SPIKA wa Bunge, Job Ndugai amesema, wabunge wana majonzi kwa sababu wamefiwa na mwenzao, wamezidiwa, na wamechanganyikiwa na wanamshujuru Mungu kwa maisha ya rais wa Awamu ya Tano, Hayati John Magufuli.
Ndugai alisema jana katika viwanja vya Bunge kuwa, walikuwa na Magufuli tangu mwaka 1995 Magufuli akiwa mbunge, naibu waziri, waziri na hatimaye Rais wa Tanzania hivyo ni mwenzao na sehemu ya Jumuiya ya Bunge.
“Katika historia ya maisha yake kwa miaka 26, amepita kwenye lango lile la Msekwa au lango hili hapa alipolala mbele hapa,” alisema muda mfupi kabla ya wabunge kuuaga mwili wa Rais Magufuli.
“John rafiki yangu, John ndugu yangu, kiongozi wangu, mtani wangu, kalale salama John. Wabunge tutakuenzi kwa kuchapa kazi zaidi. Mama Janeth Magufuli na familia poleni, tusisahau kumtanguliza Mungu mbele kama alivyotufundisha siku zote,” alisema Ndugai.
Alisema, Rais Magufuli alikuwa mtani wake na kuna siku alimuuliza siku akiaga dunia (Ndugai) atazikwa wapina akamjibu Kongwa, na pia kiongozi huyo akamuuliza na yeye (Magufuli) akifa atazikwa wapi.
“Nikamwambia wewe ukifa tutakuzika Ugogoni kwa sababu umetupa heshima kubwa sana kufanya makao makuu Dodoma, kwa hiyo tutakuzika kwenye nchi yako ya Dodoma.”
“Pili, mimi nina sheria hapa mkononi ya mazishi ya viongozi kwa hiyo wewe bwana Dodoma hutoki, na mimi na wabunge tutahakikisha tunakuzika Dodoma,” alisema Ndugai.
Alisema Rais Magufuli hakutaka kuzikwa Dodoma, alitaka azikwe Chato na alihakikisha hilo linatekelezwa, hivyo anaishukuru serikali kwa kutekeleza alichokitaka kiongozi huyo.
Ndugai alisema, Rais Magufuli alikuwa mtu mwema aliyepanda mbegu kwenye udongo mzuri, kajenga barabara za lami kila kona, madaraja, masoko, meli, viwanja vya ndege, Bwawa la Mwalimu Nyerere, viwanda, shule, vyuo, vituo vya afya, hospitali za rufaa.
“Hiyo ilikuwa ni mbegu uliyokuwa ukipanda. Naamini mbegu hiyo imeanguka kwenye udongo mzuri, sisi Watanzania tutaendelea kuikuza mbegu hiyo na kuhakikisha inamea na kuzaa matunda zaidi na zaidi,” alisema.
Ndugai alisema, mbegu nyingine aliyopanda Magufuli ni uwajibikaji katika serikali, utii katika nchi, uchapakazi, uzalendo katika nchi, ubunifu, matumizi mazuri ya fedha za serikali, na kuchukua hatua kwa wasiotekeleza wajibu wao.
“Wabunge wenzangu tumeondokewa na kiongozi, tazama Watanzania wanavyolia kila mahali Rafiki yetu JPM umeweza kuhamisha makao makuuu kutoka Dar es Salaam kuja Dodoma, naamini hili litaendelezwa na serikali inayofuata na ni jambo kubwa sana ulilolifanya, lilishindikana miaka yote, likawezekana wakati wako,” alisema.
Ndugai alisema wabunge wanamshukuru Mungu kwa maisha ya Magufuli ambaye siku zote aliishi kwa kumtanguliza Mungu na pia, alimshukuru kwa kumpa fursa ya kufanya nae kazi.
“Kwa miaka 20 ambayo nimekuwa hapa bungeni nimefanya nae kazi kwa karibu kama rafiki yangu, kama ndugu yangu, nilimfahamu vizuri kama kiongozi wangu. Lakini safari leo imetimia na mwendo ameumaliza. Rafiki yangu John leo umelala hapa mbele yetu”.
Alisema, Rais Magufuli alikuwa akimueleza kuhusu Tanzania anayoitaka na wabunge walikuwa na wajibu wa kumuunga mkono kwa kutunga sheria na kupitisha bajeti ya kuwezesha ndoto hizo kutimia, kutoa ushauri kwa serikali na mara zote walimuunga mkono.
“Waheshimiwa wabunge tumetenga tarehe 30 siku tutakayoanza Bunge hapa tutakuwa na program maalumu ambayo tutafanya shughuli hiyo ndani ya ukumbi wa Bunge ambako tutakuwa na azimio maalumu,” alisema Ndugai.
Alimuomba Mungu ampe afya njema Rais Samia Suluhu Hassan awe hodari, mwenye subira, awe mstahimilivu, na mwenye hekima.
“Na sisi wabunge tunaahidi kusimama na Mama Samia, liwe jua, iwe mvua,” alisema Ndugai.