Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ndugai agoma kufukuza wabunge 19

51e6c35f6b96c540285b8c2c357d02e7.jpeg Ndugai agoma kufukuza wabunge 19

Tue, 4 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai amesema atawalinda wabunge 19 wa Viti Maalumu kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) hivyo waendelee kuchapa kazi.

Pia amemkumbusha Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye (CCM) kuwa hana uhuru wa kuzungumzia wabunge wenzake vibaya katika mitandao ya kijamii. Ndugai aliyasema hayo jana bungeni jijini Dodoma.

“Niwaambie vyama vya siasa jamani mimi ni spika mzoefu nimekuwa hapa bungeni miaka 20 sasa naelekea ishirini na tano nina uzoefu wa kutosha wapo watu wanaopiga kelele Ndugai anavunja Katiba yaani hawaelewi watendalo kabisa,” alisema Spika Ndugai.

Alisema ni vyema makatibu wa vyama vya siasa wanaomuandikia jambo la migogoro wamuandikie barua rasmi badala ya vipeperushi.

“Katibu Mkuu wa chama chochote kile akiniandikia jambo lenye mgogoro ambao unapelekea mambo ya kikatiba, mgogoro unaotoka kwako msiniandikie kipeperushi, unasema Spika chukua hatua fukuza fulani na fulani,” alisema.

Aliongeza, “Kazi yangu mojawapo ni kulinda wabunge, mkiruhusu hayo mtapata tabu waheshimiwa. Katibu Mkuu wa chama chochote huko ulikotoka anaandika tu barua kipeperushi halafu mimi naenda kufukuza haiendi hivyo.”

Aliwataka viongozi hao waandike barua na kuambatanisha na katiba ya chama husika kwa sababu hawezi kujua Katiba ya kila chama.

“Aniambatanishie na muhtasari wa kikao kilichofanya maamuzi maana inawezekana huyo Katibu Mkuu kaamka tu kaandika halafu na mimi nakurupuka nachukua hatua nitakuwa ni Spika au kitu cha ajabu,” alisema Soika Ndugai.

“Naangalia je hawa wabunge waliofukuzwa walipata nafasi ya kuhojiwa, kujieleza, walipata natural justice, walisikilizwa? Nifukuze watu ambao hawakusikilizwa popote ndio mnataka hivyo... Mheshimiwa Nape mambo haya mazito.”

Alisema kuna vyama vimejaa udikteta na na mfumo dume, na kwamba, suala la wanawake 19 kufukuzwa kwa mpigo lazima litazamwe.

Spika alisema wabunge hao wamekata rufaa kutokana na kuwa ndani ya Katiba ya Chadema kuna chombo ambacho ni Baraza Kuu ndicho chenye uamuzi wa juu.

“Kwa hiyo waheshimiwa (wabunge wa Chadema) endeleeni kuchapa kazi, msiwe na wasiwasi…mpo mikono salama. haijapangwa kuwa lazima spika achukue hatua siku mbili au nne, bali busara yake anakwenda taratibu anajiridhisha taratibu sasa kwa nini watu wananiingilia lakini,” alifafanua.

Kuhusu Nape, alisema, “Lakini majuzi imetokea maneno kidogo…mdogo wangu Nape yakamtoka maneno na yamezunguka sana kwa sababu ni mbunge, ikifika mahali mbunge anasikika mnaanza kupishana haipendezi eeh..”

Aliongeza, “Kwa hiyo sitapinga hoja zake kwa sababu ana uhuru after all kitu kimoja hana uhuru kwa sababu ya kanuni ni kuwasema vibaya wabunge wenzake, nafikiri hilo kanuni linakataza hivyo hilo lazima nilikemee.”

Ndugai aliwasihi wabunge 19 wa Chadema kumsamehe Nape pamoja na kuwa wamewakosea sana kwa kuwaita wabunge hao majina ya mitaani.

“Aliwataja kwa majina ya mitaani ambayo kwa kweli, kwa kweli, kwa kweli alikosea sana na niliongea naye na alikiri kuwa naamini aliteleza hivyo sitamsimamisha hapa aseme chochote.

“Ninachokuombeni waheshimiwa (wabunge wa Chadema) mumsamehe bure. Mtu akikufanyia kosa kubwa sana unachoweza kufanya ni kumsaheme aliwakosea sana…aliwakosea sana... aliwakosea sana,” alisema.

“Nape mdogo angu unapo-deal na wanawake duniani pote unaongea nao kwa heshima na ndio practice ya dunia na wale wote wasioelewa hivyo ndivyo ilivyo. Wanawake ni mama zetu, dada zetu ni mabinti zetu, tunawazaa, tunawapenda, hii hata katika mila zetu, hata nyie wenyewe mtanikubalia.”

Chanzo: www.habarileo.co.tz