Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nec kutumia Sh180 bilioni uchaguzi mkuu

102265 Pic+nec Nec kutumia Sh180 bilioni uchaguzi mkuu

Mon, 13 Apr 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeomba kuidhinishiwa Sh185.9 bilioni katika bajeti ya mwaka 2020/2021, huku Sh180 bilioni zikielekezwa kuendesha uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Hata hivyo, fedha hizo ni mbali na Sh144 bilioni ambazo NEC ilitengewa katika bajeti ya 2019/20 inayoishia Juni na hivyo kuifanya bajeti yake kwa uchaguzi kufikia zaidi ya Sh324 bilioni ikiwa ni tofauti na bajeti ya uchaguzi mkuu wa 2015 iliyokuwa Sh273 bilioni.

Fedha hizo (Sh180 bilioni) ni za uchaguzi mkuu, unaohusisha nafasi za Rais, wabunge, wawakilishi na madiwani ambao hufanyika wiki ya mwisho ya Oktoba ya mwaka wa tano tangu uchaguzi uliopita.

Maombi hayo ni kwa mujibu wa randama ya mpango wa bajeti ya NEC kwa mwaka 2020/2021 ambayo inakwenda sambamba na bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu iliyowasilishwa katika mkutano wa Bunge unaoendelea.

Tayari bajeti hiyo imepitishwa.

Katika bajeti ya ofisi hiyo, fungu la NEC ni namba 61 na jumla ya fedha zilizopo ni Sh312.8 bilioni

Pia Soma

Advertisement
Kwa mujibu wa randama hiyo, NEC imeomba fedha za matumizi ya kawaida Sh3.24 bilioni kwa ajili ya mishahara na Sh2.47blioni za matumizi mengine.

Shughuli zilizopangwa kutekelezwa kwa fedha hizo za uchaguzi ni kuimarisha mifumo ya habari, elimu na mawasiliano wakati wa uchaguzi.

Nyingine ni kuandaa mikutano mbalimbali ya wadau wa uchaguzi, kuendesha mafunzo kwa watendaji wa uchaguzi, kununua na kusafirisha vifaa vya uchaguzi na kuboresha mifumo ya usimamizi wa uchaguzi.

Shughuli nyingine ni kuratibu, kufuatilia na kufanya tathmini ya uchaguzi mkuu, kutoa elimu ya mpigakura, kufanya ukaguzi wa matumizi ya fedha za uchaguzi, kupitia na kufanya marekebisho ya sheria na kanuni za uchaguzi mkuu, kuandaa na kuwasilisha taarifa ya uchaguzi, kufanya vikao vya tume kwa mujibu wa sheria.

Shughuli nyingine ni kusimamia uendeshaji wa uchaguzi, kuratibu na kusimamia uangalizi wa uchaguzi mkuu ufuatiliaji na tathmini ya uchaguzi mkuu na kuandaa na kuwasilisha taarifa ya uchaguzi mkuu.

Aidha, NEC ilipokea Sh954.5 milioni nje ya ukomo wa bajeti kwa ajili ya uendeshaji wa uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Singida Mashariki na udiwani katika kata 13.

Aidha, katika kufanya maandalizi ya uchaguzi mkuu, Nec ilipokea Sh139.4 bilioni nje ya ukomo wa bajeti kwa ajili ya uboreshaji wa Daftari la Wapigakura na ununuzi wa magari kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu.

Randama hiyo inasema Sh118.07 bilioni zimetumika kwa ajili ya uboreshaji wa Daftari la Wapigakura na Sh4.37 bilioni kwa ununuzi wa magari ya uchaguzi mkuu.

Katika mwaka wa fedha 2019/20 NEC iliidhinishiwa kukusanya maduhuli ya Sh20 milioni kutoka vyanzo vyake ambavyo ni uuzaji wa nyaraka za zabuni na dhamana za wagombea ambao hawakufikisha asilimia 10 ya kura zote halali zilizohesabiwa au kama alijiondoa kuwa mgombea baada ya siku ya uteuzi.

Hadi kufikia Februari 2020, NEC haikukusanya kiasi chochote cha maduhuli na katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Singida Mashariki na udiwani katika kata 13 Tanzania Bara, wagombea wote walipita bila kupingwa na hivyo hakukuwa na makusanyo ya dhamana.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mohamed Mchengerwa alisema Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zimeombewa Sh219.47 bilioni kwa ajili ya mpango wa maendeleo.

Alisema Sh194.36 bilioni ni za ndani na Sh25.1 bilioni ni fedha za nje.

“Uchambuzi wa kamati umebaini kuwa bajeti ya maendeleo imeongezeka kwa Sh162.73 bilioni.Ongezeko hilo ni sawa na asilimia 297.3 ya bajeti ya maendeleo iliyoidhinishwa na Bunge kwa mwaka wa fedha 2019/2020,” alisema.

Alisema mabadiliko hayo katika bajeti ya maendeleo pamoja na sababu nyingine muhimu, yanatokana na kuongezeka kwa bajeti ya fungu la NEC kwa ajili ya kuiwezesha menejimenti ya uchaguzi itekeleze majukumu yake yanayoikabili mwaka huu kwa ufanisi mkubwa zaidi.

Chanzo: mwananchi.co.tz