa Mjumbe wa Halmashauri kuu ya Taifa ya CCM.

Hata hivyo, anasema ndoto ya kuendeleza kitega uchumi hicho ilizingirwa na deni la Sh86 milioni alizokuwa anadai mkandarasi ambazo alizilipa Karamagi.

“Niliona hatuwezi kuanza tena ujenzi wakati tuna deni la milioni 86 tunazodaiwa, Karamagi alitulipia zote na jengo likawa huru. Siwezi kujua alivyozipata lakini alitusaidia,” anasema Ngeze.

Baada ya hatua hiyo kukamilika Ngeze akiwa na mwenyekiti wa chama, anasema walipata ari kubwa ya kuendeleza mradi huo ambapo nao walitakiwa kubadilisha ramani ya jengo baada ya chama kubadili muundo.

Anasema wazo la awali ilikuwa ni idara zote za chama kama ile ya siasa, fedha na nyingine kuwa na ofisi kwenye eneo moja la ghorofa na muundo mpya wa CCM uliondoa ulazima wa kupewa kipaumbele cha kuwa na ofisi.

“Wakati huo mwaka 2003 chama kilifanya mabadiliko ya kimuundo na sisi tukaomba ramani irekebishwe kwa kuwa muundo mpya ulikuwa unapunguza baadhi ya idara ilikuwa tuchukue ghorofa moja tu na maeneo mengine benki na taasisi,” anaema Ngeze

Ngeze anasema mikoa ya Kilimanjaro, Mwanza, Iringa na Dar es Salaam ilibahatika kuwa na majengo ya kisasa yenye ofisi za chama ikilinganishwa na Kagera kwa sababu ilianza ujenzi kabla ya wimbi la mfumo wa vyama vingi kutua hapa nchini, vinginevyo nao wangekwama kwa kuwa mfumo uliotumika ni uleule wa kumega fedha za mazao ya wakulima.

“Wakati huo chama kilikuwa kimeshika hatamu ilikuwa ni kuiagiza tu Serikali na vyama vya ushirika kutekeleza mara moja huku wewe ukisubiri kuletewa hundi ofisini,” anasema Ngeze.

Ngeze kama kamusi

Kwa maneno yake, Ngeze anasema, “Kwenye huu mradi mimi ndiye dictionary iliyobaki (mwenye maelezo yote). Natamani nishuhudie mradi huu unaanza kufanya kazi nikiwa bado hai. Ni jambo linalonisononesha kwa muda mrefu kila ninapopita na kuona lilivyotelekezwa,” anasema.

Kama jengo hilo lingekuwa umekamilika thamani yake ingekuwa mara dufu sasa hasa baada ya hivi karibuni Serikali kupandisha hadhi mapori matano ya akiba kuwa Hifadhi za Taifa.

Mwenyekiti huyo wa CCM mstaafu anasema ramani ya jengo hilo ilikuwa inakwenda sambamba na ujenzi wa hoteli ya kisasa kwenye kiwanja hicho. “Hili jengo limekaa muda mrefu, naona suala la hoteli ya kitalii haizungumzwi. Pale kuna eneo lililotengwa kwa ajili hiyo. Tulisema baada ya jengo ni hoteli pamoja na kusaidia uchumi wa chama pia wananchi wengi wangenufaika,” anasema Ngeze.

Anawataka viongozi wa chama kuweka msukumo mpya kwenye kitegauchumi hicho kwa kuwa hiyo ni mali ya chama inayotegemewa kuingiza kipato badala ya kuendelea kutelekezwa.

Maendeleo ya chama

Mbali na jengo hilo, Ngeze anasema chama hicho hakiwezi kuwa na msingi mzuri wa kujitegemea kama hakina mikakati ya kumiliki ardhi.

Anasema wakati wake alifanikisha ajenda hiyo katika Wilaya ya Karagwe aliyosema inaongoza kwa kuwa na vitega uchumi vingi baada ya kumiliki ardhi

1.Wananchi wakiingia na kutoka kwenye jengo la kitega uchumi cha CCM mjini Bukoba ambao haujakamilka kwa miaka zaidi ya 25 wakati wa maonyesho ya Saba Saba. Picha na Phinias Bashaya

2.Mwenyekiti mstaafu wa CCM Mkoa wa Kagera na Mbunge wa zamani wa Jimbo la Ngara Pius Ngeze



Chanzo: mwananchi.co.tz