Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ndio kwanza kumekucha! Kina mbatia watangaza kongamano Dar

Mbatiaapoiic Data Ndio kwanza kumekucha! Kina mbatia watangaza kongamano Dar

Fri, 15 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baada ya mtifuano wa pande mbili za chama cha NCCR-Mageuzi ikiwemo ile inayomuunga mkono James Mbatia na inayompinga, hatimaye upande wa mwanasiasa huyo umeahidi kuanza kufanya shughuli za siasa za chama hicho.

 Wamesema hatua hiyo ni baada ya ukimya wa muda na kwamba wamefikia uamuzi huo, kutokana na kuthibitisha kikao kilichoisimamisha sekretarieti ya chama hicho akiwemo Mbatia, hakikuwa halali.

Upande wa Mbatia unakuja na uamuzi huo ikiwa ni miezi miwili imepita tangu, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, iridhie uamuzi wa halmashauri kuu ya NCCR-Mageuzi kuisimamisha sekretarieti hiyo.

“Uamuzi wa Kikao cha Halmashauri ya chama hicho kilichofanyika Mei 21 mwaka huu, ulikuwa halali kwa akidi ya wajumbe wake. Kwa mamlaka ya ofisi hii, tunamtaka Mbatia kutojihusisha na siasa ndani ya chama hicho hadi uamuzi huo utakapotenguliwa na chama,” alisema Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa nchini, Sisty Nyahoza.

Licha ya kusimamishwa, leo Alhamisi Julai 14, 2022 Mkuu wa Idara ya Uenezi na Mahusiano kwa Umma, Edward Simbeye ambaye ni miongoni mwa waliosimamishwa, amesema wanatarajia kufanya kongamano Julai 23, 2022 jijini Dar es Salaam.

Amesema kongamano hilo litafuatiwa na ziara ya uongozi wa chama hicho katika Mikoa 15 ya Tanzania bara, itakayoongozwa na Mbatia.

Advertisement “Tumerudi kufanya majukumu yetu ya chama ya kila siku na tumeanza vikao na Mkoa wa Dar es Salaam na hivi karibuni kufikia jumatatu tutatangaza ziara za mikoa 15 nchi nzima na itaongozwa na Mwenyekiti wetu James Mbatia,” amesema.

“Waswahili wanasema ukiona ukimya mwingi ujue una kishindo,” ni maneno aliyoyasema Simbeye kusisitiza shughuli hizo wanazotarajia kuzifanya.

Hata hivyo, Simbeye ameeleza kuhusu uamuzi wa kusimamishwa kwao, akisisitiza haukuwa halali kutokana na kikao hicho kutokidhi akidi.

Ni watu 34 pekee ndiyo waliohudhuria kikao hicho kihalali na kati yao tisa walidanganywa kwamba kikao hicho kilikuwa ni semina ya msajili wa vyama vya siasa.

Simbeye ameithibitisha kauli yake hiyo kwa kuonyesha viapo vya wajumbe 56 wa halmashauri kuu, wakieleza kuwa hawakuwa wameshiriki kikao hicho.

“Halmashauri yetu ina wajumbe 81, wajumbe 56 wamesaini viapo kwamba hawakushiriki kikao hicho huku walioshiriki na kufanya maamuzi ni watu 25 ambao hawana akidi ya kufanya maamuzi yoyote,” amesema.

Amesema hatua ya kusaini viapo hivyo nchi nzima inalenga kuudhihirishia umma kwamba kilichofanyika katika kikao cha kuwaondoa ni utoto.

Alipotafutwa Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi kueleza iwapo wanasiasa hao wana uhalali wa kufanya shughuli za kisiasa, ameeleza anachokifahamu ni kwamba walimwandikia Waziri (Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, George Simbachawene) kuhusu mgogoro wao.

“Jambo lao bado halijashughulikiwa maana walimwandikia Waziri, kwa hiyo litakapoletwa kwetu ndiyo tutashughulikia. Lakini sisi hatukuwasimamisha walisimamishwa na wenzao (halmashauri kuu),” amesema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live