Jina la Basil Lema si geni masikioni. Katibu wa Chadema mkoani Kilimanjaro tangu mwaka 2009, akiwa ameshika nafasi hiyo kwa vipindi vitatu mfululizo, akifanya kazi na aliyekuwa mwenyekiti wa mkoa na mbunge, Phillemon Ndesamburo (marehemu).
Lema ambaye amekuwa akijinasibu kama mwalimu wa chama na mtengenezaji wa mikakati, ni miongoni mwa makada wa chama hicho wanaotajwa kurusha karata yao ya ubunge katika jimbo la Moshi Mjini baada ya Japhary Michael ambaye ametangaza kutogombea tena.
Habari hizi zinaibua picha ya mwaka 2015 pale alipoingia kwenye kinyang’anyiro cha ubunge katika jimbo hilo akichuana na Japhary na Elikunda Kipoko, baadaye alijitoa kabla ya kura za maoni.
Akizungumzia katika mahojiano na Mwananchi, Lema anasema wakati huo aliingia kwenye mchakato wa ubunge baada ya kuona anakidhi vigezo lakini akajitoa kwa ushauri wa Ndesamburo, kuwa ampishe Japhary Michael aliyekuwa meya kwa wakati huo.
“(Ndesamburo) Aliniambia ingekuwa bora nimpishe aliyekuwa meya kwa wakati huo, agombee ubunge na baada ya yeye, kwa kuwa umri wangu ni mzuri ningegombea mbele ya safari,” anasema.
“Binafsi, nilikuwa ninaona nakidhi vigezo, lakini alinishauri sana nimuachie Japhary. Na alinipa sababu tatu, kwamba ninayo nafasi baadaye, tunaingia kwenye kampeni nzito za uchaguzi ambazo tunahitaji kushinda majimbo mengi ya uchaguzi, na kama Mkoa wa Kilimanjaro, ofisi ya mkoa tulikuwa mimi na yeye (Ndesamburo) kwa wakati ule.”
Sababu ya tatu, ni kwamba Ndesamburo alikuwa tayari amemwandaa Japhary, hoja ambayo Lema aliona hakuna heshima kama kiongozi kuandaa mtu wa kumrithi.
Hivyo, Ndesamburo alimtaka Lema arudi wakaongeze nguvu ili kusaidia wengine wapate ubunge na kukiwezesha chama kupata majimbo mengi.
Je, ndoto ya ubunge bado ingalipo? Lema anasema kwa sasa ndoto yake si ya kuwa mbunge yeye peke yake, bali kufanya watu wengi zaidi kuwa wabunge, ikiwa ni pamoja na kuwaandaa vijana wengi zaidi kuingia Chadema.
“...wajiandae na waandaliwe vizuri jinsi ya kuwa wabunge, na nikibahatika kuwaandaa vijana takribani 50, nitafurahi sana kwani hainisaidii sana kwa umri huu nilio nao, kukimbilia bungeni nikakae huko mtu mmoja kama ulimi mdomoni.
“Nahitaji kuwa na vijana wengi, waende na damu inayochemka Bungeni wakafanye mabadiliko makubwa kwa nchi yao. Tamaa ile na shauku ya ubunge niliyokuwa nayo mwaka 2015 kwa sasa imepoa sana, kwa sababu ya kuiangalia nchi inakokwenda. Inahitaji damu mpya, vyama vyetu vya siasa vinahitaji damu mpya, na tunakwenda kwenye siasa zinazohitaji fikra tofauti sana, si hizi za kwetu tena.”
Je, madai kuwa atagombea ubunge 2020 Moshi Mjini yana ukweli kiasi gani? Lema hakutaka kuweka wazi hilo, anasema ni sahihi na zikisemwa vizuri ni tamu na kwamba Moshi kuna mbunge na hajatoa taarifa rasmi kuwa hagombei.
“Hizo habari zimesemwa sana, na sizichukii kwa sababu ni dhambi mimi kuwa mbunge, hapana. Ninazichukia kwa sababu hazijakaa kwa maridhiano, zimekaa kimgogoro na hicho kwangu kama kiongozi naona hapana. Ningeupata ubunge ili watu wa Moshi wawe wamoja, ili Tanzania iwe moja, hiyo ni shangwe kwangu”
“Lakini, kuupata ubunge halafu watu hawako pamoja, inanisaidia nini? Lakini la pili ni kwamba Moshi ina mbunge na hajaniambia rasmi kwamba hagombei ubunge na kama asipogombea tutatangaza uchaguzi na wale wanaoutaka watachukua fomu na atakayeshinda katika kura za maoni atagombea ubunge lakini kwa sasa hivi na kwa mujibu wa katiba ya Chadema, mbunge aliyeko madarakani anabaki kuwa mbunge na kwa kila gharama na tunamlinda.”
Kwa nafasi yake ya ukatibu wa mkoa, Lema anaona kuna mafanikio makubwa. Kubwa ni kunyakua majimbo sita na halmashauri tano kutoka mikononi mwa CCM mwaka 2015.
“Mara ya kwanza nilipogombea ukatibu wa mkoa mwaka 2009, tulikuwa na jimbo moja la Moshi Mjini na hatukuwa na halmashauri hata moja, wala orodha ya wanachama. Nikawaahidi wanachama kuwa nitahakikisha Chadema kimekuwa maarufu katika mkoa mzima wa Kilimanjaro,” anasema.
Anasema alianza vita ya kisiasa na katika uchaguzi mkuu mwaka 2010, chama hicho kilifanikiwa kuchukua majimbo mawili zaidi ya Rombo na Hai, kikaendelea kuishikilia Moshi Mjini na pia kikapata halmashauri mbili za Manispaa ya Moshi na Hai.
“Mwaka 2014 nilipogombea tena ukatibu kwa mara ya Pili, nikawaambia sasa ninautaka mkoa mzima, tukaweka mikakati na tuliongeza nguvu maeneo ya upareni na mwaka 2015 tukapata jimbo la Same Mashariki, Rombo, Moshi Vijijini, Moshi Mjini, Hai, Siha na Vunjo kupitia NCCR- Mageuzi tukishirikiana kama Ukawa, hivyo jumla tukapata majimbo saba kati ya tisa ya mkoa Kilimanjaro, CCM ikabaki na majimbo mawili – Mwanga na Same Magharibi ambayo hata hivyo ilishinda kwa kiwango kidogo,” anaongeza.
Kwa upande wa halmashauri CCM ilisalia na mbili na Chadema ikachukua tano.
“Pamoja na figisufigisu zote zinazofanyika, CCM wajue tumejipanga zaidi kimkakati na sasa tunakwenda kuchukua majimbo yote tisa na halmashauri zote saba; Si Kilimanjaro pekee, bali tunakwenda na mikoa mingine ya jirani,” anatamba Lema.
Akizungumzia changamoto, Lema anasema siasa inakuwa ni mapambano wakati manufaa yakiwa machache au hakuna.
“Wakati manufaa ya kisiasa ni machache au hakuna, kuna umoja na mshikamano mkubwa sana, lakini fursa zinapoongezeka inakuwa kazi ngumu mno kuwaweka watu pamoja, migogoro inazaliwa kwa sababu ya fursa.
“Nimekutana na kazi ngumu kuwaweka watu pamoja, pale wanapoingia kila mmoja anapambana kupata maslahi. Tatizo tulilonalo kwenye vyama vya siasa, si tu Chadema, tumewapunja elimu watendaji wetu wa siasa.”
Anasema wanawapeleka watu kuingia bungeni, huku wakiwa hawajui hata ladha ya historia ya chama kilichompitisha, hivyo ipo haja ya wagombea kupitishwa kwenye mafunzo kupata elimu na mwanga kabla ya kuchukua fomu na kugombea nafasi mbalimbali.
“Wagombea wapitishwe darasani ili wafahamu wakipata hizo nafasi, wanapaswa kufanya nini, kwani tukiwaacha waende kila mmoja anakuja na wito wake na hawajui Chadema au chama kingine kilichompitisha kilitaka kufanya nini”
“Na hii ndiyo maana wabunge wa CCM, wana hoja zao, dhidi ya wabunge wa upinzani na wale wa upinzani wana hoja zao dhidi ya wabunge wa CCM, kwa hiyo vita ni dhidi ya wabunge kwa wabunge, na si vita dhidi ya matatizo ya wananchi.
“Hiki ndicho kilio changu. Ninaumia sana na migogoro ndani ya vyama vya siasa, kwa sababu ninafikiria ni lini nitafanikiwa kuwaweka darasani wagombea na watendaji wa chama changu, kwa kuwa chama hiki ni lazima nikijenge kwa kuwa kinakwenda kuchukua nchi,” anasisitiza.
Kila mwanasiasa ana alama yake ya mafanikio katika siasa, Lema, alama hiyo Freeman Mbowe, mwenyekiti wa Chadema. Anasema anavutiwa naye kutokana na uvumilivu wake, kipimo ambacho anasema watu hawataki kukikubali kwenye siasa.
“Watu wengi wanafikiri siasa ni namna unavyojitangaza na kutangazwa, lakini siasa ni vile unavyovumilia, kusimamia na kung’ang’ania msingi wa dira yako. Ije mvua, liwake jua, bado unang’ang’ania hata pale ambapo wale unaowatetea hawaelewi, bado unang’ang’ania kwa sababu ya wito ulioko ndani yako.”
Akiwaangalia wapambanaji wa Afrika na duniani, Lema anamuona Mbowe ni tofauti kwa kuwa wapo ambao kazi walizofanya ni za kutukuzwa kama kina Nelson Mandela, lakini wakati wanapambana wao, jamii nzima ilikuwa nyuma yao ikiwashangilia, na hasara waliyoipata ilikuwa ya muda wao tu.
“Lakini, Freeman Mbowe amepata hasara ya muda wake, fedha zake, mali zake, maisha yake ya baadaye na amepata pia hasara ya usalama wake, lakini bado ana-move (anasonga). Ninamuona ni mwanasiasa wa kipekee katika zama hizi,” anasema.
Anasema mwanasiasa mwingine wa mfano kwake, ni marehemu Ndesamburo kutokana na kipaji kikubwa alichokuwa nacho cha kuunganisha watu.
Pamoja na mafanikio pia kuna changamoto na baadhi ya mambo ambayo yamekuwa magumu kwake, mojawapo anasema ni “msiba wa Philemon Ndesamburo. Hili ni pigo kubwa kwangu, ni maumivu makubwa niliyapata.”
Ndesamburo alipofariki dunia Lema anasema “nilipwaya, nilichoka sana, nilishindwa sana na nilifikia kiwango cha kuomba chama nipumzike, lakini kwa kuwa ilionekana itakuwa na tafsiri mbaya, nikashawishiwa, nisipumzike”
Anasema Ndesamburo alikuwa rafiki, baba, bosi na msiri wake, hivyo kifo chake kilimuumiza na kumrudisha nyuma.